2 Mambo ya Nyakati Mlango 36 2nd Chronicles

2 Mambo ya Nyakati 36:1

Watu wa nchi wakamtwaa Yehoahazi mwana wa Yosia, wakamtawaza awe mfalme katika Yerusalemu badala ya babaye.

2 Mambo ya Nyakati 36:2

Yehoahazi alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitatu alipoanza kutawala; akatawala huko Yerusalemu miezi mitatu.

2 Mambo ya Nyakati 36:3

Naye mfalme wa Misri akamwondoa katika Yerusalemu, akaitoza nchi talanta mia za fedha, na talanta moja ya dhahabu.

2 Mambo ya Nyakati 36:4

Mfalme wa Misri akamtawaza Eliakimu nduguye awe mfalme juu ya Yuda na Yerusalemu, akambadilisha jina lake kuwa Yehoyakimu. Neko akamtwaa Yehoahazi nduguye, akamchukua mpaka Misri.

2 Mambo ya Nyakati 36:5

Yehoyakimu alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala; akatawala katika Yerusalemu miaka kumi na mmoja; akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana, Mungu wake.

2 Mambo ya Nyakati 36:6

Juu yake akakwea Nebukadreza,

2 Mambo ya Nyakati 36:7

Nebukadreza akachukua baadhi ya vyombo vya nyumba ya Bwana mpaka Babeli, akavitia katika hekalu lake huko Babeli.

2 Mambo ya Nyakati 36:8

Basi mambo yote ya Yehoyakimu yaliyosalia, na machukizo yake aliyoyafanya, nayo yaliyoonekana kwake, tazama, yameandikwa katika kitabu cha wafalme wa Israeli na Yuda; na Yekonia

2 Mambo ya Nyakati 36:9

Yekonia alikuwa na umri wa miaka kumi na minane alipoanza kutawala; akatawala katika Yerusalemu miezi mitatu na siku kumi; akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana.

2 Mambo ya Nyakati 36:10

Mwaka ulipokwisha, Nebukadreza akatuma wajumbe, akamchukua mpaka Babeli; pamoja na vyombo vya thamani vya nyumba ya Bwana; akamtawaza Sedekia nduguye awe mfalme juu ya Yuda na Yerusalemu.

2 Mambo ya Nyakati 36:11

Sedekia alikuwa na umri wa miaka ishirini na mmoja, alipoanza kutawala; akatawala katika Yerusalemu miaka kumi na mmoja;

2 Mambo ya Nyakati 36:12

akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana, Mungu wake; wala hakujinyenyekesha mbele ya Yeremia nabii aliponena kwa kinywa cha Bwana.

2 Mambo ya Nyakati 36:13

Tena akamwasi mfalme Nebukadreza, aliyemwapisha kwa Mungu; lakini akajifanyia shingo ngumu, akajitia moyo nguvu asimgeukie Bwana, Mungu wa Israeli.

2 Mambo ya Nyakati 36:14

Na zaidi ya hayo wakuu wote wa makuhani, na watu, wakakosa mno sawasawa na machukizo yote ya mataifa; wakainajisi nyumba ya Bwana aliyoitakasa katika Yerusalemu.

2 Mambo ya Nyakati 36:15

Naye Bwana, Mungu wa baba zao, akatuma kwao kwa mikono ya wajumbe wake, akiondoka mapema, na kutuma; kwa sababu aliwahurumia watu wake, na makao yake;

2 Mambo ya Nyakati 36:16

lakini waliwadhihaki wajumbe wa Mungu, na kuyadharau maneno yake, na kuwacheka manabii wake, hata ilipozidi ghadhabu ya Bwana juu ya watu wake, hata kusiwe na kuponya.

2 Mambo ya Nyakati 36:17

Kwa hiyo akaleta juu yao mfalme wa Wakaldayo, aliyewaua vijana wao kwa upanga nyumbani mwa patakatifu pao, asiwahurumie kijana wala mwanamwali, mzee wala mkongwe; akawatia wote mkononi mwake.

2 Mambo ya Nyakati 36:18

Na vyombo vyote vya nyumba ya Mungu, vikubwa kwa vidogo, na hazina za nyumba ya Bwana, na hazina za mfalme, na za wakuu wake; vyote pia akavileta Babeli.

2 Mambo ya Nyakati 36:19

Wakaiteketeza nyumba ya Mungu, wakaubomoa ukuta wa Yerusalemu, wakayateketeza kwa moto majumba yake yote, wakaviharibu vyombo vyake vyote vya thamani.

2 Mambo ya Nyakati 36:20

Na wale waliookoka na upanga akawachukua mpaka Babeli; wakamtumikia yeye na wanawe hata kulipoingia milki ya Uajemi;

2 Mambo ya Nyakati 36:21

ili kulitimiza neno la Bwana kwa kinywa cha Yeremia, hata nchi itakapofurahia sabato zake; kwa maana siku zote ilipokaa ukiwa ilishika sabato, kutimiza miaka sabini.

2 Mambo ya Nyakati 36:22

Ikawa katika mwaka wa kwanza wa Koreshi, mfalme wa Uajemi, ili kwamba neno la Bwana alilolisema kwa kinywa cha Yeremia lipate kutimizwa, Bwana akamwamsha roho yake Koreshi, mfalme wa Uajemi, hata akapiga mbiu katika ufalme wake wote, akaiandika pia, akisema,

2 Mambo ya Nyakati 36:23

Koreshi, mfalme wa Uajemi asema hivi; Bwana, Mungu wa mbinguni, amenipa falme zote za dunia; naye ameniagiza nimjengee nyumba katika Yerusalemu, ulioko Yuda. Basi kila mtu katika ninyi nyote mlio watu wake, Bwana, Mungu wake, na awe pamoja naye, na akwee.