Mithali Mlango 16 Proverbs

Mithali 16:1

Maandalio ya moyo ni ya mwanadamu; Bali jawabu la ulimi hutoka kwa Bwana.

Mithali 16:2

Njia zote za mtu ni safi machoni pake mwenyewe; Bali Bwana huzipima roho za watu.

Mithali 16:3

Mkabidhi Bwana kazi zako, Na mawazo yako yatathibitika.

Mithali 16:4

Bwana amefanya kila kitu kwa kusudi lake; Naam, hata wabaya kwa siku ya ubaya.

Mithali 16:5

Kila mwenye moyo wa kiburi ni chukizo kwa Bwana; Hakika, hatakosa adhabu.

Mithali 16:6

Kwa rehema na kweli uovu husafishwa; Kwa kumcha Bwana watu hujiepusha na maovu.

Mithali 16:7

Njia za mtu zikimpendeza Bwana, Hata adui zake huwapatanisha naye.

Mithali 16:8

Afadhali mali kidogo pamoja na haki, Kuliko mapato mengi pamoja na udhalimu.

Mithali 16:9

Moyo wa mtu huifikiri njia yake; Bali Bwana huziongoza hatua zake.

Mithali 16:10

Kukata maneno huwa katika midomo ya mfalme; Kinywa chake hakitakosa katika hukumu.

Mithali 16:11

Mizani ya haki na vitanga vyake ni vya Bwana; Mawe yote ya mfukoni ni kazi yake.

Mithali 16:12

Wafalme wakitenda yasiyo haki ni chukizo; Maana kiti cha enzi huthibitika kwa haki.

Mithali 16:13

Midomo ya haki ni furaha ya wafalme; Nao humpenda yeye asemaye yaliyo sawa.

Mithali 16:14

Hasira ya mfalme ni kama wajumbe wa mauti; Lakini mtu mwenye hekima ataituliza.

Mithali 16:15

Kuna uhai katika nuru ya uso wa mfalme, Na fadhili zake ni kama wingu la masika.

Mithali 16:16

Si afadhali kupata hekima kuliko dhahabu? Naam, yafaa kuchagua ufahamu kuliko fedha.

Mithali 16:17

Njia kuu ya mwenye haki ni kujitenga na uovu; Yeye ashikaye njia yake huihifadhi nafsi yake.

Mithali 16:18

Kiburi hutangulia uangamivu; Na roho yenye kutakabari hutangulia maanguko.

Mithali 16:19

Afadhali kuwa na roho ya unyenyekevu pamoja na maskini, Kuliko kugawanya nyara pamoja na wenye kiburi.

Mithali 16:20

Atakayelitafakari neno atapata mema; Na kila amwaminiye Bwana ana heri.

Mithali 16:21

Aliye na hekima moyoni ataitwa mwenye busara; Utamu wa maneno huongeza elimu.

Mithali 16:22

Ufahamu ni chemchemi ya uzima kwake aliye nao; Bali kufundishwa kwa wapumbavu ni upuzi wao.

Mithali 16:23

Moyo wake mwenye hekima hufundisha kinywa chake; Huzidisha elimu ya midomo yake.

Mithali 16:24

Maneno yapendezayo ni kama sega la asali; Ni tamu nafsini, na afya mifupani.

Mithali 16:25

Iko njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu; Lakini mwisho wake ni njia za mauti.

Mithali 16:26

Nafsi yake mfanya kazi hujifanyia kazi; Maana kinywa chake humtia bidii.

Mithali 16:27

Mtu asiyefaa kitu huchimba shimo la madhara; Katika midomo yake mna moto uteketezao.

Mithali 16:28

Mtu mshupavu huondokesha fitina; Na mchongezi huwafarakanisha rafiki.

Mithali 16:29

Mtu mkali humshawishi mwenzake; Humwongoza katika njia isiyo njema.

Mithali 16:30

Afumbaye macho, kusudi lake ni kuwaza yaliyopotoka; Aikazaye midomo yake hutokeza mabaya.

Mithali 16:31

Kichwa chenye mvi ni taji ya utukufu, Kama kikionekana katika njia ya haki.

Mithali 16:32

Asiye mwepesi wa hasira ni mwema kuliko shujaa; Na mtu aitawalaye roho yake kuliko mtu atekaye mji.

Mithali 16:33

Kura hutupwa katika mikunjo ya nguo; Lakini hukumu zake zote ni za Bwana.