Mithali Mlango 26 Proverbs

Mithali 26:1

Kama theluji wakati wa joto, na mvua wakati wa mavuno; Kadhalika heshima haimpasi mpumbavu.

Mithali 26:2

Kama shomoro katika kutanga-tanga kwake, Na kama mbayuwayu katika kuruka kwake; Kadhalika laana isiyo na sababu haimpigi mtu.

Mithali 26:3

Mjeledi kwa farasi, lijamu kwa punda, Na fimbo kwa mgongo wa mpumbavu.

Mithali 26:4

Usimjibu mpumbavu sawasawa na upumbavu wake; Usije ukafanana naye.

Mithali 26:5

Umjibu mpumbavu sawasawa na upumbavu wake; Asije akawa mwenye hekima machoni pake.

Mithali 26:6

Apelekaye ujumbe kwa mkono wa mpumbavu Hujikata miguu, na kunywa hasara.

Mithali 26:7

Miguu yake achechemeaye huwa dhaifu; Kadhalika mithali katika kinywa cha mpumbavu.

Mithali 26:8

Kama mfuko wa vito katika chungu ya mawe; Kadhalika mtu amheshimuye mpumbavu.

Mithali 26:9

Kama mwiba uingiao katika mkono wa mlevi; Kadhalika mithali katika kinywa cha mpumbavu.

Mithali 26:10

Fundi stadi hufanyiza vitu vyote; Bali amwajiriye mpumbavu ni kama awaajiriye watu wapitao.

Mithali 26:11

Kama vile mbwa arudiavyo matapiko yake; Kadhalika mpumbavu afanya upumbavu tena.

Mithali 26:12

Je! Wamwona mtu mwenye hekima machoni pake mwenyewe? Afadhali kumtumaini mpumbavu kuliko yeye.

Mithali 26:13

Mtu mvivu husema, Simba yuko njiani, Simba yuko katika njia kuu.

Mithali 26:14

Kama vile mlango ugeukavyo katika bawaba zake; Kadhalika mtu mvivu katika kitanda chake.

Mithali 26:15

Mtu mvivu hutia mkono wake sahanini; Kwamchosha kuupeleka tena kinywani pake.

Mithali 26:16

Mtu mvivu ni mwenye hekima machoni pake, Kuliko watu saba wawezao kutoa sababu.

Mithali 26:17

Mtu apitaye na kujisumbua kwa ugomvi usio wake; Ni kama mtu ashikaye mbwa kwa masikio yake.

Mithali 26:18

Kama mtu mwenye wazimu atupaye mienge, Na mishale, na mauti;

Mithali 26:19

Ndivyo alivyo amdanganyaye mwenzake, Na kusema, Je! Sikufanya mzaha tu?

Mithali 26:20

Moto hufa kwa kukosa kuni; Na bila mchongezi fitina hukoma.

Mithali 26:21

Kama makaa juu ya makaa yanayowaka, Na kama kuni juu ya moto; Ndivyo mtu mgomvi achocheavyo uadui.

Mithali 26:22

Maneno ya mchongezi ni kama vitoweo. Nayo hushukia pande za ndani za tumbo.

Mithali 26:23

Midomo ijipendekezayo pamoja na moyo mbaya Ni kama kigae kilichofunikizwa taka za fedha.

Mithali 26:24

Achukiaye huficha chuki kwa midomo yake; Naye huweka akiba ya hila moyoni mwake.

Mithali 26:25

Anenapo maneno mazuri usimsadiki; Kwa maana ana machukizo saba moyoni mwake.

Mithali 26:26

Ingawa chuki hufunikizwa kwa hila; Uovu wake utadhihirika mbele ya kusanyiko.

Mithali 26:27

Achimbaye shimo atatumbukia mwenyewe; Naye abingirishaye jiwe litamrudia.

Mithali 26:28

Ulimi unenao uongo huwachukia wale uliowajeruhi; Na kinywa cha kujipendekeza hutenda uharibifu.