Mithali Mlango 30 Proverbs

Mithali 30:1

Maneno ya Aguri bin Yake; mausia mtu huyu aliyomwambia Ithieli, naam, Ithieli na Ukali.

Mithali 30:2

Hakika nimekuwa kama mnyama, wala si mtu; Wala sina ufahamu wa mwanadamu;

Mithali 30:3

Wala sikujifunza hekima; Wala sina maarifa ya kumjua Mtakatifu.

Mithali 30:4

Ni nani aliyepanda mbinguni na kushuka chini? Ni nani aliyekamata upepo kwa makonzi yake? Ni nani aliyeyafunga maji ndani ya nguo yake? Ni nani aliyefanya imara ncha zote za nchi? Jina lake ni nani? Na ni nani jina la mwanawe, kama wajua?

Mithali 30:5

Kila neno la Mungu limehakikishwa; Yeye ni ngao yao wamwaminio.

Mithali 30:6

Usiongeze neno katika maneno yake; Asije akakulaumu, ukaonekana u mwongo.

Mithali 30:7

Mambo haya mawili nimekuomba; Usininyime [matatu] kabla sijafa.

Mithali 30:8

Uniondolee ubatili na uongo; Usinipe umaskini wala utajiri; Unilishe chakula kilicho kadiri yangu.

Mithali 30:9

Nisije nikashiba nikakukana, Nikasema, Bwana ni nani? Wala nisiwe maskini sana nikaiba, Na kulitaja bure jina la Mungu wangu.

Mithali 30:10

Usimchongee mtumwa kwa bwana wake; Asije akakulaani, ukaonekana una hatia.

Mithali 30:11

Kuna kizazi cha watu wamlaanio baba yao; Wala hawambariki mama yao.

Mithali 30:12

Kuna kizazi cha watu walio safi machoni pao wenyewe; Ambao hawakuoshwa uchafu wao.

Mithali 30:13

Kuna kizazi cha watu ambao macho yao yameinuka kama nini! Na kope zao zimeinuka sana.

Mithali 30:14

Kuna kizazi cha watu ambao meno yao ni panga; Na vigego vyao ni kama visu. Ili kuwala maskini waondolewe katika nchi, Na wahitaji katika wanadamu.

Mithali 30:15

Mruba anao binti wawili, Waliao, Nipe! Nipe! Kuna vitu vitatu visivyoshiba kamwe, Naam, vinne visivyosema, Basi!

Mithali 30:16

Kuzimu; na tumbo lisilozaa; Nchi isiyoshiba maji; na moto usiosema, Basi!

Mithali 30:17

Jicho la mtu amdhihakiye babaye, Na kudharau kumtii mamaye; Kunguru wa bondeni wataling'oa, Na vifaranga vya tai watalila.

Mithali 30:18

Kuna mambo matatu yaliyo ya ajabu kwangu, Naam, kuna manne nisiyoyafahamu.

Mithali 30:19

Mwendo wa tai katika hewa; Na mwendo wa nyoka juu ya mwamba; Mwendo wa merikebu katikati ya bahari; Na mwendo wa mtu pamoja na msichana.

Mithali 30:20

Hivyo ndivyo mwendo wa mwanamke mzinifu; Hula, akapangusa kinywa chake, Akasema, Sikufanya uovu.

Mithali 30:21

Kwa ajili ya mambo matatu nchi hutetemeka, Naam, kwa ajili ya manne haiwezi kuvumilia.

Mithali 30:22

Mtumwa apatapo kuwa mfalme; Mpumbavu ashibapo chakula;

Mithali 30:23

Mwanamke mwenye kuchukiza aolewapo; Na mjakazi aliye mrithi wa bibi yake.

Mithali 30:24

Kuna viumbe vinne duniani vilivyo vidogo; Lakini vina akili nyingi sana.

Mithali 30:25

Chungu ni watu wasio na nguvu; Lakini hujiwekea chakula wakati wa hari.

Mithali 30:26

Wibari ni watu dhaifu; Lakini hujifanyia nyumba katika miamba.

Mithali 30:27

Nzige hawana mfalme; Lakini huenda wote pamoja vikosi vikosi.

Mithali 30:28

Mjusi hushika kwa mikono yake; Lakini yumo majumbani mwa wafalme.

Mithali 30:29

Kuna watatu wenye mwendo wa kupendeza, Naam, wanne walio na mwendo mzuri.

Mithali 30:30

Simba aliye hodari kupita wanyama wote; Wala hajiepushi na aliye yote;

Mithali 30:31

Jimbi aendaye tambo; na beberu; Na mfalme ambaye haasiki.

Mithali 30:32

Ikiwa umefanya kipumbavu kwa kujikuza; Au ikiwa umewaza mabaya; Basi weka mkono wako juu ya kinywa chako.

Mithali 30:33

Kwa maana kupiga maziwa huleta siagi; Na kupiga pua hutokeza damu; kadhalika kuchochea hasira hutokeza ugomvi.