Mithali Mlango 4 Proverbs

Mithali 4:1

Wanangu, yasikilizeni mausia ya baba yenu, Tegeni masikio mpate kujua ufahamu.

Mithali 4:2

Kwa kuwa nawapa mafundisho mazuri; Msiiache sheria yangu.

Mithali 4:3

Maana nalikuwa mwana kwa baba yangu, Mpole, mpenzi wa pekee wa mama yangu.

Mithali 4:4

Naye akanifundisha, akaniambia, Moyo wako uyahifadhi maneno yangu; Shika amri zangu ukaishi.

Mithali 4:5

Jipatie hekima, jipatie ufahamu; usiusahau; Wala usiyakatae maneno ya kinywa changu.

Mithali 4:6

Usimwache, naye atakuhifadhi; Umpende, naye atakulinda.

Mithali 4:7

Bora hekima, basi jipatie hekima; Naam, kwa mapato yako yote jipatie ufahamu.

Mithali 4:8

Umtukuze, naye atakukuza; Atakupatia heshima, ukimkumbatia.

Mithali 4:9

Atakupa neema kuwa kilemba kichwani; Na kukukirimia taji ya uzuri.

Mithali 4:10

Mwanangu, sikiliza, na kuzipokea kauli zangu; Na miaka ya maisha yako itakuwa mingi.

Mithali 4:11

Nimekufundisha katika njia ya hekima; Nimekuongoza katika mapito ya unyofu.

Mithali 4:12

Uendapo, hatua zako hazitadhiikika, Wala ukipiga mbio hutajikwaa.

Mithali 4:13

Mkamate sana elimu, usimwache aende zake; Mshike, maana yeye ni uzima wako.

Mithali 4:14

Usiingie katika njia ya waovu, Wala usitembee katika njia ya wabaya.

Mithali 4:15

Jiepushe nayo, usipite karibu nayo, Igeukie mbali, ukaende zako.

Mithali 4:16

Maana hawalali isipokuwa wametenda madhara; Huondolewa usingizi, ikiwa hawakumwangusha mtu.

Mithali 4:17

Maana wao hula mkate wa uovu, Nao hunywa divai ya jeuri.

Mithali 4:18

Bali njia ya wenye haki ni kama nuru ing'aayo, Ikizidi kung'aa hata mchana mkamilifu.

Mithali 4:19

Njia ya waovu ni kama giza; Hawajui ni kitu gani kiwakwazacho.

Mithali 4:20

Mwanangu, sikiliza maneno yangu; Tega sikio lako, uzisikie kauli zangu.

Mithali 4:21

Zisiondoke machoni pako; Uzihifadhi ndani ya moyo wako.

Mithali 4:22

Maana ni uhai kwa wale wazipatao, Na afya ya mwili wao wote.

Mithali 4:23

Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo; Maana ndiko zitokako chemchemi za uzima.

Mithali 4:24

Kinywa cha ukaidi ukitenge nawe, Na midomo ya upotovu uiweke mbali nawe.

Mithali 4:25

Macho yako yatazame mbele, Na kope zako zitazame mbele yako sawasawa.

Mithali 4:26

Ulisawazishe pito la mguu wako, Na njia zako zote zithibitike;

Mithali 4:27

Usigeuke kwa kuume wala kwa kushoto; Ondoa mguu wako maovuni.