Mithali Mlango 29 Proverbs

Mithali 29:1

Aonywaye mara nyingi akishupaza shingo, Atavunjika ghafula, wala hapati dawa.

Mithali 29:2

Wenye haki wakiwa na amri, watu hufurahi; Bali mwovu atawalapo, watu huugua.

Mithali 29:3

Apendaye hekima humfurahisha babaye; Bali ashikamanaye na makahaba hutapanya mali.

Mithali 29:4

Mfalme huithibitisha nchi kwa hukumu; Bali yeye apokeaye rushwa huipindua.

Mithali 29:5

Mwenye kujipendekeza kwa jirani yake, Hutandika wavu ili kuitega miguu yake.

Mithali 29:6

Kuna mtego katika kosa la mtu mbaya; Bali mwenye haki huimba na kufurahi.

Mithali 29:7

Mwenye haki huyaangalia madai ya maskini; Bali mtu mbaya hana ufahamu hata ayajue.

Mithali 29:8

Watu wenye dharau huwasha mji moto; Bali wenye hekima hugeuzia mbali ghadhabu.

Mithali 29:9

Mwenye hekima akijadiliana na mpumbavu; Akikasirika au akicheka, pia hapana raha.

Mithali 29:10

Wamwagao damu humchukia mtu mkamilifu; Bali wenye haki humtunza nafsi yake.

Mithali 29:11

Mpumbavu hudhihirisha hasira yake yote; Bali mwenye hekima huizuia na kuituliza.

Mithali 29:12

Mwenye kutawala akisikiliza uongo; Basi watumishi wake wote watakuwa waovu.

Mithali 29:13

Maskini na mdhalimu hukutana pamoja; Bwana huwatia nuru macho yao wote wawili.

Mithali 29:14

Mfalme awahukumuye maskini kwa uaminifu; Kiti chake cha enzi kitathibitika milele.

Mithali 29:15

Fimbo na maonyo hutia hekima; Bali mwana aliyeachiliwa humwaibisha mamaye.

Mithali 29:16

Waovu wakiongezeka, maasi huongezeka; Bali wenye haki watayatazama maanguko yao.

Mithali 29:17

Mrudi mwanao naye atakustarehesha; Naam, atakufurahisha nafsi yako.

Mithali 29:18

Pasipo maono, watu huacha kujizuia; Bali ana heri mtu yule aishikaye sheria.

Mithali 29:19

Haitoshi mtumwa kuonywa kwa maneno; Maana ajapoyafahamu hataitika.

Mithali 29:20

Je! Umemwona mtu mwenye kuhamaki katika maneno? Afadhali kumtumaini mpumbavu kuliko yeye.

Mithali 29:21

Amtunduiaye mtumwa wake tangu utoto, Mwisho wake atakuwa ni mwanawe.

Mithali 29:22

Mtu wa hasira huchochea ugomvi; Na mtu mwenye ghadhabu huasi sana.

Mithali 29:23

Kiburi cha mtu kitamshusha; Bali mwenye roho ya unyenyekevu ataheshimiwa.

Mithali 29:24

Mshiriki wa mwivi huichukia nafsi yake mwenyewe; Asikia maapizo, wala hana neno.

Mithali 29:25

Kuwaogopa wanadamu huleta mtego; Bali amtumainiye Bwana atakuwa salama.

Mithali 29:26

Watu wengi hutafuta upendeleo wa mkuu; Bali hukumu ya kila mtu hutoka kwa Bwana

Mithali 29:27

Mtu aliye dhalimu ni chukizo kwa wenye haki; Na mnyofu wa mwenendo ni chukizo kwa waovu.