Mithali Mlango 19 Proverbs

Mithali 19:1

Afadhali maskini aendaye katika unyofu wake, Kuliko mpotofu wa midomo aliye mpumbavu.

Mithali 19:2

Tena si vizuri nafsi ya mtu ikose maarifa; Naye afanyaye haraka kwa miguu hutenda dhambi.

Mithali 19:3

Upumbavu wa mtu hupotosha njia yake; Na moyo wake hununa juu ya Bwana.

Mithali 19:4

Utajiri huongeza rafiki wengi; Bali maskini hutengwa na rafiki yake.

Mithali 19:5

Shahidi wa uongo hakosi ataadhibiwa; Wala asemaye uongo hataokoka.

Mithali 19:6

Watu wengi watamsihi mkuu ili awafadhili; Na kila mtu ni rafiki yake atoaye tunu.

Mithali 19:7

Ndugu zote wa maskini humchukia; Jinsi gani rafiki zake huzidi kujitenga naye! Huwafuata kwa maneno, lakini wametoweka.

Mithali 19:8

Apataye hekima hujipenda nafsi yake; Ashikaye ufahamu atapata mema.

Mithali 19:9

Shahidi wa uongo hakosi ataadhibiwa; Naye asemaye uongo ataangamia.

Mithali 19:10

Maisha ya anasa hayampasi mpumbavu; Sembuse mtumwa awatawale wakuu.

Mithali 19:11

Busara ya mtu huiahirisha hasira yake; Nayo ni fahari yake kusamehe makosa.

Mithali 19:12

Ghadhabu ya mfalme ni kama ngurumo ya simba; Bali hisani yake kama umande juu ya majani.

Mithali 19:13

Mwana mpumbavu ni msiba kwa babaye; Na ugomvi wa mke kama kutona-tona daima.

Mithali 19:14

Nyumba na mali ni urithi apatao mtu kwa babaye; Bali mke mwenye busara, mtu hupewa na Bwana.

Mithali 19:15

Uvivu humtia mtu katika usingizi mzito; Na nafsi yake mvivu itaona njaa.

Mithali 19:16

Yeye aihifadhiye amri huihifadhi nafsi yake; Bali yeye asiyeziangalia njia zake atakufa.

Mithali 19:17

Amhurumiaye maskini humkopesha Bwana; Naye atamlipa kwa tendo lake jema.

Mithali 19:18

Mrudi mwanao, kwa maana liko tumaini; Wala usiikaze nafsi yako kwa kuangamia kwake.

Mithali 19:19

Mtu wa hasira nyingi atachukua adhabu yake, Maana ujapomwokoa huna budi kufanya tena.

Mithali 19:20

Sikiliza mashauri, ukapokee mafundisho, Upate kuwa na hekima siku zako za mwisho.

Mithali 19:21

Mna hila nyingi moyoni mwa mtu; Lakini shauri la Bwana ndilo litakalosimama.

Mithali 19:22

Haja ya mwanadamu ni hisani yake; Ni afadhali maskini kuliko mwongo.

Mithali 19:23

Kumcha Bwana huelekea uhai; Atakaa ameshiba; hatajiliwa na ubaya.

Mithali 19:24

Mtu mvivu hutia mkono wake sahanini; Ila hataki hata kuupeleka kinywani pake.

Mithali 19:25

Mpige mwenye mzaha, na mjinga atapata busara; Mwonye mwenye ufahamu, naye atatambua maarifa.

Mithali 19:26

Apotezaye mali za babaye na kumfukuza mamaye, Ni mwana aaibishaye, na kuleta lawama.

Mithali 19:27

Mwanangu, acha kusikia mafundisho, Ukitaka tu kuyaasi maneno ya maarifa.

Mithali 19:28

Shahidi asiyefaa kitu hudhihaki hukumu, Na vinywa vya wasio haki humeza uovu.

Mithali 19:29

Hukumu zimewekwa tayari kwa wenye mzaha; Na mapigo kwa mgongo wa wapumbavu.