Mithali Mlango 12 Proverbs

Mithali 12:1

Kila apendaye mafundisho hupenda maarifa; Bali yeye achukiaye kulaumiwa ni kama mnyama.

Mithali 12:2

Mtu mwema atapata upendeleo kwa Bwana; Bali mtu wa hila atahukumiwa naye.

Mithali 12:3

Mtu hatathibitika kwa njia ya uovu; Shina la mwenye haki halitaondolewa kamwe.

Mithali 12:4

Mwanamke mwema ni taji ya mumewe; Bali aaibishaye ni kama kuoza mifupani mwake.

Mithali 12:5

Mawazo ya mwenye haki ni adili; Bali mashauri ya mtu mwovu ni hadaa.

Mithali 12:6

Maneno ya waovu huotea damu; Bali kinywa cha wanyofu kitawaokoa.

Mithali 12:7

Waovu huangamia, hata hawako tena; Bali nyumba ya mwenye haki itasimama.

Mithali 12:8

Mtu atasifiwa kwa kadiri ya akili zake; Bali mwenye moyo wa ukaidi atadharauliwa.

Mithali 12:9

Afadhali mtu anayedharauliwa, ikiwa ana mtumwa, Kuliko ajisifuye, ikiwa anahitaji chakula.

Mithali 12:10

Mwenye haki huufikiri uhai wa mnyama wake; Bali huruma za mtu mwovu ni ukatili.

Mithali 12:11

Alimaye shamba lake atakuwa na chakula tele; Bali afuataye mambo ya upuzi hana ufahamu.

Mithali 12:12

Asiye haki hutamani nyavu za wabaya; Bali shina lao wenye haki huleta matunda.

Mithali 12:13

Katika kosa la midomo kuna mtego kwa mbaya; Bali mwenye haki atatoka katika taabu.

Mithali 12:14

Mtu atashiba mema kwa matunda ya kinywa chake; Na atarudishiwa matendo ya mikono yake.

Mithali 12:15

Njia ya mpumbavu imenyoka machoni pake mwenyewe; Bali yeye aliye na hekima husikiliza shauri.

Mithali 12:16

Ghadhabu ya mpumbavu hujulika mara; Bali mtu mwerevu husitiri aibu.

Mithali 12:17

Atamkaye maneno ya kweli hufunua haki; Bali shahidi wa uongo hutamka hila.

Mithali 12:18

Kuna anenaye bila kufikiri, kama kuchoma kwa upanga; Bali ulimi wa mwenye haki ni afya.

Mithali 12:19

Mdomo wa kweli utathibitishwa milele; Bali ulimi wa uongo ni wa kitambo tu.

Mithali 12:20

Hila imo mioyoni mwao wafikirio uovu; Bali wafanyao mashauri ya amani, kwao kuna furaha.

Mithali 12:21

Mwenye haki hatapatikana na msiba wo wote; Bali wasio haki watajazwa mabaya.

Mithali 12:22

Midomo ya uongo ni chukizo kwa Bwana; Bali watendao uaminifu ndio furaha yake.

Mithali 12:23

Mwanadamu mwenye busara husitiri maarifa; Bali moyo wa wapumbavu hutangaza upumbavu.

Mithali 12:24

Mkono wa mwenye bidii utatawala; Bali mvivu atalipishwa kodi.

Mithali 12:25

Uzito katika moyo wa mtu huuinamisha; Bali neno jema huufurahisha.

Mithali 12:26

Mwenye haki ni kiongozi cha mwenzake; Bali njia ya wasio haki huwakosesha.

Mithali 12:27

Mtu mvivu hapiki mawindo yake; Bali mwenye bidii anazo mali za thamani.

Mithali 12:28

Katika njia ya haki kuna uhai; Wala hakuna mauti katika mapito yake.