2 Mambo ya Nyakati Mlango 15 2nd Chronicles

2 Mambo ya Nyakati 15:1

Ndipo roho ya Mungu ikamjia Azaria mwana wa Odedi;

2 Mambo ya Nyakati 15:2

naye akatoka ili amlaki Asa, akamwambia, Nisikieni, Ee Asa, na Yuda wote na Benyamini; Bwana yu pamoja nanyi, mkiwa pamoja naye; nanyi mkimtafuta ataonekana kwenu; lakini mkimwacha atawaacha ninyi.

2 Mambo ya Nyakati 15:3

Basi tangu siku nyingi Israeli wamekuwa hawana Mungu wa kweli, wala hawana kuhani afundishaye, wala hawana torati;

2 Mambo ya Nyakati 15:4

lakini walipomgeukia Bwana, Mungu wa Israeli, katika msiba wao, na kumtafuta, akaonekana kwao.

2 Mambo ya Nyakati 15:5

Hata na zamani zile hakukuwa na amani kwake atokaye, wala kwake aingiaye, ila fadhaa kubwa juu yao wote wakaao katika nchi.

2 Mambo ya Nyakati 15:6

Wakavunjika-vunjika, taifa juu ya taifa, na mji juu ya mji; kwani Mungu aliwafadhaisha kwa shida zote.

2 Mambo ya Nyakati 15:7

Nanyi jipeni nguvu, wala mikono yenu isilegee; kwa maana kazi yenu itakuwa na ijara.

2 Mambo ya Nyakati 15:8

Naye Asa alipoyasikia maneno hayo, yaani, unabii wa mwana wa Odedi nabii, akatiwa nguvu, akayaondolea mbali machukizo yote katika nchi ya Yuda na Benyamini, na katika miji aliyoitwaa milimani mwa Efraimu; akaifanyiza tena madhabahu ya Bwana, iliyokuwako mbele ya ukumbi wa Bwana.

2 Mambo ya Nyakati 15:9

Akakusanya Yuda wote na Benyamini, na hao wageni waliokaa kwao, wa Efraimu, na wa Manase, na wa Simeoni; kwa kuwa walimwangukia wengi katika Israeli, walipoona kwamba Bwana, Mungu wake, alikuwa pamoja naye.

2 Mambo ya Nyakati 15:10

Basi wakakusanyika huko Yerusalemu mwezi wa tatu, katika mwaka wa kumi na tano wa kumiliki kwake Asa.

2 Mambo ya Nyakati 15:11

Wakamchinjia Bwana siku ile, katika nyara walizozileta, dhabihu za ng'ombe mia saba, na kondoo elfu saba.

2 Mambo ya Nyakati 15:12

Wakafanya agano, ya kuwa watamtafuta Bwana, Mungu wa baba zao, kwa mioyo yao yote, na kwa roho zao zote;

2 Mambo ya Nyakati 15:13

na ya kwamba ye yote asiyemtafuta Bwana, Mungu wa Israeli, atauawa, akiwa mdogo au mkubwa, kwamba ni mwanamume au mwanamke.

2 Mambo ya Nyakati 15:14

Wakamwapia Bwana kwa sauti kuu, na kwa kelele, na kwa mapanda, na kwa baragumu.

2 Mambo ya Nyakati 15:15

Na Yuda wote wakakifurahia kile kiapo; kwani wameapa kwa moyo wao wote, na kumtafuta kwa mapenzi yao pia; naye ameonekana kwao; naye Bwana akawastarehesha pande zote.

2 Mambo ya Nyakati 15:16

Hata na Maaka mamaye Asa, mfalme akamwondolea daraja yake asiwe malkia, kwa kuwa amefanya sanamu ya kuchukiza kwa Ashera; basi Asa akaikata sanamu yake, akaiponda, akaiteketeza penye kijito cha Kidroni.

2 Mambo ya Nyakati 15:17

Lakini mahali pa juu hapakuondolewa katika Israeli; ila moyo wake Asa ulikuwa mkamilifu siku zake zote.

2 Mambo ya Nyakati 15:18

Akavileta nyumbani mwa Mungu vitu alivyovitakasa babaye, na vile alivyovitakasa mwenyewe, fedha, na dhahabu, na vyombo.

2 Mambo ya Nyakati 15:19

Wala hapakuwa na vita tena hata mwaka wa thelathini na tano wa kutawala kwake Asa.