Mithali Mlango 9 Proverbs

Mithali 9:1

Hekima umeijenga nyumba yake, Amezichonga nguzo zake saba;

Mithali 9:2

Amechinja nyama zake, umechanganya divai yake, Ameiandalia meza yake pia.

Mithali 9:3

Amewatuma wajakazi wake, analia, Mahali pa mjini palipoinuka sana,

Mithali 9:4

Kila aliye mjinga na aingie humu. Tena amwambia mtu aliyepungukiwa na akili,

Mithali 9:5

Njoo ule mkate wangu, Ukanywe divai niliyoichanganya.

Mithali 9:6

Enyi wajinga, acheni ujinga, mkaishi, Mkaende katika njia ya ufahamu.

Mithali 9:7

Amkemeaye mwenye dharau hujipatia fedheha; Amkaripiaye mtu mbaya hujipatia aibu.

Mithali 9:8

Usimkaripie mwenye dharau, asije akakuchukia; Mkaripie mwenye hekima, naye atakupenda.

Mithali 9:9

Mwelimishe mwenye hekima, naye atazidi kuwa na hekima; Mfundishe mwenye haki, naye atazidi kuwa na elimu;

Mithali 9:10

Kumcha Bwana ni mwanzo wa hekima; Na kumjua Mtakatifu ni ufahamu.

Mithali 9:11

Maana, kwa msaada wangu siku zako zitazidishwa; Na miaka ya maisha yako itaongezwa.

Mithali 9:12

Kama una hekima, una hekima kwa nafsi yako; Na kama una dharau, utaichukua peke yako.

Mithali 9:13

Mwanamke mpumbavu hupiga kelele, Ni mjinga, hajui kitu.

Mithali 9:14

Hukaa mlangoni pa nyumba yake, Juu ya kiti mahali pa mjini palipoinuka,

Mithali 9:15

Apate kuwaita wapitao njiani, Waendao moja kwa moja katika njia zao.

Mithali 9:16

Kila aliye mjinga na aingie humu. Tena amwambia mtu aliyepungukiwa na akili,

Mithali 9:17

Maji yaliyoibiwa ni matamu, Na mkate ulioliwa kwa siri hupendeza.

Mithali 9:18

Lakini huyo hajui ya kuwa wafu wamo humo; Ya kuwa wageni wake wamo chini kuzimuni.