2 Mambo ya Nyakati Mlango 27 2nd Chronicles

2 Mambo ya Nyakati 27:1

Yothamu alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala; akatawala katika Yerusalemu miaka kumi na sita; na jina la mamaye aliitwa Yerusha binti Sadoki.

2 Mambo ya Nyakati 27:2

Akafanya yaliyo ya adili machoni pa Bwana, sawasawa na yote aliyoyafanya Uzia babaye; isipokuwa hakuingia hekaluni mwa Bwana. Lakini watu walikuwa wakali kufanya maovu.

2 Mambo ya Nyakati 27:3

Ndiye aliyelijenga lango la juu la nyumba ya Bwana, na juu ya ukuta wa Ofeli akajenga sana.

2 Mambo ya Nyakati 27:4

Tena akajenga miji katika milima ya Yuda, na mwituni akajenga ngome na minara.

2 Mambo ya Nyakati 27:5

Kisha akapigana na mfalme wa wana wa Amoni, akawashinda. Na wana wa Amoni wakampa mwaka ule ule talanta mia za fedha, na kori elfu kumi za ngano, na elfu kumi za shayiri. Hayo ndiyo waliyomtolea wana wa Amoni, mwaka wa pili pia, na mwaka wa tatu.

2 Mambo ya Nyakati 27:6

Basi Yothamu akawa na nguvu, kwa kuwa alizitengeneza njia zake mbele za Bwana, Mungu wake.

2 Mambo ya Nyakati 27:7

Na mambo yote ya Yothamu yaliyosalia, na vita vyake vyote, na njia zake, tazama, yameandikwa katika kitabu cha wafalme wa Israeli na Yuda.

2 Mambo ya Nyakati 27:8

Alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala; akatawala miaka kumi na sita huko Yerusalemu.

2 Mambo ya Nyakati 27:9

Yothamu akalala na babaze, wakamzika katika mji wa Daudi; na Ahazi mwanawe akatawala mahali pake.