2 Mambo ya Nyakati Mlango 10 2nd Chronicles

2 Mambo ya Nyakati 10:1

Rehoboamu akaenda Shekemu; maana Israeli wote walikuwa wamekuja Shekemu, ili wamfanye mfalme.

2 Mambo ya Nyakati 10:2

Ikawa Yeroboamu mwana wa Nebati aliposikia, (maana alikuwako Misri, ambako amekimbilia mbele ya mfalme Sulemani), Yeroboamu akarudi kutoka Misri.

2 Mambo ya Nyakati 10:3

Wakapeleka ujumbe, wakamwita, Yeroboamu akaja na Israeli wote, wakamwambia Rehoboamu, wakasema,

2 Mambo ya Nyakati 10:4

Baba yako alilifanya zito kongwa letu; basi sasa upunguze utumwa mgumu wa baba yako, na kongwa lake zito alilotutwika, nasi tutakutumikia.

2 Mambo ya Nyakati 10:5

Akawaambia, Mnirudie baada ya siku tatu. Watu wakaenda zao.

2 Mambo ya Nyakati 10:6

Mfalme Rehoboamu akataka shauri kwa wazee, waliosimama mbele ya Sulemani baba yake, alipokuwa hai bado, akasema, Mwanipa shauri gani la kuwajibu watu hawa?

2 Mambo ya Nyakati 10:7

Wakamwambia, wakasema, Ukiwa mwema kwao watu hawa, na kuwapendeza, na kuwaambia maneno mazuri, ndipo watakapokuwa watumishi wako siku zote.

2 Mambo ya Nyakati 10:8

Lakini akaliacha shauri lile la wazee walilompa, akataka shauri kwa wale vijana waliokua pamoja naye, waliosimama mbele yake.

2 Mambo ya Nyakati 10:9

Akawaambia, Je! Mwanipa shauri gani la kuwajibu watu hawa, waliosema nami, wakisema, Utufanyie jepesi kongwa alilotutwika baba yako.

2 Mambo ya Nyakati 10:10

Na wale vijana waliokua pamoja naye wakamwambia, wakasema, Uwaambie hivi watu wale waliosema nawe, wakinena, Baba yako alilifanya zito kongwa letu, lakini wewe tufanyie jepesi; uwaambie hivi, Kidole changu cha mwisho ni kinene kuliko kiuno cha baba yangu.

2 Mambo ya Nyakati 10:11

Basi kama baba yangu aliwatwika kongwa zito, mimi nitaongeza kongwa lenu; baba yangu akiwapiga kwa mijeledi, lakini mimi nitawapiga kwa nge.

2 Mambo ya Nyakati 10:12

Basi Yeroboamu na watu wote wakamjia Rehoboamu siku ya tatu, kama mfalme alivyoamuru, akisema, Mnirudie siku ya tatu.

2 Mambo ya Nyakati 10:13

Mfalme akawajibu kwa ukali; mfalme Rehoboamu akaliacha shauri la wazee, akasema nao kwa shauri la vijana,

2 Mambo ya Nyakati 10:14

akinena, Baba yangu aliwafanyia kongwa zito, nami nitawaongezea; baba yangu aliwapiga kwa mijeledi, lakini mimi nitawapiga kwa nge.

2 Mambo ya Nyakati 10:15

Basi mfalme hakuwasikia wale watu; maana jambo hili lilitoka kwa Mungu, ili alithibitishe neno lake alilomwambia Yeroboamu mwana wa Nebati kwa mkono wa Ahiya Mshiloni.

2 Mambo ya Nyakati 10:16

Basi Israeli wote walipoona ya kuwa mfalme hawasikilizi, watu wakamjibu mfalme, wakasema, Tuna sehemu gani katika Daudi? Wala hatuna urithi katika mwana wa Yese; nendeni zenu hemani kwenu, enyi Israeli, kila mtu; sasa itunze nyumba yako mwenyewe, Daudi. Basi wakaenda zao Israeli wote hemani kwao.

2 Mambo ya Nyakati 10:17

Lakini kwa habari za wana wa Israeli waliokaa katika miji ya Yuda, Rehoboamu alitawala juu yao.

2 Mambo ya Nyakati 10:18

Ndipo mfalme Rehoboamu akamtuma Adoramu, msimamizi wa shokoa; nao wana wa Israeli wakamtupia mawe, hata akafa. Mfalme Rehoboamu akafanya haraka kupanda garini mwake, ili akimbilie Yerusalemu.

2 Mambo ya Nyakati 10:19

Hivyo Israeli wakaasi juu ya nyumba ya Daudi, hata leo.