Kumbukumbu la Torati Mlango 22 Deuteronomy

Kumbukumbu la Torati 22:1

Umwonapo ng'ombe wa nduguyo au kondoo wake akipotea, usijifiche kama usiyemwona; sharti utamrudisha kwa nduguyo.

Kumbukumbu la Torati 22:2

Na kwamba yule nduguyo hayupo karibu nawe, au ukiwa humjui, umchukue kwenu nyumbani kwako, uwe naye hata aje nduguyo kumtafuta, nawe mrudishie.

Kumbukumbu la Torati 22:3

Tena fanya vivyo kwa punda wake; tena fanya vivyo kwa mavazi yake; tena fanya vivyo kwa kila kitu kilichopotea cha nduguyo, kilichompotea ukakiona wewe; usijifiche kama usiyekiona.

Kumbukumbu la Torati 22:4

Umwonapo punda wa nduguyo, au ng'ombe wake, ameanguka kando ya njia, usijifiche kama usiyemwona; sharti umsaidie kumwinua tena.

Kumbukumbu la Torati 22:5

Mwanamke asivae mavazi yampasayo mwanamume, wala mwanamume asivae mavazi ya mwanamke; kwa maana kila afanyaye mambo hayo ni machukizo kwa Bwana, Mungu wako.

Kumbukumbu la Torati 22:6

Kiota cha ndege kikitukia kuwa mbele yako njiani, katika mti wo wote, au chini, chenye makinda au mayai, naye koo ameatamia juu ya makinda, au juu ya mayai, usimtwae yule koo pamoja na makinda;

Kumbukumbu la Torati 22:7

sharti umwache yule koo aende zake, lakini makinda waweza kuyatwaa uwe nayo; ili upate kufanikiwa, ufanye siku zako kuwa nyingi.

Kumbukumbu la Torati 22:8

Utakapojenga nyumba mpya, fanya ukuta kando-kando ya dari lako, usije ukaleta damu juu ya nyumba yako, mtu akianguka huko.

Kumbukumbu la Torati 22:9

Usipande shamba lako la mizabibu aina mbili za mbegu; yasije yakaondolewa matunda yote, mbegu ulizopanda na maongeo ya mizabibu yako.

Kumbukumbu la Torati 22:10

Usilime kwa ng'ombe na punda wakikokota jembe pamoja.

Kumbukumbu la Torati 22:11

Usivae nguo iliyochanganyikana sufu na kitani pamoja.

Kumbukumbu la Torati 22:12

Ujifanyizie vishada katika pembe nne za mavazi yako ya kujifunika.

Kumbukumbu la Torati 22:13

Mtu akitwaa mke, akamwingilia na kumchukia,

Kumbukumbu la Torati 22:14

kisha akamshitaki mambo ya aibu kumzushia jina baya, akasema, Nimemtwaa mwanamke huyu, nami nilipomkaribia sikuona kwake alama za ubikira;

Kumbukumbu la Torati 22:15

ndipo babaye yule kijana na mamaye watakapotwaa alama za yule kijana za ubikira, wawatolee wazee wa mji langoni;

Kumbukumbu la Torati 22:16

na baba yake yule kijana awaambie wazee, Mwanamume huyu nilimpa binti yangu awe mkewe, naye amchukia;

Kumbukumbu la Torati 22:17

angalieni, amemwekea mambo ya aibu, asema, Sikuona kwa binti yako alama za ubikira, nazo hizi ndizo alama za binti yangu za ubikira. Na wayakunjue yale mavazi mbele ya wazee wa mji.

Kumbukumbu la Torati 22:18

Basi wazee wa mji ule na wamtwae yule mtu mume na kumrudi,

Kumbukumbu la Torati 22:19

wamtoze shekeli mia za fedha, wampe babaye yule kijana, kwa kuwa amemzulia jina baya mwanamwali wa Israeli; naye awe mkewe; hana ruhusa ya kumwacha siku zake zote.

Kumbukumbu la Torati 22:20

Lakini likiwa ni kweli neno hili, la kutoonekana kwake yule kijana alama za ubikira;

Kumbukumbu la Torati 22:21

na wamtoe nje yule kijana mlangoni pa nyumba ya baba yake, na waume wa mji wake wampige kwa mawe hata afe; kwa vile alivyofanya upumbavu katika Israeli, kwa kufanya ukahaba katika nyumba ya baba yake; ndivyo utakavyoondoa uovu katikati yako.

Kumbukumbu la Torati 22:22

Akifumaniwa mtu mume amelala na mwanamke aliyeolewa na mume, na wafe wote wawili, mtu mume aliyelala na mwanamke, na yule mwanamke naye; ndivyo utakavyoondoa uovu katika Israeli.

Kumbukumbu la Torati 22:23

Pakiwa na kijana aliye mwanamwali ameposwa na mume, na mwanamume akimkuta mjini, akalala naye;

Kumbukumbu la Torati 22:24

watoeni nje katika lango la mji ule, mkawapige kwa mawe hata wafe; yule kijana, kwa kuwa hakupiga ukelele, naye yu ndani ya mji; na yule mume, kwa kuwa amemtweza mke wa mwenzake; ndivyo utakavyoondoa uovu katikati yako.

Kumbukumbu la Torati 22:25

Lakini yule mtu mume kama akimkuta kondeni kijana aliyeposwa, naye mume akamtenza nguvu, akalala naye; yule mtu mume aliyelala naye na afe pekee;

Kumbukumbu la Torati 22:26

lakini yule kijana usimfanye neno; hana dhambi yule kijana ipasayo kuuawa, kwa kuwa ni mfano wa mtu kumwondokea mwenzake akamwua, ni vivyo lilivyo jambo hili;

Kumbukumbu la Torati 22:27

kwani alimkuta kondeni; yule kijana aliyeposwa akalia, pasiwe na mtu wa kumwokoa.

Kumbukumbu la Torati 22:28

Mtu mume akimwona kijana aliye mwanamwali ambaye hajaposwa, akamshika na kulala naye, wakaonekana;

Kumbukumbu la Torati 22:29

yule mtu mume aliyelala naye na ampe baba yake yule kijana shekeli hamsini za fedha, kisha na awe mkewe, kwa kuwa amemtweza; hana ruhusa ya kumwacha siku zake zote.

Kumbukumbu la Torati 22:30

Mtu mume asimtwae mke wa baba yake, wala asifunue ncha ya mavazi ya baba yake.