2 Mambo ya Nyakati Mlango 7 2nd Chronicles

2 Mambo ya Nyakati 7:1

Basi Sulemani alipokwisha maombi hayo, moto ukashuka kutoka mbinguni, ukateketeza sadaka ya kuteketezwa na dhabihu; utukufu wa Bwana ukaijaza nyumba.

2 Mambo ya Nyakati 7:2

Wala makuhani hawakuweza kuingia nyumbani mwa Bwana, kwa kuwa utukufu wa Bwana umeijaza nyumba ya Bwana.

2 Mambo ya Nyakati 7:3

Wakatazama wana wa Israeli wote, uliposhuka ule moto, utukufu wa Bwana ulipokuwapo juu ya nyumba; wakasujudu kifulifuli hata nchi sakafuni, wakaabudu, wakamshukuru Bwana, wakisema, Kwa kuwa ni mwema; kwa maana fadhili zake ni za milele.

2 Mambo ya Nyakati 7:4

Ndipo mfalme na watu wote wakatoa dhabihu mbele za Bwana.

2 Mambo ya Nyakati 7:5

Mfalme Sulemani akatoa sadaka ya ng'ombe ishirini na mbili elfu, na kondoo mia na ishirini elfu. Ndivyo mfalme na watu wote walivyoifanya wakfu nyumba ya Mungu.

2 Mambo ya Nyakati 7:6

Wakasimama makuhani sawasawa na malinzi yao; Walawi nao pamoja na vinanda vya Bwana, alivyovifanya Daudi mfalme, ili kumshukuru Bwana, kwa maana fadhili zake ni za milele, hapo aliposifu Daudi kwa mikono yao; nao makuhani wakapiga panda mbele yao; nao Israeli wote wakasimama.

2 Mambo ya Nyakati 7:7

Tena Sulemani akaitakasa behewa katikati, iliyokuwa mbele ya nyumba ya Bwana; kwa kuwa hapo ndipo alipotoa sadaka za kuteketezwa, na mafuta ya sadaka za amani; kwa sababu ile madhabahu ya shaba aliyoifanya Sulemani haikutosha kuzipokea sadaka ya kuteketezwa, na sadaka ya unga, na mafuta.

2 Mambo ya Nyakati 7:8

Basi, wakati ule Sulemani akafanya sikukuu, na Israeli wote pamoja naye, kusanyiko kubwa sana, toka maingilio ya Hamathi mpaka kijito cha Misri, muda wa siku saba.

2 Mambo ya Nyakati 7:9

Hata siku ya nane wakaita kusanyiko la makini; kwa maana walishika kuitakasa madhabahu siku saba, na sikukuu siku saba.

2 Mambo ya Nyakati 7:10

Akawaruhusu watu waende hemani kwao siku ya ishirini na tatu, ya mwezi wa saba, wakifurahi na kuchangamka mioyoni kwa wema wote Bwana aliomfanyia Daudi, na Sulemani, na Israeli watu wake.

2 Mambo ya Nyakati 7:11

Hivyo Sulemani akaimaliza nyumba ya Bwana, na nyumba ya mfalme; na yote yaliyomwingia Sulemani moyoni ayafanye nyumbani mwa Bwana, na nyumbani mwake mwenyewe, akayafanikisha.

2 Mambo ya Nyakati 7:12

Bwana akamtokea Sulemani usiku, akamwambia, Nimesikia uliyoyaomba, na mahali hapa nimejichagulia kuwa nyumba ya dhabihu.

2 Mambo ya Nyakati 7:13

Nikizifunga mbingu isiwe mvua, tena nikiamuru nzige kula nchi, au nikiwapelekea watu wangu tauni;

2 Mambo ya Nyakati 7:14

ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao.

2 Mambo ya Nyakati 7:15

Sasa macho yangu yatafumbuka, na masikio yangu yatasikiliza maombi ya watu waombao mahali hapa.

2 Mambo ya Nyakati 7:16

Maana sasa nimeichagua nyumba hii na kuitakasa, ili kwamba jina langu lipate kuwako huko milele; yatakuwako na macho yangu, na moyo wangu daima.

2 Mambo ya Nyakati 7:17

Nawe, ukienda mbele yangu kama alivyokwenda Daudi baba yako, ufanye sawasawa na yote niliyokuamuru, na kuzishika sheria zangu na hukumu zangu;

2 Mambo ya Nyakati 7:18

ndipo nitakithibitisha kiti cha enzi cha ufalme wako, kama nilivyoagana na Daudi baba yako, nikisema, Hutakosa kuwa na mtu wa kutawala katika Israeli.

2 Mambo ya Nyakati 7:19

Lakini mkigeuka, na kuziacha sheria zangu na amri zangu nilizoweka mbele yenu, mkienda, na kuitumikia miungu mingine, na kuiabudu;

2 Mambo ya Nyakati 7:20

ndipo nitawang'oa katika nchi yangu niliyowapa; na nyumba hii niliyoitakasa kwa jina langu, nitaiondosha itoke mbele zangu, nami nitaifanya kuwa mithali na tukano katikati ya watu wote.

2 Mambo ya Nyakati 7:21

Na nyumba hii, iliyo juu, kila apitaye ataona ushangao, atasema, Mbona Bwana ameitendea hivi nchi hii, na nyumba hii?

2 Mambo ya Nyakati 7:22

Nao watajibu, Kwa sababu walimwacha Bwana, Mungu wa baba zao, aliyewaleta kutoka nchi ya Misri, wakashikamana na miungu mingine, wakaiabudu, na kuitumikia; kwa hiyo ameyaleta mabaya haya yote juu yao.