Mithali Mlango 5 Proverbs

Mithali 5:1

Mwanangu, sikiliza hekima yangu; Tega sikio lako, mzisikie akili zangu;

Mithali 5:2

Upate kuilinda busara, Na midomo yako iyahifadhi maarifa.

Mithali 5:3

Maana midomo ya malaya hudondoza asali, Na kinywa chake ni laini kuliko mafuta;

Mithali 5:4

Lakini mwisho wake ni mchungu kuliko pakanga; Ni mkali kama upanga wa makali kuwili.

Mithali 5:5

Miguu yake inatelemkia mauti; Hatua zake zinashikamana na kuzimu;

Mithali 5:6

Hata asiweze kuiona njia sawa ya uzima; Njia zake ni za kutanga-tanga wala hana habari.

Mithali 5:7

Basi, wanangu, nisikilizeni sasa, Wala msiache maneno ya kinywa changu.

Mithali 5:8

Itenge njia yako mbali naye, Wala usiukaribie mlango wa nyumba yake.

Mithali 5:9

Usije ukawapa wengine heshima yako, Na wakorofi miaka yako;

Mithali 5:10

Wageni wasije wakashiba nguvu zako; Kazi zako zikawa ndani ya nyumba ya mgeni;

Mithali 5:11

Nawe ukaziombolea siku zako za mwisho, Nyama yako na mwili wako utakapoangamia;

Mithali 5:12

Ukasema, Jinsi nilivyochukia maonyo, Na moyo wangu ukadharau kukemewa;

Mithali 5:13

Wala sikuisikia sauti ya waalimu wangu, Wala sikuwategea sikio langu walionifundisha!

Mithali 5:14

Nalikuwa karibu na kuingia katika maovu yote, Katikati ya mkutano na kusanyiko.

Mithali 5:15

Unywe maji ya birika lako mwenyewe, Na maji yenye kububujika katika kisima chako.

Mithali 5:16

Je! Chemchemi zako zitawanyike mbali, Na mito ya maji katika njia kuu?

Mithali 5:17

Yawe yako mwenyewe peke yako, Wala si ya wageni pamoja nawe.

Mithali 5:18

Chemchemi yako ibarikiwe; Nawe umfurahie mke wa ujana wako.

Mithali 5:19

Ni ayala apendaye na paa apendezaye; Maziwa yake yakutoshe sikuzote; Na kwa upendo wake ushangilie daima.

Mithali 5:20

Mwanangu! Mbona unashangilia malaya, Na kukikumbatia kifua cha mgeni?

Mithali 5:21

Kwa maana njia za mwanadamu zi mbele za macho ya Bwana, Na mienendo yake yote huitafakari.

Mithali 5:22

Maovu yake yeye yatampata mdhalimu, Naye atashikwa kwa kamba za dhambi zake.

Mithali 5:23

Atakufa huyo kwa kukosa maonyo, Naye atapotea kwa wingi wa ujinga wake.