Kumbukumbu la Torati Mlango 28 Deuteronomy

Kumbukumbu la Torati 28:1

Itakuwa utakaposikia sauti ya Bwana, Mungu wako, kwa bidii, kutunza kuyafanya maagizo yake yote nikuagizayo leo, ndipo Bwana, Mungu wako, atakapokutukuza juu ya mataifa yote ya duniani;

Kumbukumbu la Torati 28:2

na baraka hizi zote zitakujilia na kukupata usikiapo sauti ya Bwana, Mungu wako.

Kumbukumbu la Torati 28:3

Utabarikiwa mjini, utabarikiwa na mashambani.

Kumbukumbu la Torati 28:4

Utabarikiwa uzao wa tumbo lako, na uzao wa nchi yako, na uzao wa wanyama wako wa mifugo, maongeo ya ng'ombe wako, na wadogo wa kondoo zako.

Kumbukumbu la Torati 28:5

Litabarikiwa kapu lako, na chombo chako cha kukandia unga.

Kumbukumbu la Torati 28:6

Utabarikiwa uingiapo, utabarikiwa na utokapo.

Kumbukumbu la Torati 28:7

Bwana atawafanya adui zako wainukao juu yako kupigwa mbele yako; watakutokea kwa njia moja, lakini watakimbia mbele yako kwa njia saba.

Kumbukumbu la Torati 28:8

Bwana ataiamuru baraka ije juu yako katika ghala zako, na mambo yote utakayotia mkono wako; naye atakubarikia katika nchi akupayo Bwana, Mungu wako.

Kumbukumbu la Torati 28:9

Bwana atakuweka uwe taifa takatifu kwake, kama alivyokuapia; utakaposhika maagizo ya Bwana, Mungu wako, na kutembea katika njia zake.

Kumbukumbu la Torati 28:10

Na mataifa yote ya duniani watakuona umeitwa kwa jina la Bwana, nao watakuwa na hofu kwako.

Kumbukumbu la Torati 28:11

Bwana atakufanya uwe na wingi wa uheri, katika uzao wa tumbo lako, na uzao wa wanyama wako wa mifugo, na uzao wa nchi yako, katika nchi Bwana aliyowaapia baba zako kwamba atakupa.

Kumbukumbu la Torati 28:12

Atakufunulia Bwana hazina yake nzuri, nayo ni mbingu, kwa kutoa mvua ya nchi yako kwa wakati wake, na kwa kubarikia kazi yote ya mkono wako; nawe utakopesha mataifa mengi, wala hutakopa wewe.

Kumbukumbu la Torati 28:13

Bwana atakufanya kuwa kichwa, wala si mkia; nawe utakuwa juu tu, wala huwi chini; utakapoyasikiza maagizo ya Bwana, Mungu wako, nikuagizayo hivi leo, kuyaangalia na kufanya;

Kumbukumbu la Torati 28:14

msipokengeuka katika maneno niwaamuruyo leo kwa lo lote, kwenda mkono wa kuume wala wa kushoto, kwa kuifuata miungu mingine na kuitumikia.

Kumbukumbu la Torati 28:15

Lakini itakuwa usipotaka kuisikiza sauti ya Bwana, Mungu wako, usiyaangalie kufanya maagizo yake yote na amri zake, nikuagizazo hivi leo, ndipo zitakapokujia laana hizi zote na kukupata.

Kumbukumbu la Torati 28:16

Utalaaniwa mjini, utalaaniwa na mashambani.

Kumbukumbu la Torati 28:17

Litalaaniwa kapu lako na chombo chako cha kukandia.

Kumbukumbu la Torati 28:18

Utalaaniwa uzao wa tumbo lako, na uzao wa nchi yako, maongeo ya ng'ombe wako, na wadogo wa kondoo zako.

Kumbukumbu la Torati 28:19

Utalaaniwa uingiapo, utalaaniwa na utokapo,

Kumbukumbu la Torati 28:20

Bwana atakuletea laana na mashaka, na kukemewa, katika yote utakayotia mkono wako kuyafanya, hata uangamie na kupotea kwa upesi; kwa ule uovu wa matendo yako, uliyoniacha kwayo.

Kumbukumbu la Torati 28:21

Bwana atakuambatanisha na tauni, hata atakapokwisha kukuondoa katika nchi uingiayo kwa kuimiliki.

Kumbukumbu la Torati 28:22

Bwana atakupiga kwa kifua kikuu, na kwa homa, na kwa kuwashwa, na kwa hari ya moto, na kwa upanga, na kwa ukaufu, na kwa koga; navyo vitakufukuza hata uangamie.

Kumbukumbu la Torati 28:23

Na mbingu zako zilizo juu ya kichwa chako zitakuwa shaba, na nchi iliyo chini yako itakuwa chuma.

Kumbukumbu la Torati 28:24

Bwana atafanya mvua ya nchi yako iwe vumbi na mchanga; itakujilia juu yako kutoka mbinguni hata uangamie.

Kumbukumbu la Torati 28:25

Bwana atakufanya upigwe mbele ya adui zako; utawatokea juu yao kwa njia moja, lakini utakimbia mbele yao kwa njia saba; nawe utatupwa huko na huko katika falme zote za duniani.

Kumbukumbu la Torati 28:26

Na mzoga wako utakuwa chakula cha ndege wote wa angani, na wanyama wote wa duniani, pasiwe na mtu wa kuwafukuza.

Kumbukumbu la Torati 28:27

Bwana atakupiga kwa majipu ya Misri, na kwa bawasiri, na kwa pele, na kwa kujikuna, ambayo hupati kupoa.

Kumbukumbu la Torati 28:28

Bwana atakupiga kwa wazimu, na kwa upofu, na kwa bumbuazi la moyoni;

Kumbukumbu la Torati 28:29

utakwenda kwa kupapasa-papasa mchana, kama apapasavyo kipofu gizani, wala hufanikiwi katika njia zako; nawe sikuzote utaonewa na kutekwa nyara, wala hapatakuwa na mtu wa kukuokoa.

Kumbukumbu la Torati 28:30

Utaposa mke na mume mwingine atalala naye; utajenga nyumba usiikae; utapanda mizabibu usitumie matunda yake.

Kumbukumbu la Torati 28:31

Ng'ombe wako atachinjwa mbele ya macho yako, usile nyama yake; utanyang'anywa punda wako mbele ya uso wako kwa jeuri, usirudishiwe; kondoo zako watapewa adui zako, usipate mtu wa kukuokoa.

Kumbukumbu la Torati 28:32

Wanao na binti zako litapewa taifa lingine, na macho yako yataangalia, na kuzimia kwa kuwatamani mchana kutwa; wala hapatakuwa na kitu katika uwezo wa mkono wako.

Kumbukumbu la Torati 28:33

Matunda ya nchi yako, na taabu yako yote, vitaliwa na taifa usilolijua; utaonewa tu, na kupondwa chini daima;

Kumbukumbu la Torati 28:34

hata uwe mwenye wazimu kwa yaonwayo na macho yako, utakayoyaona.

Kumbukumbu la Torati 28:35

Bwana atakupiga magoti na miguu kwa jipu lililo zito, usilopata kupozwa, tokea wayo wa mguu mpaka utosi wa kichwa.

Kumbukumbu la Torati 28:36

Bwana atakupeleka wewe, na mfalme wako utakayemweka juu yako, kwa taifa usilolijua wewe wala baba zako; nawe huko utatumikia miungu mingine ya miti na mawe.

Kumbukumbu la Torati 28:37

Nawe utakuwa ushangao, na mithali, na dharau, kati ya mataifa yote huko atakakokuongoza Bwana.

Kumbukumbu la Torati 28:38

Mbegu nyingi utazichukua nje shambani, lakini utavuna haba, kwa kuwa nzige watazila.

Kumbukumbu la Torati 28:39

Utapanda mizabibu na kuitengeza, wala hutakunywa katika divai yake, wala kuichuma kwani italiwa na mabuu.

Kumbukumbu la Torati 28:40

Utakuwa na mizeituni katika mipaka yako yote usijipake mafuta yake; kwa kuwa mzeituni wako utapukutika.

Kumbukumbu la Torati 28:41

Utazaa wana na binti, lakini hawatakuwa wako wewe; kwa sababu watakwenda utumwani.

Kumbukumbu la Torati 28:42

Miti yako yote, na mazao ya nchi yako, nzige watakuwa nayo.

Kumbukumbu la Torati 28:43

Mgeni aliye kati yako atazidi kupaa juu yako; nawe utazidi kushuka chini.

Kumbukumbu la Torati 28:44

Yeye atakukopesha, wala wewe usimkopeshe; yeye atakuwa ni kichwa, wewe utakuwa mkia.

Kumbukumbu la Torati 28:45

Na laana hizi zote zitakujilia juu yako, zitakuandama na kukupata, hata uangamizwe, kwa kuwa hukuisikiza sauti ya Bwana, Mungu wako, kushika maagizo yake na amri zake alizokuagiza;

Kumbukumbu la Torati 28:46

nazo zitakuwa juu yako kwa ishara na ajabu, na juu ya uzao wako milele;

Kumbukumbu la Torati 28:47

kwa kuwa hukumtumikia Bwana, Mungu wako, kwa furaha na moyo wa kushukuru, kwa ajili ya ule wingi wa vitu vyote;

Kumbukumbu la Torati 28:48

kwa hiyo utawatumikia adui zako atakaowaleta Bwana juu yako, kwa njaa, na kwa kiu, na kwa uchi, na kwa uhitaji wa vitu vyote; naye atakuvika kongwa la chuma shingoni mwako, hata atakapokwisha kukuangamiza.

Kumbukumbu la Torati 28:49

Bwana atakuletea taifa juu yako kutoka mbali, kutoka ncha ya dunia, kama arukavyo tai; taifa usiloufahamu ulimi wake;

Kumbukumbu la Torati 28:50

taifa lenye uso mkali, ambalo haliangalii uso wa mzee, wala halipendelei kijana;

Kumbukumbu la Torati 28:51

naye atakula uzao wa ng'ombe wako wa mifugo, na uzao wa nchi yako mpaka utakapokwisha kuangamizwa; wala hatakuachia nafaka, wala divai, wala mafuta, wala maongeo ya ng'ombe wako, wala wana-kondoo wako, hata atakapokwisha kukuangamiza.

Kumbukumbu la Torati 28:52

Naye atakuhusuru katika malango yako yote, hata kuta zako ndefu, zenye maboma, ulizokuwa ukiziamini, zishuke, katika nchi yako yote kila upande; naye atakuhusuru katika malango yako yote kila upande, katika nchi yako yote aliyokupa Bwana, Mungu wako.

Kumbukumbu la Torati 28:53

Nawe utakula uzao wa tumbo lako mwenyewe, nyama ya wana wako na binti zako aliokupa Bwana, Mungu wako; katika mazingirwa na katika mkazo utakaokazwa na adui zako.

Kumbukumbu la Torati 28:54

Mtu mume kati yenu aliye mwororo na laini sana, jicho lake litakuwa ovu juu ya nduguye, na juu ya mke wa kifuani mwake, na juu ya masalio ya wanawe waliosalia naye;

Kumbukumbu la Torati 28:55

hata asitake wao mmojawapo apewe katika nyama ya wanawe atakaowala, kwa kuwa hana kitu kilichomsalia kwake; katika mazingirwa na mkazo utakaokazwa na adui yako katika malango yako yote.

Kumbukumbu la Torati 28:56

Mwanamke kati yenu aliye mwororo na laini, ambaye hangehatirisha kuweka wayo wa mguu wake nchi kwa umalidadi na ulaini, jicho lake huyu litakuwa ovu juu ya mume wa kifuani mwake, na juu ya mwanawe, na juu ya binti yake,

Kumbukumbu la Torati 28:57

na juu ya mchanga wake atokaye katikati ya miguu yake, na juu ya wanawe atakaowazaa; kwa kuwa atawala kwa siri, kwa uhitaji wa vitu vyote; katika mazingirwa na mkazo utakaokazwa na adui yako katika malango yako.

Kumbukumbu la Torati 28:58

Kama hutaki kutunza kufanya maneno yote ya torati hii yaliyoandikwa katika kitabu hiki, upate kulicha jina hili la fahari na utisho, Bwana, MUNGU WAKO;

Kumbukumbu la Torati 28:59

ndipo atakapofanya Bwana mapigo yako yawe ya ajabu, na mapigo ya uzao wako, mapigo makubwa kwa kweli, ya kudumu sana, na magonjwa mazito ya kudumu sana.

Kumbukumbu la Torati 28:60

Naye atakurejezea maradhi yote ya Misri juu yako uliyokuwa ukiyaogopa, nayo yataambatana nawe.

Kumbukumbu la Torati 28:61

Tena kila ugonjwa, na kila pigo yasiyoandikwa katika kitabu cha torati hii, atakutia nayo Bwana juu yako, hata utakapokwisha kuangamizwa.

Kumbukumbu la Torati 28:62

Nanyi mtasalia wachache kwa hesabu, ninyi mliokuwa mfano wa nyota za mbinguni kwa wingi; kwa kuwa hukuisikiza sauti ya Bwana, Mungu wako.

Kumbukumbu la Torati 28:63

Tena itakuwa, kama vile alivyokuwa akifurahi Bwana juu yenu kwa kuwatendea mema na kuwafanya kuwa wengi, ndivyo atakavyofurahi Bwana juu yenu kwa kuwapoteza na kuwaangamiza; nanyi mtanyakuliwa katika hiyo nchi mwingiayo kuimiliki.

Kumbukumbu la Torati 28:64

Bwana atakutawanya katika mataifa yote, tokea ncha hii ya dunia hata ncha hii ya dunia; nawe huko utatumikia miungu mingine usiyoijua wewe wala baba zako, nayo ni miti na mawe.

Kumbukumbu la Torati 28:65

Wala katika mataifa hayo hutapata raha iwayo yote, wala hutakuwa na kituo cha wayo wa mguu wako; lakini Bwana atakupa huko moyo wa kutetema, na macho ya kuzimia, na roho ya kudhoofika;

Kumbukumbu la Torati 28:66

na uzima wako utakuwa na wasiwasi mbele yako; nawe utakuwa na woga usiku na mchana, wala hutaamini kamwe maisha yako;

Kumbukumbu la Torati 28:67

asubuhi utasema, Laiti ingekuwa jioni! Na jioni utasema, Laiti ingekuwa asubuhi! Kwa kicho cha moyo wako utakavyokucha, na kuona kwa macho yako utakavyoona.

Kumbukumbu la Torati 28:68

Bwana atakurudisha tena Misri kwa merikebu, kwa njia ambayo nilikuambia, Hutaiona tena po pote; nanyi huko mtajiuza nafsi zenu kwa adui zenu kuwa watumwa na wajakazi, wala hapana atakayewanunua.