2 Mambo ya Nyakati Mlango 28 2nd Chronicles

2 Mambo ya Nyakati 28:1

Ahazi alikuwa na umri wa miaka ishirini alipoanza kutawala; akatawala katika Yerusalemu miaka kumi na sita; wala hakufanya yaliyo ya adili machoni pa Bwana, kama Daudi babaye;

2 Mambo ya Nyakati 28:2

bali akaziendea njia za wafalme wa Israeli, akawafanyizia mabaali sanamu za kusubu.

2 Mambo ya Nyakati 28:3

Tena akafukiza uvumba katika bonde la mwana wa Hinomu, akawateketeza wanawe motoni, sawasawa na machukizo ya mataifa, aliowafukuza Bwana mbele ya wana wa Israeli.

2 Mambo ya Nyakati 28:4

Akatoa dhabihu na kufukiza uvumba katika mahali pa juu, na vilimani, na chini ya kila mti wenye majani mabichi.

2 Mambo ya Nyakati 28:5

Kwa hiyo Bwana, Mungu wake, akamtia mkononi mwa mfalme wa Shamu; wakampiga, wakachukua wa watu wake wafungwa wengi sana, wakawaleta Dameski. Tena akatiwa mkononi mwa mfalme wa Israeli, aliyempiga mapigo makuu.

2 Mambo ya Nyakati 28:6

Kwa kuwa Peka mwana wa Remalia akawaua katika Yuda siku moja watu mia na ishirini elfu, mashujaa wote; kwa sababu walikuwa wamemwacha Bwana, Mungu wa baba zao.

2 Mambo ya Nyakati 28:7

Naye Zikri, mtu hodari wa Efraimu, akawaua Maaseya mwana wa mfalme, na Azrikamu mkuu wa nyumba, na Elkana, aliyekuwa wa pili wake mfalme.

2 Mambo ya Nyakati 28:8

Wana wa Israeli wakachukua wa ndugu zao wafungwa mia mbili elfu, wanawake, na wana, na binti, pia wakachukua kwao nyara nyingi, wakazileta nyara Samaria.

2 Mambo ya Nyakati 28:9

Lakini kulikuwako huko nabii wa Bwana, jina lake aliitwa Odedi; akatoka kuwalaki jeshi waliokuja Samaria, akawaambia, Angalieni, kwa kuwa Bwana, Mungu wa baba zenu, aliwakasirikia Yuda, yeye amewatia mikononi mwenu, nanyi mmewaua kwa ghadhabu iliyofikia mbinguni.

2 Mambo ya Nyakati 28:10

Na sasa mwanuia kuwatawala wana wa Yuda na Yerusalemu, wawe kwenu watumwa na wajakazi; lakini ninyi nanyi je! Hamna hatia zenu wenyewe juu ya Bwana, Mungu wenu?

2 Mambo ya Nyakati 28:11

Haya, nisikieni mimi basi, mwarudishe wafungwa, mliowachukua mateka wa ndugu zenu; kwa maana ghadhabu ya Bwana iliyo kali i juu yenu.

2 Mambo ya Nyakati 28:12

Ndipo wakaondoka juu ya hao waliotoka vitani baadhi ya wakuu wa wana wa Efraimu, Azaria, mwana wa Yohanani, na Berekia mwana wa Meshilemothi, na Yehizkia mwana wa Shalumu, na Amasa mwana wa Hadlai,

2 Mambo ya Nyakati 28:13

wakawaambia, Hamtawaleta wafungwa humo; kwa sababu mnayanuia yatakayotutia hatiani mbele za Bwana, kuongeza dhambi zetu, na hatia yetu; maana hatia yetu ni kubwa, na ghadhabu kali ipo juu ya Israeli.

2 Mambo ya Nyakati 28:14

Basi watu wenye silaha wakawaacha wafungwa na nyara mbele ya wakuu na kusanyiko lote.

2 Mambo ya Nyakati 28:15

Wakaondoka wale watu waliotajwa majina yao, wakawatwaa wafungwa, wakawavika kwa zile nyara wote wao waliokuwa uchi, wakawapa mavazi na viatu, wakawalisha, wakawanywesha, wakawatia mafuta, wakawapandisha waliokuwa dhaifu miongoni mwao juu ya punda wakawaleta Yeriko, mji wa mitende, kwa ndugu zao; kisha wakarudi Samaria.

2 Mambo ya Nyakati 28:16

Wakati ule mfalme Ahazi akatuma wajumbe kwa mfalme wa Ashuru ili amsaidie.

2 Mambo ya Nyakati 28:17

Kwa kuwa Waedomi walikuwa wamekuja tena, na kuwapiga Yuda, na kuwachukua wafungwa.

2 Mambo ya Nyakati 28:18

Wafilisti pia walikuwa wameingia miji ya Shefela, na ya Negebu ya Yuda, nao wameutwaa Beth-shemeshi, na Ayaloni, na Gederothi, na Soko pamoja na miji yake, na Timna pamoja na miji yake, na Gimzo pia na miji yake; wakakaa humo.

2 Mambo ya Nyakati 28:19

Kwa maana Bwana aliinamisha Yuda kwa ajili ya Ahazi mfalme wa Israeli; kwa kuwa yeye aliwafanyia Yuda aibu, na kumwasi Bwana mno.

2 Mambo ya Nyakati 28:20

Na Tiglath-pileseri mfalme wa Ashuru akamjia, akamfadhaisha, asimtie nguvu kwa lo lote.

2 Mambo ya Nyakati 28:21

Kwa maana Ahazi alitwaa sehemu katika nyumba ya Bwana, na katika nyumba ya mfalme, na ya wakuu, akampa mfalme wa Ashuru; asisaidiwe na jambo hilo.

2 Mambo ya Nyakati 28:22

Na wakati alipofadhaishwa, akazidi kumwasi Bwana, huyo mfalme Ahazi.

2 Mambo ya Nyakati 28:23

Kwani akaitolea dhabihu miungu ya Dameski iliyompiga, akasema, Kwa sababu miungu ya wafalme wa Shamu imewasaidia wao, mimi nitaitolea dhabihu, ili inisaidie mimi. Lakini ndiyo iliyomwangamiza yeye na Israeli wote.

2 Mambo ya Nyakati 28:24

Tena Ahazi akakusanya vyombo vyote vya nyumba ya Mungu, akavikata vipande vipande vyombo vya nyumba ya Mungu, akaifunga milango ya nyumba ya Bwana; akajifanyizia madhabahu katika kila pembe ya Yerusalemu.

2 Mambo ya Nyakati 28:25

Na katika kila mji wa Yuda akafanya mahali pa juu pa kuifukizia miungu mingine uvumba, akamkasirisha Bwana, Mungu wa babaze.

2 Mambo ya Nyakati 28:26

Basi mambo yake yote yaliyosalia, na njia zake zote, za kwanza na za mwisho, tazama, yameandikwa katika kitabu cha wafalme wa Yuda na Israeli.

2 Mambo ya Nyakati 28:27

Ahazi akalala na babaze, wakamzika mjini, yaani, Yerusalemu; maana hawakumleta makaburini mwa wafalme wa Israeli; na Hezekia mwanawe akatawala mahali pake.