Kumbukumbu la Torati Mlango 13 Deuteronomy

Kumbukumbu la Torati 13:1

Kukizuka katikati yako nabii, au mwotaji wa ndoto, akikutolea ishara au ajabu,

Kumbukumbu la Torati 13:2

ikatukia hiyo ishara au hiyo ajabu aliyokuambia akisema, Na tuifuate miungu mingine usiyoijua, tuitumikie hiyo;

Kumbukumbu la Torati 13:3

wewe usiyasikize maneno ya nabii yule, au yule mwotaji wa ndoto, kwa kuwa Bwana, Mungu wenu, yuawajaribu, apate kujua kwamba mwampenda Bwana, Mungu wenu, kwa mioyo yenu yote na roho zenu zote.

Kumbukumbu la Torati 13:4

Tembeeni kwa kumfuata Bwana, Mungu wenu; mcheni na kushika maagizo yake na kuisikia sauti yake, nanyi mtumikieni na kushikamana naye.

Kumbukumbu la Torati 13:5

Na yule nabii, au yule mwotaji wa ndoto, na auawe, kwa kuwa amesema yaliyopotoka juu ya Bwana, Mungu wenu, aliyewatoa katika nchi ya Misri, akakukomboa katika nyumba ya utumwa, apate yule mtu kukupotoa katika njia aliyokuamuru Bwana, Mungu wako, uiendee. Ndivyo utakavyouondoa uovu utoke katikati yako.

Kumbukumbu la Torati 13:6

Atakapokushawishi kwa siri ndugu yako, mwana wa mamaako, au mwana wako, au binti yako, au mke wa kifuani mwako, au rafiki yako aliye kama moyo wako, akikuambia, Twende tukaabudu miungu mingine usiyoijua wewe wala baba zako;

Kumbukumbu la Torati 13:7

katika miungu ya mataifa yaliyo kando-kando yenu karibu nawe au mbali nawe, tokea ncha moja ya dunia hata ncha ya pili ya dunia;

Kumbukumbu la Torati 13:8

usimkubalie wala usimsikize; wala jicho lako lisimwonee huruma, wala usimwache, wala usimfiche;

Kumbukumbu la Torati 13:9

mwue kweli; mkono wako na uwe wa kwanza juu yake katika kumwua, na baadaye mikono ya watu wote.

Kumbukumbu la Torati 13:10

Nawe mtupie mawe hata afe; kwa kuwa alitaka kukupotoa na Bwana, Mungu wako aliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa.

Kumbukumbu la Torati 13:11

Na Israeli wote watasikia na kuogopa, wasifanye tena uovu mfano wa huo katikati yako.

Kumbukumbu la Torati 13:12

Ukisikia yasemwa habari ya miji yako mmojawapo, akupayo Bwana, Mungu wako, ukae humo, ukiambiwa,

Kumbukumbu la Torati 13:13

Kumetoka katikati yako mabaradhuli kadha wa kadha, wamewapotoa wenyeji wa mji wao, wakisema, Twendeni tukaabudu miungu mingine msiyoijua;

Kumbukumbu la Torati 13:14

ndipo nawe uulize na kutafuta, ukiuliza kwa bidii; nawe angalia, ikiwa kweli, na jambo lile halina shaka, kwamba machukizo mfano wa haya yafanyika katikati yako;

Kumbukumbu la Torati 13:15

hakika yako uwapige wenyeji wa mji ule kwa makali ya upanga, kwa kuwaangamiza kabisa, pamoja na vitu vyote vilivyomo, na wanyama walio humo, kwa makali ya upanga.

Kumbukumbu la Torati 13:16

Na nyara zake zote uzikusanyie katikati ya njia yake; na mji uuteketeze kwa moto, na nyara zake zote, kuwe sadaka kamili ya kuteketezwa kwa Bwana, Mungu wako; nao utakuwa magofu milele; usijengwe tena.

Kumbukumbu la Torati 13:17

Kisishikamane na mkono wako kitu cho chote katika kitu kilichoharimishwa; ili ageuke Bwana na ukali wa hasira zake akurehemu, akuonee huruma, na kukufanya kuwa wengi, kama alivyowaapia baba zako;

Kumbukumbu la Torati 13:18

utakaposikiza sauti ya Bwana, Mungu wako kwa kushika maagizo yake yote nikuagizayo leo, ufanye yaliyoelekea machoni pa Bwana, Mungu wako.