Mithali Mlango 11 Proverbs

Mithali 11:1

Mizani ya hadaa ni chukizo kwa Bwana; Bali vipimo vilivyo sawasawa humpendeza.

Mithali 11:2

Kijapo kiburi ndipo ijapo aibu; Bali hekima hukaa na wanyenyekevu.

Mithali 11:3

Ukamilifu wao wenye haki utawaongoza Bali ukaidi wao wenye fitina utawaangamiza.

Mithali 11:4

Mali hazifaidii kitu siku ya ghadhabu; Bali haki huokoa na mauti.

Mithali 11:5

Haki yake mtu mkamilifu itamwongoza njia yake; Bali mtu mwovu ataanguka kwa uovu wake.

Mithali 11:6

Haki yao wenye haki itawaokoa; Bali wafanyao fitina watanaswa kwa hila yao wenyewe.

Mithali 11:7

Mtu mwovu atakapokufa, taraja lake lapotea; Na matumaini ya uovu huangamia.

Mithali 11:8

Mwenye haki huokolewa katika dhiki, Na mtu mwovu ataiingia badala yake.

Mithali 11:9

Asiyemcha Mungu humpoteza jirani yake kwa kinywa chake; Bali wenye haki watapona kwa maarifa.

Mithali 11:10

Wenye haki wasitawipo, mji hufurahi; Waovu waangamiapo, watu hupiga kelele.

Mithali 11:11

Mji hutukuzwa kwa mbaraka wa mwenye haki; Bali mji hupinduliwa kwa kinywa cha mwovu.

Mithali 11:12

Asiye na akili humdharau mwenziwe; Bali mtu aliye na ufahamu hunyamaza.

Mithali 11:13

Mwenye kitango akisingizia hufunua siri; Bali mwenye roho ya uaminifu husitiri mambo.

Mithali 11:14

Pasipo mashauri taifa huanguka; Bali kwa wingi wa washauri huja wokovu.

Mithali 11:15

Amdhaminiye mgeni hakosi ataumia; Achukiaye mambo ya dhamana yu salama.

Mithali 11:16

Mwanamke wa adabu huheshimiwa daima; Na watu wakali hushika mali siku zote.

Mithali 11:17

Mwenye rehema huitendea mema nafsi yake; Aliye mkali hujisumbua mwili wake.

Mithali 11:18

Mtu mwovu hupata mshahara wa udanganyifu; Apandaye haki ana thawabu ya hakika.

Mithali 11:19

Haki huelekea uzima; Afuataye maovu hufuata mauti yake mwenyewe.

Mithali 11:20

Wenye kuhalifu moyoni ni chukizo kwa Bwana; Walio wakamilifu katika njia zao humpendeza.

Mithali 11:21

Hakika, mtu mwovu hatakosa adhabu; Bali wazao wa wenye haki wataokoka.

Mithali 11:22

Kama pete ya dhahabu katika pua ya nguruwe, Kadhalika mwanamke mzuri asiye na akili.

Mithali 11:23

Haja ya mwenye haki ni mema tu; Bali kutaraji kwake mtu mwovu ni ghadhabu.

Mithali 11:24

Kuna atawanyaye, lakini huongezewa zaidi; Kuna azuiaye isivyo haki, lakini huelekea uhitaji.

Mithali 11:25

Nafsi ya mtu mkarimu itawandishwa; Anyweshaye atanyweshwa mwenyewe.

Mithali 11:26

Awanyimaye watu nafaka, watu watamlaani; Auzaye nafaka, baraka itakuwa kichwani pake.

Mithali 11:27

Atafutaye mema kwa bidii hutafuta fadhili; Atafutaye madhara, hayo yatamjia.

Mithali 11:28

Azitegemeaye mali zake ataanguka; Mwenye haki atasitawi kama jani.

Mithali 11:29

Ataabishaye nyumba yake mwenyewe ataurithi upepo; Mpumbavu atakuwa mtumwa wa mtu mwenye moyo wa akili.

Mithali 11:30

Mazao ya mwenye haki ni mti wa uzima; Na mwenye hekima huvuta roho za watu.

Mithali 11:31

Tazama, mwenye haki atalipwa duniani; Basi mwovu na mkosaji si mara nyingi zaidi?