Mithali Mlango 24 Proverbs

Mithali 24:1

Usiwahusudu watu waovu, Wala usitamani kuwa pamoja nao;

Mithali 24:2

Kwa maana moyo wao hufikiri dhuluma, Na midomo yao huongea madhara.

Mithali 24:3

Nyumba hujengwa kwa hekima, Na kwa ufahamu huthibitika,

Mithali 24:4

Na kwa maarifa vyumba vyake hujazwa Vitu vyote vya thamani na vya kupendeza.

Mithali 24:5

Mtu mwenye hekima ana nguvu; Naam, mtu wa maarifa huongeza uwezo;

Mithali 24:6

Maana kwa mashauri ya akili utafanya vita; Na kwa wingi wa washauri huja wokovu.

Mithali 24:7

Kwa mpumbavu hekima haipatikani; Hafumbui kinywa chake langoni.

Mithali 24:8

Mtu afikiriye kutenda maovu, Watu watamwita mtundu;

Mithali 24:9

Fikira za mpumbavu ni dhambi, Na mwenye mzaha huwachukiza watu.

Mithali 24:10

Ukizimia siku ya taabu, Nguvu zako ni chache.

Mithali 24:11

Uwaokoe wanaochukuliwa ili wauawe; Nao walio tayari kuchinjwa uwaopoe.

Mithali 24:12

Ukisema, Sisi hatukujua hayo; Je! Yeye aipimaye mioyo siye afahamuye? Naye ailindaye nafsi yako siye ajuaye? Je! Hatamlipa kila mtu sawasawa na kazi yake?

Mithali 24:13

Mwanangu, ule asali, kwa maana ni njema, Na sega la asali lililo tamu ulionjapo.

Mithali 24:14

Basi utaijua hekima kuwa tamu kwa nafsi yako; Ikiwa umekwisha kuiona; Ndipo itakapofuata thawabu; Wala tumaini lako halitabatilika.

Mithali 24:15

Ewe mtu mbaya, usiyavizie makao yake mwenye haki; Wala usipaharibu mahali pake pa kupumzika;

Mithali 24:16

Kwa maana mwenye haki huanguka mara saba akaondoka tena; Bali wasio haki hukwazwa na mabaya.

Mithali 24:17

Usifurahi, adui yako aangukapo; Wala moyo wako usishangilie ajikwaapo;

Mithali 24:18

Bwana asije akaliona hilo, likamkasirisha; Akageuzia mbali naye hasira yake.

Mithali 24:19

Usikasirike kwa sababu ya watenda mabaya; Wala usiwahusudu wabaya;

Mithali 24:20

Kwa maana mtu mbaya hapati thawabu; Taa ya mtu mbaya itazimika.

Mithali 24:21

Mwanangu, mche Bwana, na mfalme; Wala usishirikiane na wenye kigeugeu;

Mithali 24:22

Maana msiba wao utatokea kwa ghafula; Tena ni nani aujuaye uharibifu wa miaka yao.

Mithali 24:23

Haya nayo pia ni maneno ya wenye akili. Kupendelea watu katika hukumu si kwema.

Mithali 24:24

Amwambiaye mtu mwovu, Wewe una haki; Kabila za watu watamlaani, taifa watamchukia.

Mithali 24:25

Bali kwao wakemeao furaha itakuwako; Na baraka ya kufanikiwa itawajilia.

Mithali 24:26

Aibusu midomo atoaye jawabu la haki.

Mithali 24:27

Tengeneza kazi yako huko nje, Jifanyizie kazi yako tayari shambani, Ukiisha, jenga nyumba yako.

Mithali 24:28

Usimshuhudie jirani yako pasipo sababu, Wala usidanganye kwa midomo yako.

Mithali 24:29

Usiseme, Nitamtenda kama alivyonitenda mimi; Nitamlipa mtu huyo sawasawa na tendo lake.

Mithali 24:30

Nalipita karibu na shamba la mvivu, Na shamba la mizabibu la mtu asiye na akili.

Mithali 24:31

Kumbe! Lote pia limemea miiba; Uso wake ulifunikwa kwa viwawi; Na ukuta wake wa mawe umebomoka.

Mithali 24:32

Ndipo nilipoangalia na kufikiri sana; Naliona, nikapata mafundisho.

Mithali 24:33

Bado kulala kidogo, kusinzia kidogo, Bado kukunja mikono upate usingizi!

Mithali 24:34

Hivyo, umaskini wako huja kama mnyang'anyi, Na uhitaji wako kama mtu mwenye silaha.