Mithali Mlango 8 Proverbs

Mithali 8:1

Je! Hekima halii? Ufahamu hatoi sauti yake?

Mithali 8:2

Juu ya mahali palipoinuka karibu na njia, Penye njia panda, ndipo asimamapo.

Mithali 8:3

Karibu na malango, mahali pa kuingia mjini, Mahali pa kuyaingilia malango anapiga kelele.

Mithali 8:4

Enyi watu, nawaita ninyi; Na sauti yangu ni kwa wanadamu.

Mithali 8:5

Enyi wajinga, fahamuni werevu, Nanyi wapumbavu, mpate moyo wa kufahamu.

Mithali 8:6

Sikieni, maana nitasema yaliyo mazuri, Na kufumbua midomo yangu kutakuwa maadili.

Mithali 8:7

Maana kinywa changu kitasema kweli, Na uovu ni chukizo kwa midomo yangu.

Mithali 8:8

Maneno yote ya kinywa changu yana haki; Hapana hata neno lililopotoka au la ukaidi.

Mithali 8:9

Yote humwelea yule afahamuye, Yote huelekea mbele yao waliopata maarifa.

Mithali 8:10

Pokea mafundisho yangu, wala si fedha, Na maarifa kuliko dhahabu safi.

Mithali 8:11

Maana hekima ni bora kuliko marijani; Wala vyote vinavyotamanika havilingani nayo.

Mithali 8:12

Mimi, hekima, nimefanya werevu kuwa kao langu; Natafuta maarifa na busara.

Mithali 8:13

Kumcha Bwana ni kuchukia uovu; Kiburi na majivuno, na njia mbovu, Na kinywa cha ukaidi pia nakichukia.

Mithali 8:14

Shauri ni langu, na maarifa yaliyo sahihi; Mimi ni ufahamu, mimi nina nguvu.

Mithali 8:15

Kwa msaada wangu wafalme humiliki, Na wakuu wanahukumu haki.

Mithali 8:16

Kwa msaada wangu wakuu hutawala, Na waungwana, naam, waamuzi wote wa dunia.

Mithali 8:17

Nawapenda wale wanipendao, Na wale wanitafutao kwa bidii wataniona.

Mithali 8:18

Utajiri na heshima ziko kwangu, Naam, utajiri udumuo, na haki pia.

Mithali 8:19

Matunda yangu hupita dhahabu, naam, dhahabu safi, Na faida yangu hupita fedha iliyo teule.

Mithali 8:20

Natembea katika njia ya haki, Katikati ya mapito ya hukumu.

Mithali 8:21

Niwarithishe mali wale wanipendao, Tena nipate kuzijaza hazina zao.

Mithali 8:22

Bwana alikuwa nami katika mwanzo wa njia yake, Kabla ya matendo yake ya kale.

Mithali 8:23

Nalitukuka tokea milele, tangu awali, Kabla haijawako dunia.

Mithali 8:24

Wakati visipokuwako vilindi nalizaliwa, Wakati zisipokuwako chemchemi zilizojaa maji.

Mithali 8:25

Kabla milima haijawekwa imara, Kabla ya vilima nalizaliwa.

Mithali 8:26

Alipokuwa hajaiumba dunia, wala makonde Wala chanzo cha mavumbi ya dunia;

Mithali 8:27

Alipozithibitisha mbingu nalikuwako; Alipopiga duara katika uso wa bahari;

Mithali 8:28

Alipofanya imara mawingu yaliyo juu; Chemchemi za bahari zilipopata nguvu;

Mithali 8:29

Alipoipa bahari mpaka wake, Kwamba maji yake yasiasi amri yake; Alipoiagiza misingi ya nchi;

Mithali 8:30

Ndipo nilipokuwa pamoja naye, kama stadi wa kazi; Nikawa furaha yake kila siku; Nikifurahi daima mbele zake;

Mithali 8:31

Nikiifurahia dunia inayokaliwa na watu; Na furaha yangu ilikuwa pamoja na wanadamu.

Mithali 8:32

Basi, wanangu, nisikilizeni sasa; Maana heri hao wazishikao amri zangu.

Mithali 8:33

Sikieni mafundisho, mpate hekima, Wala msiikatae.

Mithali 8:34

Ana heri mtu yule anisikilizaye, Akisubiri sikuzote malangoni pangu, Akingoja penye vizingiti vya milango yangu.

Mithali 8:35

Maana yeye anionaye mimi aona uzima, Naye atapata kibali kwa Bwana.

Mithali 8:36

Bali anikosaye hujidhuru nafsi yake mwenyewe, Na wao wanichukiao hupenda mauti.