Kumbukumbu la Torati Mlango 15 Deuteronomy

Kumbukumbu la Torati 15:1

Kila miaka saba, mwisho wake, fanya maachilio.

Kumbukumbu la Torati 15:2

Na jinsi ya maachilio ni hii, kila mkopeshaji na akiache alichomkopesha mwenziwe, wala asimlipize mwenziwe wala nduguye; kwa kuwa imepigwa mbiu ya maachilio ya Bwana.

Kumbukumbu la Torati 15:3

Waweza kumtoza mgeni; lakini kila uwiacho kwa nduguyo mkono wako utamwachilia.

Kumbukumbu la Torati 15:4

Lakini hawatakuwako maskini kwenu; (kwa kuwa Bwana atakubarikia kweli katika nchi akupayo Bwana, Mungu wako, uimiliki, iwe urithi wako;)

Kumbukumbu la Torati 15:5

kwamba utaisikiza tu kwa bidii sauti ya Bwana, Mungu wako, uyatunze maagizo haya yote nikuagizayo leo, kuyafanya.

Kumbukumbu la Torati 15:6

Kwani Bwana, Mungu wako, atakubarikia, kama alivyokuahidi; nawe utakopesha mataifa mengi, lakini hutakopa; tena utayatawala mataifa mengi, usitawaliwe na wao.

Kumbukumbu la Torati 15:7

Kama akiwapo mtu maskini pamoja nawe, nduguzo mmojawapo, ndani ya malango yako mojawapo, katika nchi yako akupayo Bwana, Mungu wako, usifanye moyo wako kuwa mgumu, wala usimfumbie mkono wako nduguyo maskini;

Kumbukumbu la Torati 15:8

lakini mfumbulie mkono wako kwa kweli, umkopeshe kwa kweli yatoshayo haja yake katika ahitajiayo.

Kumbukumbu la Torati 15:9

Jitunze, msiwe na neno lisilofaa moyoni mwako, kusema, Umekaribia mwaka wa saba, mwaka wa maachilio; jicho lako likawa ovu juu ya nduguyo usimpe kitu; naye akamlilia Bwana juu yako, ikawa ni dhambi kwako.

Kumbukumbu la Torati 15:10

Mpe kwa kweli, wala moyo wako usisikitike utakapompa; kwa kuwa atakubarikia Bwana, Mungu wako, kwa neno hili katika kazi yako yote, na katika kila utakalotia mkono wako.

Kumbukumbu la Torati 15:11

Kwa maana maskini hawatakoma katika nchi milele; ndipo ninakuamuru na kukuambia, Mfumbulie kwa kweli mkono wako nduguyo, mhitaji wako, maskini wako, katika nchi yako.

Kumbukumbu la Torati 15:12

Ikiwa nduguyo, mume wa Kiebrania, au mwanamke wa Kiebrania, akiuzwa kwako, naye amekutumikia miaka sita; basi mwaka wa saba mwache huru aondoke kwako.

Kumbukumbu la Torati 15:13

Nawe utakapomwacha huru aondoke kwako, usimwache aende zake mikono mitupu;

Kumbukumbu la Torati 15:14

umwangalie kwa wema katika kundi lako, na sakafu yako ya nafaka, na kinu chako cha divai; mpe kama alivyokubarikia Bwana, Mungu wako.

Kumbukumbu la Torati 15:15

Nawe kumbuka kwamba ulikuwa mtumwa katika nchi ya Misri, akakukomboa Bwana, Mungu wako; kwa hiyo mimi nakuamuru neno hili hivi leo.

Kumbukumbu la Torati 15:16

Hata itakuwa, akikuambia, Siondoki kwako; kwa sababu akupenda wewe na nyumba yako, kwa kuwa yu hali njema kwako;

Kumbukumbu la Torati 15:17

ndipo utwae uma, uupenyeze katika sikio lake uingie katika ubao wa mlango, naye atakuwa mtumishi wako milele. Na kijakazi chako naye mfanye vivyo.

Kumbukumbu la Torati 15:18

Wala usione ugumu, utakapomwacha huru kuondoka kwako; kwani amekutumikia miaka sita kwa ujira mara mbili wa mwajiriwa; na Bwana, Mungu wako, atakubarikia kwa yote utakayofanya.

Kumbukumbu la Torati 15:19

Wazaliwa wa kwanza waume wote wazaliwao katika kundi lako la ng'ombe na la kondoo, uwatakase kwa Bwana, Mungu wako; usifanye kazi kwa mzaliwa wa kwanza wa ng'ombe wako, wala usimkate manyoya mzaliwa wa kwanza wa kundi lako la kondoo.

Kumbukumbu la Torati 15:20

Utamla mbele za Bwana, Mungu wako, mwaka hata mwaka mahali atakapochagua Bwana, wewe na nyumba yako.

Kumbukumbu la Torati 15:21

Lakini akiwa na kilema, akichechea, au akiwa kipofu, au mwenye kilema kibaya cho chote, usimsongezee Bwana, Mungu wako, sadaka.

Kumbukumbu la Torati 15:22

Utamla ndani ya malango yako; wasio tohara na wenye tohara pia watakula, kama unavyokula paa na kulungu.

Kumbukumbu la Torati 15:23

Pamoja na haya usile damu yake; uimwage nchi kama maji.