Kumbukumbu la Torati Mlango 7 Deuteronomy

Kumbukumbu la Torati 7:1

Bwana, Mungu wako, atakapokutia katika nchi uendayo kuimiliki, atakapoyang'oa mataifa mengi watoke mbele yako, Mhiti, na Mgirgashi, na Mwamori, na Mkanaani, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi, mataifa saba makubwa yenye nguvu kukupita wewe;

Kumbukumbu la Torati 7:2

wakati Bwana, Mungu wako, atakapowatoa mbele yako, nawe utawapiga; wakati huo ndipo uwaondoe kabisa; usifanye agano nao, wala kuwahurumia; wala usioane nao;

Kumbukumbu la Torati 7:3

binti yako usimpe mwanawe mume, wala usimtwalie mwanao mume binti yake.

Kumbukumbu la Torati 7:4

Kwa kuwa atamkengeusha mwanao mume asinifuate, ili wapate kuabudu miungu mingine; ndipo itakapowaka hasira ya Bwana juu yenu, naye atakuangamiza upesi.

Kumbukumbu la Torati 7:5

Lakini watendeni hivi; zivunjeni madhabahu zao zibomosheni nguzo zao, yakateni maashera yao, ziteketezeni kwa moto sanamu zao za kuchonga.

Kumbukumbu la Torati 7:6

Kwa maana wewe u taifa takatifu kwa Bwana, Mungu wako; Bwana Mungu wako, amekuchagua kuwa watu wake hasa, zaidi ya mataifa yote walioko juu ya uso wa nchi.

Kumbukumbu la Torati 7:7

Bwana hakuwapenda ninyi, wala hakuwachagua ninyi, kwa sababu mlikuwa wengi kuliko mataifa yote, maana mlikuwa wachache kuliko watu wote;

Kumbukumbu la Torati 7:8

bali kwa sababu Bwana anawapenda, na kwa sababu alitaka kuutimiza uapo wake aliowaapia baba zenu, ndiyo sababu Bwana akawatoa kwa mkono wa nguvu, akawakomboa katika nyumba ya utumwa, katika mkono wa Farao, mfalme wa Misri.

Kumbukumbu la Torati 7:9

Basi jueni ya kuwa Bwana, Mungu wenu, ndiye Mungu; Mungu mwaminifu, ashikaye agano lake na rehema zake kwao wampendao, na kushika amri zake, hata vizazi elfu;

Kumbukumbu la Torati 7:10

naye huwalipa wamchukiao mbele ya uso wao, kuwaangamiza. Hatakuwa mlegevu kwake yeye amchukiaye, atamlipa mbele ya uso wake.

Kumbukumbu la Torati 7:11

Basi zishike amri, na sheria, na hukumu ninazokuamuru leo, uzitende.

Kumbukumbu la Torati 7:12

Na itakuwa, kwa sababu mwazisikiliza hukumu hizi, na kuzishika na kuzitenda, basi Bwana, Mungu wako, atakutimilizia agano na rehema aliyowaapia baba zako;

Kumbukumbu la Torati 7:13

naye atakupenda na kukubarikia na kukuongeza tena ataubarikia uzao wa tumbo lako, na uzao wa nchi yako, nafaka zako na divai yako, na mafuta yako, maongeo ya ng'ombe zako, na wadogo wa kondoo zako, katika nchi aliyowaapia baba zako kuwa atakupa.

Kumbukumbu la Torati 7:14

Utabarikiwa kuliko mataifa yote; hakutakuwa na mtu mume wala mke aliye tasa kati yenu; wala kati ya wanyama wenu wa mifugo.

Kumbukumbu la Torati 7:15

Na Bwana atakuondolea ugonjwa wote; wala hatatia juu yako maradhi yo yote mabaya uyajuayo ya Misri, lakini atayaweka juu ya wote wakuchukiao.

Kumbukumbu la Torati 7:16

Nawe angamiza mataifa yote atakayokupa Bwana, Mungu wako; jicho lako lisiwahurumie, wala usiitumikie miungu yao; kwani litakuwa ni mtego kwako jambo hilo.

Kumbukumbu la Torati 7:17

Nawe kama ukisema moyoni mwako, Mataifa haya ni mengi kunipita mimi; nitawatoaje katika milki yao?

Kumbukumbu la Torati 7:18

Usiwaogope; kumbuka sana Bwana, Mungu wako, alivyomfanya Farao na Misri yote;

Kumbukumbu la Torati 7:19

uyakumbuke hayo majaribu makuu yaliyoyaona macho yako, na hizo ishara, na maajabu, na mkono wa nguvu, na mkono ulionyoka, aliokutolea nje Bwana, Mungu wako; ndivyo atakavyowafanya Bwana, Mungu wako, mataifa yote unaowaogopa.

Kumbukumbu la Torati 7:20

Tena Bwana, Mungu wako, atampeleka mavu kati yao, hata hao watakaosalia, hao wajifichao, waangamie mbele zako.

Kumbukumbu la Torati 7:21

Usiingiwe na kicho kwa sababu yao; kwa kuwa Bwana, Mungu wako, yu katikati yako, Mungu mkuu, mwenye utisho.

Kumbukumbu la Torati 7:22

Naye Bwana, Mungu wako, atayatupia nje mataifa yale mbele yako kidogo kidogo; haikupasi kuwaangamiza kwa mara moja, wasije wakaongezeka kwako wanyama wa mwitu.

Kumbukumbu la Torati 7:23

Ila Bwana, Mungu wako, atawatoa mbele yako, atawatia mashaka, mashaka makuu, hata waishe kuangamizwa.

Kumbukumbu la Torati 7:24

Na wafalme wao atakutilia mkononi mwako, nawe utalipoteza jina lao litoke chini ya mbingu; hapana mtu atakayeweza kusimama mbele yako, hata utakapokwisha kuwaangamiza.

Kumbukumbu la Torati 7:25

Sanamu za kuchonga za miungu yao mtaziteketeza kwa moto; usitamani fedha wala dhahabu iliyo juu yao, wala usiitwae iwe yako usije ukanaswa nayo; kwa maana ni machukizo kwa Bwana, Mungu wako;

Kumbukumbu la Torati 7:26

na machukizo usitie ndani ya nyumba yako, usije wewe kuwa kitu cha haramu mfano wake; ukichukie kabisa, na kukikataa kabisa; kwa kuwa ni kitu kilichoharimishwa.