2 Mambo ya Nyakati Mlango 19 2nd Chronicles

2 Mambo ya Nyakati 19:1

Yehoshafati mfalme wa Yuda akarudi Yerusalemu nyumbani kwake kwa amani.

2 Mambo ya Nyakati 19:2

Yehu mwana wa Hanani mwonaji akatoka kwenda kumlaki, akamwambia mfalme Yehoshafati, Je! Imekupasa kuwasaidia waovu, na kuwapenda wamchukiao Bwana? Kwa ajili ya hayo ghadhabu i juu yako itokayo kwa Bwana.

2 Mambo ya Nyakati 19:3

Walakini yameonekana mema ndani yako, kwa kuwa umeyaondoa maashera katika nchi, na moyo wako umeukaza kumtafuta Mungu.

2 Mambo ya Nyakati 19:4

Na Yehoshafati akakaa Yerusalemu; akatoka tena kwenda kati ya watu toka Beer-sheba mpaka milima ya Efraimu, akawarudisha kwa Bwana, Mungu wa baba zao.

2 Mambo ya Nyakati 19:5

Akasimamisha makadhi katika nchi, katikati ya miji yote yenye maboma ya Yuda, mji kwa mji;

2 Mambo ya Nyakati 19:6

akawaambia hao makadhi, Angalieni myafanyayo; kwa kuwa hammfanyii mwanadamu hukumu, ila Bwana; naye yupo pamoja nanyi katika neno la hukumu.

2 Mambo ya Nyakati 19:7

Basi sasa hofu ya Bwana na iwe juu yenu; angalieni mkaifanye; kwa maana kwa Bwana, Mungu wetu, hapana uovu, wala kujali nafsi za watu, wala kupokea zawadi.

2 Mambo ya Nyakati 19:8

Tena katika Yerusalemu Yehoshafati akasimamisha wa Walawi na makuhani, na wakuu wa mbari za mababa wa Israeli wawe kwa hukumu ya Bwana, na kwa mateto. Nao wakarudi Yerusalemu.

2 Mambo ya Nyakati 19:9

Akawaagiza, akasema, Ndivyo mtakavyotenda kwa hofu ya Bwana, kwa uaminifu, na kwa moyo kamili.

2 Mambo ya Nyakati 19:10

Na kila mara watakapowajia na teto ndugu zenu wakaao mijini mwao, kati ya damu na damu, kati ya torati na amri, sheria na hukumu, mtawaonya, wasiingie hatiani mbele za Bwana, mkajiliwa na ghadhabu ninyi na ndugu zenu; fanyeni haya wala hamtakuwa na hatia.

2 Mambo ya Nyakati 19:11

Tena angalieni, Amaria, kuhani mkuu, yu juu yenu kwa maneno yote ya Bwana; naye Zebadia, mwana wa Ishmaeli, jemadari wa nyumba ya Yuda, kwa maneno yote ya mfalme; Walawi nao watakuwa wasimamizi mbele yenu. Jitieni nguvu, mtende, naye Bwana awe pamoja nao walio wema