Kumbukumbu la Torati Mlango 6 Deuteronomy

Kumbukumbu la Torati 6:1

Na hii ndiyo sheria, na amri, na hukumu, alizoziamuru Bwana, Mungu wenu, mfundishwe, mpate kuzitenda katika nchi ile mnayoivukia kuimiliki;

Kumbukumbu la Torati 6:2

upate kumcha Bwana, Mungu wako, kushika amri zake zote, na sheria zake, ninazokuamuru, wewe na mwanao, na mwana wa mwanao, siku zote za maisha yako; tena siku zako ziongezwe.

Kumbukumbu la Torati 6:3

Sikiza basi, Ee Israeli, ukaangalie kuzitenda; upate kufanikiwa, mpate kuongezeka sana, kama Bwana, Mungu wa baba zako, alivyokuahidi, katika nchi ijaayo maziwa na asali.

Kumbukumbu la Torati 6:4

Sikiza, Ee Israeli; Bwana, Mungu wetu, Bwana ndiye mmoja.

Kumbukumbu la Torati 6:5

Nawe mpende Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote.

Kumbukumbu la Torati 6:6

Na maneno haya ninayokuamuru leo, yatakuwa katika moyo wako;

Kumbukumbu la Torati 6:7

nawe uwafundishe watoto wako kwa bidii, na kuyanena uketipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo, na uondokapo.

Kumbukumbu la Torati 6:8

Yafunge yawe dalili juu ya mkono wako, nayo yatakuwa kama utepe katikati ya macho yako.

Kumbukumbu la Torati 6:9

Tena yaandike juu ya miimo ya nyumba yako, na juu ya malango yako.

Kumbukumbu la Torati 6:10

Tena itakuwa atakapokwisha Bwana, Mungu wako, kukuleta katika nchi aliyowaapia babu zako, Ibrahimu na Isaka na Yakobo, ya kuwa atakupa; miji mikubwa mizuri usiyoijenga wewe,

Kumbukumbu la Torati 6:11

na nyumba zimejaa vitu vyema vyote usizojaza wewe, na visima vimefukuliwa usivyofukua wewe, mashamba ya mizabibu na mizeituni usiyoipanda wewe, nawe utakula na kushiba;

Kumbukumbu la Torati 6:12

ndipo ujitunze, usije ukamsahau Bwana aliyekutoa nchi ya Misri, nyumba ya utumwa.

Kumbukumbu la Torati 6:13

Mche Bwana, Mungu wako; ndiye utakayemtumikia, na kuapa kwa jina lake.

Kumbukumbu la Torati 6:14

Msifuate miungu mingine katika miungu ya mataifa wawazungukao;

Kumbukumbu la Torati 6:15

kwani Bwana, Mungu wako, aliye katikati yako ni Mungu mwenye wivu; isije ikawaka juu yako hasira ya Bwana, Mungu wako, akakuangamiza kutoka juu ya uso wa nchi.

Kumbukumbu la Torati 6:16

Msimjaribu Bwana, Mungu wenu, kama mlivyomjaribu huko Masa.

Kumbukumbu la Torati 6:17

Zishikeni kwa bidii sheria za Bwana, Mungu wenu, na mashuhudizo yake, na amri zake alizokuagiza.

Kumbukumbu la Torati 6:18

Nawe fanya yaliyo sawa, na mema, machoni pa Bwana; ili mpate kufanikiwa, nawe upate kuingia na kuimiliki nchi nzuri Bwana aliyowaapia baba zako,

Kumbukumbu la Torati 6:19

ya kuwa atawasukumia nje adui zako wote mbele yako, kama alivyosema Bwana.

Kumbukumbu la Torati 6:20

Na zamani zijazo atakapokuuliza mwanao, akikuambia, N'nini mashuhudizo, na amri, na hukumu, alizowaagiza Bwana, Mungu wetu?

Kumbukumbu la Torati 6:21

Ndipo umwambie mwanao, Tulikuwa watumwa wa Farao huko Misri; Bwana, akatutoa kutoka Misri kwa mkono wa nguvu;

Kumbukumbu la Torati 6:22

Bwana akaonya ishara na maajabu, makubwa, mazito, juu ya Misri, na juu ya Farao, na juu ya nyumba yake yote, mbele ya macho yetu;

Kumbukumbu la Torati 6:23

akatutoa huko ili kututia huku, apate kutupa nchi aliyowaapia baba zetu.

Kumbukumbu la Torati 6:24

Bwana akatuamuru kuzifanya amri hizi zote, tumche Bwana, Mungu wetu, tuone mema sikuzote ili atuhifadhi hai kama hivi leo.

Kumbukumbu la Torati 6:25

Tena itakuwa haki kwetu, tukitunza kufanya maagizo haya yote mbele ya Bwana, Mungu wetu, kama alivyotuagiza.