Mithali Mlango 2 Proverbs

Mithali 2:1

Mwanangu, kama ukiyakubali maneno yangu, Na kuyaweka akiba maagizo yangu;

Mithali 2:2

Hata ukatega sikio lako kusikia hekima, Ukauelekeza moyo wako upate kufahamu;

Mithali 2:3

Naam, ukiita busara, Na kupaza sauti yako upate ufahamu;

Mithali 2:4

Ukiutafuta kama fedha, Na kuutafutia kama hazina iliyositirika;

Mithali 2:5

Ndipo utakapofahamu kumcha Bwana, Na kupata kumjua Mungu.

Mithali 2:6

Kwa kuwa Bwana huwapa watu hekima; Kinywani mwake hutoka maarifa na ufahamu;

Mithali 2:7

Huwawekea wanyofu akiba ya hekima kamili; Yeye ni ngao kwao waendao kwa ukamilifu;

Mithali 2:8

Apate kuyalinda mapito ya hukumu, Na kuhifadhi njia ya watakatifu wake.

Mithali 2:9

Ndipo utakapofahamu haki na hukumu, Na adili, na kila njia njema.

Mithali 2:10

Maana hekima itaingia moyoni mwako, Na maarifa yatakupendeza nafsi yako;

Mithali 2:11

Busara itakulinda; Ufahamu utakuhifadhi.

Mithali 2:12

Ili kukuokoa na njia ya uovu, Na watu wanenao yaliyopotoka;

Mithali 2:13

Watu waziachao njia za unyofu, Ili kuziendea njia za giza;

Mithali 2:14

Wafurahio kutenda mabaya; Wapendezwao na upotoe wa waovu;

Mithali 2:15

Waliopotoka katika njia zao; Walio wakaidi katika mapito yao.

Mithali 2:16

Ili kuokoka na malaya, Naam, malaya mwenye kubembeleza kwa maneno yake;

Mithali 2:17

Amwachaye rafiki wa ujana wake, Na kulisahau agano la Mungu wake.

Mithali 2:18

Maana nyumba yake inaelekea mauti, Na mapito yake yanakwenda kwenye wafu.

Mithali 2:19

Katika hao wamwendeao harudi hata mmoja, Wala hawazifikilii njia za uzima.

Mithali 2:20

Ili upate kwenda katika njia ya watu wema, Na kuyashika mapito ya wenye haki.

Mithali 2:21

Maana wanyofu watakaa katika nchi, Na wakamilifu watadumu ndani yake.

Mithali 2:22

Bali waovu watatengwa na nchi, Nao wafanyao hila watang'olewa.