Kumbukumbu la Torati Mlango 19 Deuteronomy

Kumbukumbu la Torati 19:1

Bwana, Mungu wako, atakapoyakatilia mbali hayo mataifa yenye nchi akupayo Bwana, Mungu wako, nawe ukawafuata, na kukaa katika miji yao, na katika nyumba zao;

Kumbukumbu la Torati 19:2

itenge miji mitatu iwe kwako katikati ya nchi yako, akupayo Bwana, Mungu wako, kuimiliki.

Kumbukumbu la Torati 19:3

Itengeze njia, igawanye na mipaka ya nchi yako, akurithishayo Bwana, Mungu wako, iwe mafungu matatu, ili kwamba kila mwenye kuua mtu apate kukimbilia huko.

Kumbukumbu la Torati 19:4

Na hii ndiyo hukumu ya mwenye kuua mtu, atakayekimbilia huko awe hai; atakayemwua mwenziwe pasipo kukusudia, wala hakumchukia tangu hapo;

Kumbukumbu la Torati 19:5

kama aingiapo mtu na mwenziwe mwituni kwenda kukata kuni, akapeleka mkono wake na shoka ili kukata mti, likatoka shoka katika mpini, likampiga yule mwenziwe hata akafa; basi na akimbilie katika miji hii mmojawapo awe hai;

Kumbukumbu la Torati 19:6

asije akaandamiwa mwuaji na mwenye kulipiza kisasi cha damu, moyo wake ukali na hasira, akampata kwa njia kuwa ndefu, akamwua; wala hana haki ya kuuawa, kwa kuwa hakumchukia tangu hapo.

Kumbukumbu la Torati 19:7

Kwa sababu hii ninakuamuru, na kukuambia, Ujitengee miji mitatu.

Kumbukumbu la Torati 19:8

Na kama Bwana, Mungu wako, akiueneza mpaka wako kama alivyowaapia baba zako, akakupa na nchi yote aliyoahidi kwamba atawapa baba zako;

Kumbukumbu la Torati 19:9

nawe ukiyashika maagizo haya yote nikuagizayo leo, na kuyafanya, kumpenda Bwana, Mungu wako, na kwenda sikuzote katika njia zake, ndipo ujiongezee miji mitatu tena, pamoja na mitatu ile;

Kumbukumbu la Torati 19:10

isije ikamwagika damu ya asiye makosa kati ya nchi yako akupayo Bwana, Mungu wako, iwe urithi, ikawa na damu juu yako.

Kumbukumbu la Torati 19:11

Lakini mtu awaye yote akimchukia mwenziwe na kumwotea na kumwinukia, akampiga hata akafa; naye akakimbilia miji hii mmojawapo;

Kumbukumbu la Torati 19:12

ndipo wazee wa mji wake wapeleke ujumbe kumtwaa huko, na kumuua katika mkono wa mwenye kulipiza kisasi cha damu, apate kufa.

Kumbukumbu la Torati 19:13

Jicho lako lisimhurumie, lakini uondoe damu ya asiye makosa katika Israeli, ili upate kufanikiwa.

Kumbukumbu la Torati 19:14

Usiiondoe alama ya mpaka wa jirani yako, waliouweka watu wa kale katika urithi wako, utakaorithi ndani ya nchi akupayo Bwana, Mungu wako, uimiliki.

Kumbukumbu la Torati 19:15

Shahidi mmoja asimwinukie mtu awaye yote kumshuhudia kwa uovu wo wote, wala kwa dhambi yo yote, katika makosa akosayo yo yote; jambo na lithibitishwe kwa vinywa vya mashahidi wawili, au watatu.

Kumbukumbu la Torati 19:16

Shahidi mdhalimu akimwinukia mtu ye yote na kushuhudia juu yake ya upotoe;

Kumbukumbu la Torati 19:17

ndipo wale watu washindanao kwa mambo yale na wasimame wote wawili mbele za Bwana, mbele ya makuhani na waamuzi watakaokuwapo siku hizo;

Kumbukumbu la Torati 19:18

nao waamuzi na watafute kwa bidii; na tazama, yule shahidi akiwa shahidi wa uongo, naye ametoa ushahidi wa uongo juu ya nduguye;

Kumbukumbu la Torati 19:19

ndipo mtamfanyia kama alivyodhani kumfanyia nduguye; ndivyo utakavyoondoa uovu katikati yako.

Kumbukumbu la Torati 19:20

Na watakaosalia watasikia na kuogopa, wasifanye tena uovu mfano wa huo katikati yako.

Kumbukumbu la Torati 19:21

Wala jicho lako lisiwe na huruma; uzima kwa uzima, jicho kwa jicho, jino kwa jino, mkono kwa mkono, mguu kwa mguu.