Kumbukumbu la Torati Mlango 4 Deuteronomy

Kumbukumbu la Torati 4:1

Na sasa, Ee Israeli, zisikilizeni amri na hukumu niwafundishazo, ili mzitende; mpate kuishi na kuingia na kuimiliki nchi awapayo Bwana, Mungu wa baba zenu.

Kumbukumbu la Torati 4:2

Msiliongeze neno niwaamurulo wala msilipunguze, mpate kuzishika amri za Bwana, Mungu wenu, niwaamuruzo.

Kumbukumbu la Torati 4:3

Macho yenu yameona aliyoyatenda Bwana kwa sababu ya Baal-peori; maana wote waliomfuata Baal-peori, Bwana, Mungu wako, amewaangamiza kutoka kati yako.

Kumbukumbu la Torati 4:4

Bali ninyi mlioambatana na Bwana, Mungu wenu, mnaishi kila mmoja wenu, hata leo.

Kumbukumbu la Torati 4:5

Angalieni nimewafundisha amri na hukumu, vile vile kama Bwana, Mungu wangu, alivyoniamuru, ili mzitende katika nchi mwingiayo ili kuimiliki.

Kumbukumbu la Torati 4:6

Zishikeni basi, mkazitende, maana hii ndiyo hekima yenu na akili zenu, machoni pa mataifa watakaozisikia amri hizi zote, nao watasema, Hakika taifa hili kubwa ni watu wenye hekima na akili.

Kumbukumbu la Torati 4:7

Kwa maana liko taifa gani kubwa, lililo na Mungu aliye karibu nao, kama Bwana, Mungu wetu, alivyo, kila tumwitapo?

Kumbukumbu la Torati 4:8

Tena liko taifa gani kubwa, lililo na amri na hukumu zenye haki kama torati hii yote, ninayoiweka mbele yenu leo.

Kumbukumbu la Torati 4:9

Lakini, jihadhari nafsi yako, ukailinde roho yako kwa bidii, usije ukayasahau mambo yale uliyoyaona kwa macho yako, yakaondoka moyoni mwako siku zote za maisha yako; bali uwajulishe watoto wako na watoto wa watoto wako;

Kumbukumbu la Torati 4:10

siku ile uliyosimama mbele za Bwana wako huko Horebu, Bwana aliponiambia, Nikusanyieni watu hawa, nami nitawasikizisha maneno yangu, ili wajifunze kunicha mimi siku zote watakazoishi duniani, wakapate na kuwafundisha watoto wao.

Kumbukumbu la Torati 4:11

Mkakaribia, mkasimama chini ya ule mlima; mlima ukawaka moto mpaka kati ya mbinguni, kwa giza na mawingu, na giza kuu.

Kumbukumbu la Torati 4:12

Bwana akasema nanyi kutoka kati ya moto; mkasikia sauti ya maneno, lakini hamkuona umbo lo lote; sauti tu.

Kumbukumbu la Torati 4:13

Akawahubiri agano lake, alilowaamuru kulitenda, yaani, zile amri kumi; akaziandika juu ya mbao mbili za mawe.

Kumbukumbu la Torati 4:14

Bwana akaniamuru wakati ule niwafundishe maagizo na hukumu, mpate kuzitenda katika nchi ile mtakayoivukia ili kuimiliki.

Kumbukumbu la Torati 4:15

Jihadharini nafsi zenu basi; maana hamkuona umbo la namna yo yote siku ile Bwana aliyosema nanyi kutoka kati ya moto;

Kumbukumbu la Torati 4:16

msije mkajiharibu nafsi zenu, mkajifanyia sanamu ya kuchonga, mfano wa sura yo yote, mfano wa mwanamume au mwanamke,

Kumbukumbu la Torati 4:17

mfano wa mnyama ye yote aliye duniani, au mfano wa ndege ye yote arukaye mbinguni,

Kumbukumbu la Torati 4:18

au mfano wa kitu cho chote kitambaacho juu ya ardhi, au mfano wa samaki ye yote aliye majini chini ya nchi;

Kumbukumbu la Torati 4:19

tena usije ukainua macho yako hata mbinguni, na ulionapo jua, na mwezi, na nyota, jeshi la mbinguni lote pia, ukashawishwa na kuviabudu, na kuvitumikia, ambavyo Bwana, Mungu wako amewagawanyia watu wote chini ya mbingu zote.

Kumbukumbu la Torati 4:20

Bali Bwana amewatwaa ninyi, na kuwatoa katika tanuu ya chuma, katika Misri, mpate kuwa watu wa urithi kwake, kama mlivyo leo hivi.

Kumbukumbu la Torati 4:21

Tena Bwana alinikasirikia kwa ajili yenu, akaapa ya kwamba sitavuka Yordani, na ya kwamba sitaingia nchi ile njema, awapayo Bwana, Mungu wenu, iwe urithi.

Kumbukumbu la Torati 4:22

Lakini mimi nitakufa katika nchi hii, sina ruhusa kuvuka Yordani; bali ninyi mtavuka, na kuimiliki nchi ile njema.

Kumbukumbu la Torati 4:23

Jihadharini nafsi zenu, msije mkalisahau agano la Bwana, Mungu wenu, alilolifanya nanyi, mkajifanyia sanamu ya kuchonga, mfano wa umbo la kitu cho chote ulichokatazwa na Bwana, Mungu wenu,

Kumbukumbu la Torati 4:24

kwa kuwa Bwana, Mungu wenu, ni moto ulao, Mungu mwenye wivu.

Kumbukumbu la Torati 4:25

Utakapozaa wana, na wana wa wana, mkisha kuwa katika nchi siku nyingi, mkajiharibu na kufanya sanamu ya kuchonga kwa umbo la kitu cho chote, mkafanya ambayo ni maovu machoni pa Bwana, Mungu wako, na kumtia hasira;

Kumbukumbu la Torati 4:26

nawashuhudizia mbingu na nchi hivi leo, kwamba karibu mtaangamia kabisa juu ya nchi mwivukiayo Yordani kuimiliki, hamtafanya siku zenu ziwe nyingi juu yake, ila mtaangamizwa kabisa.

Kumbukumbu la Torati 4:27

Na Bwana atawatawanya kati ya mataifa, nanyi mtasalia watu kidogo hesabu yenu kati ya makabila, mtakakopelekwa mbali na Bwana.

Kumbukumbu la Torati 4:28

Na huko mtatumikia miungu, kazi za mikono ya watu, miti na mawe, ambao hawaoni, wala hawasikii, hawali, wala hawanusi.

Kumbukumbu la Torati 4:29

Lakini huko, kama mkimtafuta Bwana, Mungu wako, utampata, ukimtafuta kwa moyo wako wote, na roho yako yote.

Kumbukumbu la Torati 4:30

Na wakati uwapo katika mashaka, ukiisha kupatwa na mambo haya yote, siku za mwisho, utamrudia Bwana, Mungu wako, na kuisikiza sauti yake;

Kumbukumbu la Torati 4:31

kwa kuwa Bwana, Mungu wako, ni Mungu wa rehema; hatakukosa wala kukuangamiza, wala hatalisahau agano la baba zako alilowaapia.

Kumbukumbu la Torati 4:32

Maana uliza sasa siku zilizopita, zilizokuwa kabla yako, tangu siku ile Mungu aliyoumba mwanadamu juu ya nchi, na toka pembe hii ya mbingu hata pembe hii, kwamba kumetukia neno lo lote kama neno hili kubwa, au kwamba kumesikiwa habari ya neno kama hili?

Kumbukumbu la Torati 4:33

Je! Watu wakati wo wote wameisikia sauti ya Mungu ikinena toka kati ya moto, kama wewe ulivyosikia, wasife?

Kumbukumbu la Torati 4:34

Au Mungu amekwenda wakati gani akajitwalia taifa toka kati ya taifa lingine, kwa majaribu, na kwa ishara, na kwa maajabu, na kwa vita, na kwa mkono hodari, na kwa mkono ulionyoshwa, na kwa maogofya makuu, kama vile Bwana, Mungu wenu, alivyowatendea ninyi katika Misri, mbele ya macho yenu?

Kumbukumbu la Torati 4:35

Wewe umeonyeshwa haya, ili upate kujua ya kuwa Bwana ndiye Mungu, hapana mwingine ila yeye.

Kumbukumbu la Torati 4:36

Kutoka mbinguni amekusikizisha sauti yake, ili akufundishe; na juu ya nchi alikuonyesha moto wake mkuu; ukasikia maneno yake toka kati ya moto.

Kumbukumbu la Torati 4:37

Na kwa sababu aliwapenda baba zenu, kwa sababu hiyo aliwachagua wazao wao baada yao, akakutoa katika Misri kwa kuwako pamoja nawe, kwa uweza wake mwingi,

Kumbukumbu la Torati 4:38

ili kufukuza mbele yako mataifa, walio wakubwa, wenye nguvu kukupita wewe, ili kukuingiza, na kukupa nchi yao iwe urithi, kama ilivyo leo.

Kumbukumbu la Torati 4:39

Kwa hiyo ujue, leo hivi, ukaweke moyoni mwako, ya kuwa Bwana ndiye Mungu katika mbingu juu, na katika nchi chini; hapana mwingine.

Kumbukumbu la Torati 4:40

Basi, zishike sheria zake, na amri zake, ninazokuamuru leo, upate kufanikiwa, wewe na watoto wako baada yako, na siku zako ziwe nyingi katika nchi ile akupayo Bwana, Mungu wako, milele.

Kumbukumbu la Torati 4:41

Ndipo Musa akabagua miji mitatu ng'ambo ya Yordani upande wa matokeo ya jua;

Kumbukumbu la Torati 4:42

ili kwamba amwuaye mtu apate kukimbilia huko, amwuaye jirani yake pasipo kujua, wala hakumchukia tangu hapo; ili apate kuishi akimbiliapo mmojawapo miji hiyo;

Kumbukumbu la Torati 4:43

nayo ni hii, Beseri ya barani iliyo katika nchi tambarare, kwa Wareubeni; na Ramothi iliyo Gileadi, kwa Wagadi; na Golani iliyo Bashani, kwa Wamanase.

Kumbukumbu la Torati 4:44

Na torati Musa aliyowawekea wana wa Israeli ni hii;

Kumbukumbu la Torati 4:45

haya ndiyo mashuhudizo, na amri, na hukumu, Musa alizowaambia wana wa Israeli walipotoka Misri;

Kumbukumbu la Torati 4:46

ng'ambo ya Yordani, katika bonde lililoelekea Beth-peori, katika nchi ya Sihoni mfalme wa Waamori, aliyekuwa akikaa Heshboni ndiye aliyepigwa na Musa na wana wa Israeli, walipotoka Misri;

Kumbukumbu la Torati 4:47

wakaishika nchi yake, ikawa milki yao, na nchi ya Ogu mfalme wa Bashani, ndio wafalme wawili wa Waamori, waliokuwa ng'ambo ya Yordani upande wa matokeo ya jua;

Kumbukumbu la Torati 4:48

toka Aroeri, iliyo juu ya ukingoni pa bonde la Arnoni, hata mpaka mlima wa Sioni (nao ndio Hermoni),

Kumbukumbu la Torati 4:49

na Araba yote iliyo ng'ambo ya Yordani upande wa mashariki, hata mpaka bahari ya Araba, chini ya matelemko ya Pisga.