Kumbukumbu la Torati Mlango 25 Deuteronomy

Kumbukumbu la Torati 25:1

Pakiwa na mashindano kati ya watu, wakaenda maamuzini, na hao waamuzi wakawaamua; na wampe haki mwenye haki, na wamhukumie makosa yule mwovu;

Kumbukumbu la Torati 25:2

na iwe, ikimpasa kupigwa yule mwovu, alazwe chini na mwamuzi, na kupigwa mbele ya uso wake, kwa kadiri ya uovu wake, kwa kuhesabu.

Kumbukumbu la Torati 25:3

Aweza kumpiga fimbo arobaini asizidishe asije akaonekana nduguyo kuwa amedharauliwa kwako, azidishapo kwa kumpiga fimbo nyingi juu ya hizi.

Kumbukumbu la Torati 25:4

Ng'ombe apurapo nafaka usimfunge kinywa.

Kumbukumbu la Torati 25:5

Watakapoketi pamoja mtu na nduguye, mmojawapo akafa, wala hana mwana wa kiume, mke wa yule aliyekufa asiolewe nje na mgeni; nduguye yule mumewe amwingilie amweke kwake awe mkewe, kumfanyia yampasayo nduguye mumewe.

Kumbukumbu la Torati 25:6

Na iwe, yule mzaliwa wa kwanza atakayemzaa, amfuate nduguye aliyekufa kwa jina lake, lisije likafutwa jina lake katika Israeli.

Kumbukumbu la Torati 25:7

Na yule mtu kwamba hapendi kumtwaa mke wa nduguye, aende huyo mke wa nduguye langoni kwa wazee, akawaambie, Nduguye mume wangu yuakataa kumsimamishia nduguye jina katika Israeli, hataki kunitimizia yampasayo nduguye mume wangu.

Kumbukumbu la Torati 25:8

Ndipo wamwite wazee wa mji wake waseme naye; naye akisimama na kusema, Sitaki mimi kumtwaa mwanamke huyu,

Kumbukumbu la Torati 25:9

ndipo mke wa nduguye amkaribie mbele ya hao wazee, amvue kiatu chake mguuni mwake, na kumtemea mate ya uso; kisha atajibu yule mwanamke, aseme, Mume akataaye kumjengea nduguye nyumba yake na afanywe hivi.

Kumbukumbu la Torati 25:10

Na jina lake katika Israeli liitwe, Nyumba ya mvuliwa kiatu.

Kumbukumbu la Torati 25:11

Washindanapo waume wao kwa wao, akakaribia mke wa mmojawapo, ili kumwokoa mumewe katika mkono wa ampigaye, yule mke akatoa mkono wake, na kumkamata tupu yake;

Kumbukumbu la Torati 25:12

umkate ule mkono wake, lisiwe na huruma jicho lako.

Kumbukumbu la Torati 25:13

Usiwe na mawe ya kupimia mbalimbali, kubwa na dogo, katika mfuko wako.

Kumbukumbu la Torati 25:14

Usiwe na vipimo mbalimbali, kikubwa na kidogo, katika nyumba yako.

Kumbukumbu la Torati 25:15

Uwe na jiwe timilifu la haki, uwe na kipimo kitimilifu cha haki; zipate kuwa nyingi siku zako, katika nchi akupayo Bwana, Mungu wako.

Kumbukumbu la Torati 25:16

Kwa kuwa wote wayatendao mambo kama haya, wote watendao yasiyo haki, ni machukizo kwa Bwana, Mungu wako.

Kumbukumbu la Torati 25:17

Kumbuka aliyokufanya Amaleki katika njia mlipokuwa mkitoka Misri;

Kumbukumbu la Torati 25:18

jinsi alivyokukuta katika njia, akapiga katika watu wako walioachwa nyuma, wote waliokuwa wanyonge nyuma yako, ulipokuwa umechoka na kuzimia; wala asimche Mungu.

Kumbukumbu la Torati 25:19

Basi itakuwa, hapo atakapokwisha kukupumzisha Bwana, Mungu wako, katika adui zako wote walio kando-kando, katika nchi akupayo Bwana, Mungu wako, iwe urithi uimiliki, ndipo uufute ukumbuko wa Amaleki chini ya mbingu; usisahau.