Kumbukumbu la Torati Mlango 29 Deuteronomy

Kumbukumbu la Torati 29:1

Haya ndiyo maneno ya agano Bwana alilomwamuru Musa alifanye na wana wa Israeli katika nchi ya Moabu, pamoja na agano alilofanya nao Horebu.

Kumbukumbu la Torati 29:2

Musa akawaita Israeli wote akawaambia, Mmeyaona yote Bwana aliyomfanya Farao katika nchi ya Misri mbele ya macho yenu, yeye na watumwa wake wote, na nchi yake yote;

Kumbukumbu la Torati 29:3

yale majaribu makuu yaliyoyaona macho yako; hizo ishara, na ile miujiza mikuu;

Kumbukumbu la Torati 29:4

lakini Bwana hakuwapa moyo wa kujua, wala macho ya kuona, wala masikio ya kusikia, hata leo hivi.

Kumbukumbu la Torati 29:5

Nami miaka arobaini nimewaongoza jangwani; nguo zenu hazikuchakaa juu yenu, wala kiatu chako hakikuchakaa katika mguu wako.

Kumbukumbu la Torati 29:6

Hamkula mkate, wala hamkunywa divai, wala kileo; ili mpate kujua kwamba Mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.

Kumbukumbu la Torati 29:7

Nanyi mlipokuja mahali hapa, walitutokea kupigana juu yetu Sihoni mfalme wa Heshboni, na Ogu mfalme wa Bashani, tukawapiga;

Kumbukumbu la Torati 29:8

tukaitwaa nchi yao, nayo tukawapa Wareubeni, na Wagadi, na nusu ya kabila ya Manase, iwe urithi.

Kumbukumbu la Torati 29:9

Shikeni basi maneno ya agano hili myafanye, ili mfanikiwe katika yote mfanyayo.

Kumbukumbu la Torati 29:10

Leo mmesimama nyote mbele za Bwana, Mungu wenu; wakuu wenu, na kabila zenu, na wazee wenu, na maakida wenu, waume wote wa Israeli,

Kumbukumbu la Torati 29:11

vijana vyenu, na wake wenu, na mgeni wako aliye kati ya kituo chako, tokea mchanjaji wa kuni zako hata mtekaji wa maji yako;

Kumbukumbu la Torati 29:12

ili uingie katika agano la Bwana, Mungu wako, na kiapo chake, afanyacho nawe Bwana, Mungu wako, hivi leo;

Kumbukumbu la Torati 29:13

apate kukuweka leo uwe taifa kwake naye apate kuwa Mungu kwako, kama alivyokuambia, na kama alivyowaapia baba zako, Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo.

Kumbukumbu la Torati 29:14

Wala sifanyi na ninyi peke yenu agano hili na kiapo hiki;

Kumbukumbu la Torati 29:15

ila na yeye aliyesimama hapa nasi hivi leo mbele ya Bwana, Mungu wetu, na yeye naye asiyekuwapo pamoja nasi leo;

Kumbukumbu la Torati 29:16

(kwani mwajua mlivyoketi nchi ya Misri, na tulivyo kuja katikati ya mataifa hayo mliyopita katikati yao;

Kumbukumbu la Torati 29:17

nanyi mliona machukizo yao, na sanamu zao, miti na mawe, fedha na dhahabu, zilizokuwako kwao;)

Kumbukumbu la Torati 29:18

asiwe mtu katikati yenu, mume wala mke, wala jamaa, wala kabila, ageukaye moyo wake leo amwache Bwana, Mungu wetu, kwenda kuitumikia miungu ya mataifa hayo; lisiwe katikati yenu shina lizaalo uchungu na pakanga;

Kumbukumbu la Torati 29:19

ikawa asikiapo maneno ya laana hii, ajibarikie mtu huyo moyoni mwake, na kusema, Nitakuwa katika amani, nijapotembea katika upotoe wa moyo wangu kwa kuangamiza mbichi na kavu;

Kumbukumbu la Torati 29:20

Bwana hatamsamehe mtu huyo, lakini wakati huo hasira ya Bwana na wivu wake vitafuka moshi juu ya mtu yule, na laana yote iliyoandikwa katika kitabu hiki itamkalia juu yake, na Bwana atalifuta jina lake chini ya mbingu.

Kumbukumbu la Torati 29:21

Bwana atamtenga kwa uovu, kutoka kabila zote za Israeli, kwa laana zote za agano lililoandikwa katika chuo hiki cha torati.

Kumbukumbu la Torati 29:22

Na kizazi cha baadaye, wanenu watakaoinuka baada yenu, na mgeni atakayekuja kutoka nchi ya mbali, watasema, watakapoyaona mapigo ya nchi ile, na magonjwa aliyoitia Bwana;

Kumbukumbu la Torati 29:23

ya kuwa nchi yake nzima ni kibiriti, na chumvi, na kuteketea, haipandwi, wala haizai, wala nyasi hazimei humo, kama mapinduko ya Sodoma na Gomora, Adma na Seboimu, aliyoipindua Bwana kwa ghadhabu yake na hasira zake;

Kumbukumbu la Torati 29:24

mataifa yote watasema, Mbona Bwana ameifanyia hivi nchi hii? Ni nini maana yake hari ya hasira hizi kubwa?

Kumbukumbu la Torati 29:25

Ndipo watakaposema watu, Ni kwa kuwa waliacha agano la Bwana, Mungu wa baba zao, alilofanya nao hapo alipowatoa katika nchi ya Misri;

Kumbukumbu la Torati 29:26

wakaenda wakatumikia miungu mingine, wakaiabudu miungu wasiyoijua, asiyowapa yeye;

Kumbukumbu la Torati 29:27

ndipo ikawashwa hasira ya Bwana juu ya nchi hii, kwa kuleta juu yake laana yote iliyoandikwa katika kitabu hiki;

Kumbukumbu la Torati 29:28

Bwana akawang'oa katika nchi yao kwa hasira, na ghadhabu, na makamio makuu, akawatupa waende nchi nyingine, kama hivi leo.

Kumbukumbu la Torati 29:29

Mambo ya siri ni ya Bwana, Mungu wetu; lakini mambo yaliyofunuliwa ni yetu sisi na watoto wetu milele, ili tuyafanye maneno yote ya sheria hii.