2 Mambo ya Nyakati Mlango 6 2nd Chronicles

2 Mambo ya Nyakati 6:1

Ndipo Sulemani akanena, Bwana alisema ya kwamba atakaa katika giza nene.

2 Mambo ya Nyakati 6:2

Lakini nimekujengea nyumba ya kukaa, iwe mahali pa makao yako milele.

2 Mambo ya Nyakati 6:3

Mfalme akageuza uso wake, akawabarikia mkutano wote wa Israeli; na mkutano wote wa Israeli wakasimama.

2 Mambo ya Nyakati 6:4

Akasema, Bwana, Mungu wa Israeli, ahimidiwe, aliyenena kwa kinywa chake na baba yangu Daudi, akalitimiza kwa mikono yake, akasema,

2 Mambo ya Nyakati 6:5

Tangu siku ile nilipowatoa watu wangu katika nchi ya Misri, sikuchagua mji wo wote wa kabila zote za Israeli ili kujenga nyumba, jina langu liwe humo; wala sikumchagua mtu ye yote awe mkuu juu ya watu wangu Israeli;

2 Mambo ya Nyakati 6:6

lakini nimeuchagua Yerusalemu, jina langu liwe humo; na Daudi nimemchagua awe juu ya watu wangu Israeli.

2 Mambo ya Nyakati 6:7

Basi ilikuwa moyoni mwake Daudi, baba yangu, kujenga nyumba kwa jina la Bwana, Mungu wa Israeli.

2 Mambo ya Nyakati 6:8

Lakini Bwana akamwambia Daudi baba yangu, Kwa kuwa ilikuwa moyoni mwako kujenga nyumba kwa jina langu, ulifanya vema kuwaza hivi moyoni mwako;

2 Mambo ya Nyakati 6:9

lakini si wewe utakayeijenga nyumba hiyo; ila mwanao atakayetoka katika viuno vyako, yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa jina langu.

2 Mambo ya Nyakati 6:10

Basi Bwana amelitimiza neno lile alilolinena; nami nimesimama mahali pa Daudi baba yangu, na kuketi katika kiti cha enzi cha Israeli, kama Bwana alivyoahidi, nami nimeijenga nyumba kwa jina la Bwana, Mungu wa Israeli.

2 Mambo ya Nyakati 6:11

Ndimo nilimoliweka hilo sanduku, ambalo ndani yake mna agano la Bwana, alilolifanya na wana wa Israeli.

2 Mambo ya Nyakati 6:12

Akasimama mbele ya madhabahu ya Bwana, machoni pa mkutano wote wa Israeli, akainyosha mikono;

2 Mambo ya Nyakati 6:13

(maana Sulemani alikuwa amefanya mimbari ya shaba, urefu wake mikono mitano, na upana wake mikono mitano, na kwenda juu kwake mikono mitatu, na kuisimamisha katikati ya ua; akasimama juu yake, akapiga magoti mbele ya mkutano wote wa Israeli, akaikunjua mikono yake kuelekea mbinguni);

2 Mambo ya Nyakati 6:14

akasema, Ee Bwana, Mungu wa Israeli, hakuna Mungu kama wewe, mbinguni, wala duniani; ushikaye maagano na rehema kwa watumishi wako, waendao mbele zako kwa moyo wao wote;

2 Mambo ya Nyakati 6:15

uliyemtimizia mtumishi wako Daudi, baba yangu, ahadi uliyomwahidi; naam, ulinena kwa kinywa chako, ukayatimiza kwa mkono wako, kama ilivyo leo.

2 Mambo ya Nyakati 6:16

Sasa, Ee Bwana, Mungu wa Israeli, umfikilizie mtumishi wako Daudi, baba yangu, ahadi uliyomwahidia, ukisema, Hutakosa kuwa na mtu machoni pangu, wa kuketi katika kiti cha enzi cha Israeli; wakiwa tu watoto wako wataiangalia njia yao, ili kuiendea torati yangu, kama wewe ulivyokwenda mbele zangu.

2 Mambo ya Nyakati 6:17

Basi sasa, Ee Bwana, Mungu wa Israeli, ulithibitishe neno lako, ulilomwambia mtumishi wako Daudi.

2 Mambo ya Nyakati 6:18

Lakini Mungu je! Yamkini atakaa na watu duniani? Tazama, mbingu na mbingu za mbingu za mbingu hazikutoshi; siuze nyumba hii niliyoijenga!

2 Mambo ya Nyakati 6:19

Walakini umwangalie mtumwa wako anayoyaomba, na kusihi, Ee Bwana, Mungu wangu, usikie kilio na maombi anayoyaomba mtumwa wako mbele zako;

2 Mambo ya Nyakati 6:20

ili macho yako yafumbuke kwa nyumba hii mchana na usiku, mahali uliponena, ndipo utakapoliweka jina lako; usikie maombi atakayoomba mtumwa wako, akikabili mahali hapa.

2 Mambo ya Nyakati 6:21

Uyasikie atakayosihi mtumwa wako, na watu wako Israeli, watakapoomba wakikabili mahali hapa; naam, usikie toka makaoni mwako, toka mbinguni, nawe usikiapo, samehe.

2 Mambo ya Nyakati 6:22

Ikiwa mtu amemkosea mwenzake, akitiwa kiapo, aapishwe, naye akija na kuapa hapa mbele ya madhabahu yako nyumbani humu;

2 Mambo ya Nyakati 6:23

basi, usikie mbinguni, ukatende, ukawahukumu watumwa wako; ukimlipiza mwovu, kumpatilizia njia yake kichwani; ukamfanyie haki mwenye haki, ukimjalia kwa kadiri ya haki yake.

2 Mambo ya Nyakati 6:24

Ikiwa watu wako Israeli wamepigwa mbele ya adui zao, kwa sababu wamekukosa wewe; kama wakirejea kwako, na kulikiri jina lako, wakikuomba na kukusihi nyumbani humu;

2 Mambo ya Nyakati 6:25

basi usikie huko mbinguni, ukaisamehe dhambi ya watu wako Israeli, na kuwarejeza tena katika nchi uliyowapa wao na baba zao.

2 Mambo ya Nyakati 6:26

Ikiwa mbingu zimefungwa, hata hakuna mvua, kwa sababu wamekukosa wewe; kama wakiomba wakikabili mahali hapa, na kulikiri jina lako, na kuiacha dhambi yao, uwatesapo;

2 Mambo ya Nyakati 6:27

basi usikie huko mbinguni, ukaisamehe dhambi ya watumwa wako, na ya watu wako Israeli; uwafundishapo njia njema iwapasayo waiendee; ukainyeshee mvua nchi yako, uliyowapa watu wako iwe urithi.

2 Mambo ya Nyakati 6:28

Ikiwa nchi imeingia njaa, au tauni, au ukosefu wa mvua, au ukungu, au nzige, au panzi; ikiwa adui wamewahusuru katika nchi ya miji yao, au ukiwapo msiba wo wote, au uele wo wote;

2 Mambo ya Nyakati 6:29

yo yote atakayoyaomba na kusihi mtu awaye yote, au watu wako Israeli wote pamoja, watakaojua kila mtu pigo lake mwenyewe, na msiba wake mwenyewe, akiinyoshea mikono nyumba hii;

2 Mambo ya Nyakati 6:30

basi usikie huko mbinguni, ukaapo, ukasamehe, ukampatilize kila mtu kwa kadiri ya njia zake zote; wewe umjuaye moyo; (maana wewe peke yako ndiwe uijuaye mioyo ya wanadamu);

2 Mambo ya Nyakati 6:31

ili wakuche wewe, waziendee njia zako, siku zote watakazoishi katika nchi uliyowapa baba zetu.

2 Mambo ya Nyakati 6:32

Hata na mgeni naye, asiyekuwa mmoja wa watu wako Israeli, atakapokuja kutoka nchi iliyo mbali sana kwa ajili ya jina lako kuu, na mkono wako ulio hodari, na mkono wako ulionyoshwa; hao watakapokuja na kuomba wakiielekea nyumba hii;

2 Mambo ya Nyakati 6:33

basi usikie huko mbinguni, toka makaoni mwako, ukatende yote atakayokuomba huyo mgeni; ili watu wote wa dunia wapate kulijua jina lako, na kukucha wewe, kama watu wako Israeli, tena wajue ya kuwa nyumba hii niliyoijenga imeitwa kwa jina lako.

2 Mambo ya Nyakati 6:34

Ikiwa watu wako wametoka kupigana na adui zao, utakakowatuma ko kote, wakikuomba kuuelekea mji huu uliouchagua, na nyumba hii niliyoijenga kwa jina lako;

2 Mambo ya Nyakati 6:35

basi uyasikie huko mbinguni wayaombayo, na kusihi, ukaitetee haki yao.

2 Mambo ya Nyakati 6:36

Wakikukosa, (maana hakuna mtu asiyekosa), hata uwakasirikie, na kuwatia mikononi mwa adui zao, wawahamishe, na kuwachukua mateka mpaka nchi iliyo mbali au iliyo karibu;

2 Mambo ya Nyakati 6:37

basi wakikumbuka katika nchi walikohamishwa, na kutubu, na kukusihi katika nchi ya uhamisho wao, wakisema, Tumekosa, tumetenda kwa ukaidi, tumefanya maovu;

2 Mambo ya Nyakati 6:38

wakurudiapo kwa mioyo yao yote, na kwa nia zao zote, katika nchi ya uhamisho wao, adui walikowahamisha, wakiomba na kuielekea nchi uliyowapa baba zao, na mji huu uliouchagua, na nyumba hii niliyoijenga kwa jina lako;

2 Mambo ya Nyakati 6:39

basi uyasikie toka mbinguni, toka makaoni mwako, wayaombayo, na kusihi, ukaitetee haki yao; ukawasamehe watu wako, waliokosa juu yako.

2 Mambo ya Nyakati 6:40

Na sasa, Ee Mungu wangu, macho yako yafumbuke, nakusihi, masikio yako yakasikilize maombi yaombwayo mahali hapa.

2 Mambo ya Nyakati 6:41

Sasa, Ee Bwana, Mungu, uondoke, uende kwenye raha yako, wewe na sanduku la nguvu zako; makuhani wako, Ee Bwana, Mungu, wavikwe wokovu, watakatifu wako na washangilie mema.

2 Mambo ya Nyakati 6:42

Ee Bwana, Mungu, usiurudishe nyuma uso wa masihi wako,uzikumbuke fadhili za Daudi mtumishi wako.