Mithali Mlango 17 Proverbs

Mithali 17:1

Afadhali mego kavu pamoja na utulivu, Kuliko nyumba yenye karamu nyingi pamoja na magomvi.

Mithali 17:2

Mtumwa atendaye kwa busara atamtawala mwana atendaye mambo ya aibu; Tena atapata sehemu ya urithi kati ya ndugu.

Mithali 17:3

Kalibuni kwa fedha, na tanuru kwa dhahabu; Bali Bwana huijaribu mioyo.

Mithali 17:4

Mtenda mabaya husikiliza midomo ya uovu; Na mwongo hutega sikio lake kusikiliza ulimi wa madhara.

Mithali 17:5

Amdhihakiye maskini humsuta Muumba wake; Naye aufurahiaye msiba hatakosa adhabu.

Mithali 17:6

Wana wa wana ndio taji ya wazee, Na utukufu wa watoto ni baba zao.

Mithali 17:7

Maneno mazuri hayapendezi kinywani mwa mpumbavu; Siuze midomo ya uongo kinywani mwa mkuu.

Mithali 17:8

Kipawa ni kama kito cha thamani machoni pake yeye aliye nacho; Kila kigeukapo hufanikiwa.

Mithali 17:9

Afunikaye kosa hutafuta kupendwa; Bali yeye akashifuye neno hutenga rafiki.

Mithali 17:10

Lawama hupenya moyoni mwa mwenye ufahamu, Kuliko mapigo mia moyoni mwa mpumbavu.

Mithali 17:11

Mtu mwovu hataki neno ila kuasi tu; Kwa hiyo mjumbe mkali atatumwa kwake.

Mithali 17:12

Afadhali mtu akutwe na dubu aliyenyang'anywa watoto wake, Kuliko na mpumbavu katika upumbavu wake.

Mithali 17:13

Yeye arudishaye mabaya badala ya mema, Mabaya hayataondoka nyumbani mwake.

Mithali 17:14

Mwanzo wa ugomvi ni kama kutoboa penye maji; Basi acheni ugomvi kabla haujafurika.

Mithali 17:15

Yeye asemaye kwamba asiye haki ana haki; naye asemaye kwamba mwenye haki hana haki; Hao wote wawili ni chukizo kwa Bwana.

Mithali 17:16

Nini maana yake, mpumbavu kuwa na fedha mkononi mwake ya kununulia hekima, Ikiwa hana moyo wa ufahamu?

Mithali 17:17

Rafiki hupenda sikuzote; Na ndugu amezaliwa kwa siku ya taabu.

Mithali 17:18

Aliyepungukiwa na akili hupana mkono na mtu; Na kuwa mdhamini mbele ya mwenzake.

Mithali 17:19

Apendaye ugomvi hupenda dhambi; Auinuaye sana mlango wake hutafuta uharibifu.

Mithali 17:20

Mtu mwenye moyo wa ukaidi hatapata mema; Na mwenye ulimi wa upotofu huanguka katika misiba.

Mithali 17:21

Azaaye mpumbavu ni kwa huzuni yake mwenyewe; Wala baba wa mpumbavu hana furaha.

Mithali 17:22

Moyo uliochangamka ni dawa nzuri; Bali roho iliyopondeka huikausha mifupa.

Mithali 17:23

Asiye haki hutoa rushwa kifuani, Ili kuzipotosha njia za hukumu.

Mithali 17:24

Hekima huwa machoni pake mwenye ufahamu; Bali macho ya mpumbavu huwa katika ncha za dunia.

Mithali 17:25

Mwana mpumbavu ni huzuni kwa babaye, Na uchungu kwa mamaye aliyemzaa.

Mithali 17:26

Tena kumwadhibu mwenye haki si vizuri; Wala si kwema kuwapiga wakuu kwa unyofu wao.

Mithali 17:27

Azuiaye maneno yake ni mwenye maarifa; Na mwenye roho ya utulivu ana busara.

Mithali 17:28

Hata mpumbavu akinyamaza, huhesabiwa hekima; Akifumba midomo yake, huhesabiwa ufahamu.