Mithali Mlango 25 Proverbs

Mithali 25:1

Hizi nazo ni mithali za Sulemani, ambazo watu wa Hezekia, mfalme wa Yuda, walizinakili.

Mithali 25:2

Ni utukufu wa Mungu kuficha jambo; Bali ni utukufu wa mfalme kuchunguza jambo.

Mithali 25:3

Mbingu huenda juu sana, na nchi huenda chini; Lakini mioyo ya wafalme haichunguziki.

Mithali 25:4

Ondoa takataka katika fedha, Na chombo kitatokea kwa mtakasaji;

Mithali 25:5

Mwondoe asiye haki mbele ya mfalme, Na kiti chake cha enzi kitathibitika katika haki.

Mithali 25:6

Usijitukuze mbele ya uso wa mfalme; Wala usisimame mahali pa watu wakuu;

Mithali 25:7

Kwa maana ni heri kuambiwa, Njoo huku mbele; Kuliko kuwekwa nyuma machoni pa mkuu. Yale uliyoyaona kwa macho,

Mithali 25:8

Usitoke nje kwa haraka ili kuyashindania; Usije ukakosa kujua la kutenda hatimaye, Mwenzako atakapokuwa amekuaibisha.

Mithali 25:9

Ujitetee na mwenzako peke yake; Bali usiifunue siri ya mtu mwingine;

Mithali 25:10

Yeye asikiaye asije akakutukana; Na aibu yako isiondoke.

Mithali 25:11

Neno linenwalo wakati wa kufaa, Ni kama machungwa katika vyano vya fedha.

Mithali 25:12

Kipuli cha dhahabu, na pambo la dhahabu safi; Ndivyo alivyo mwonyaji mwenye hekima kwa sikio lisikialo.

Mithali 25:13

Kama baridi ya theluji wakati wa mavuno; Ndivyo alivyo mjumbe mwaminifu kwao wamtumao; Kwa maana huwaburudisha bwana zake nafsi zao.

Mithali 25:14

Kama mawingu na upepo pasipo mvua; Ndivyo alivyo yeye ajisifiaye karama kwa uongo.

Mithali 25:15

Kwa uvumilivu mwingi mkuu husadikishwa; Na ulimi laini huvunja mfupa.

Mithali 25:16

Je! Umeona asali? Kula kadiri ya kukutosha; Usije ukashiba na kuitapika.

Mithali 25:17

Mguu wako usiingie katika nyumba ya jirani yako ila kwa kiasi; Asije akakukinai na kukuchukia.

Mithali 25:18

Mtu amshuhudiaye jirani yake uongo Ni nyundo, na upanga, na mshale mkali.

Mithali 25:19

Kumtumaini asiye mwaminifu wakati wa taabu Ni kama jino lililovunjika, au mguu ulioteguka.

Mithali 25:20

Amwimbiaye nyimbo mtu mwenye moyo mzito, Ni kama yeye avuaye nguo wakati wa baridi; Ni kama siki juu ya magadi.

Mithali 25:21

Adui yako akiwa ana njaa, mpe chakula; Tena akiwa ana kiu, mpe maji ya kunywa;

Mithali 25:22

Maana utatia makaa ya moto kichwani pake; Na Bwana atakupa thawabu.

Mithali 25:23

Upepo wa kusi huleta mvua; Vile vile asingiziaye huleta uso wa ghadhabu.

Mithali 25:24

Ni afadhali kukaa katika pembe ya darini, Kuliko katika nyumba pana pamoja na mwanamke mgomvi.

Mithali 25:25

Kama vile maji ya baridi kwa mtu mwenye kiu, Ndivyo ilivyo habari njema itokayo katika nchi ya mbali.

Mithali 25:26

Mwenye haki amwangukiapo mtu mbaya Ni kama chemchemi iliyochafuka, Na kisima kilichokanyagwa.

Mithali 25:27

Haifai kula asali nyingi mno; Vile vile mtu kutafuta utukufu wake mwenyewe si utukufu.

Mithali 25:28

Asiyetawala roho yake Ni mfano wa mji uliobomolewa, usio na kuta.