Mithali Mlango 22 Proverbs

Mithali 22:1

Heri kuchagua jina jema kuliko mali nyingi; Na neema kuliko fedha na dhahabu.

Mithali 22:2

Tajiri na maskini hukutana pamoja; Bwana ndiye aliyewaumba wote wawili.

Mithali 22:3

Mwenye busara huyaona mabaya na kujificha; Bali wajinga huendelea mbele wakaumia.

Mithali 22:4

Thawabu ya unyenyekevu ambao ni kumcha Bwana Ni utajiri, na heshima, nayo ni uzima.

Mithali 22:5

Miiba na mitego huwa katika njia ya mshupavu; Yeye aitunzaye nafsi yake atakuwa mbali nayo.

Mithali 22:6

Mlee mtoto katika njia impasayo, Naye hataiacha, hata atakapokuwa mzee.

Mithali 22:7

Tajiri humtawala maskini, Naye akopaye ni mtumwa wake akopeshaye.

Mithali 22:8

Yeye apandaye uovu atavuna msiba, Na fimbo ya ghadhabu yake itakoma.

Mithali 22:9

Mwenye jicho la ukarimu atabarikiwa; Maana huwapa maskini chakula chake.

Mithali 22:10

Mtupe nje mwenye dharau, na ugomvi utatoka; Naam, fitina na fedheha zitakoma.

Mithali 22:11

Apendaye usafi wa moyo, na neema ya midomo; Mfalme atakuwa rafiki yake.

Mithali 22:12

Macho ya Bwana humhifadhi mwenye maarifa; Bali huyapindua maneno ya mtu haini.

Mithali 22:13

Mtu mvivu husema, Simba yuko nje; Nitauawa katika njia kuu.

Mithali 22:14

Kinywa cha malaya ni shimo refu; Anayechukiwa na Bwana atatumbukia ndani yake.

Mithali 22:15

Ujinga umefungwa ndani ya moyo wa mtoto; Lakini fimbo ya adhabu itaufukuzia mbali.

Mithali 22:16

Yeye awaoneaye maskini ili kuongeza mapato, Naye ampaye tajiri, hupata hasara.

Mithali 22:17

Tega sikio lako uyasikie maneno ya wenye hekima, na kuuelekeza moyo wako kwa maarifa yangu;

Mithali 22:18

maana ni vizuri kuyahifadhi ndani yako, hali yakithibitika pamoja midomoni mwako.

Mithali 22:19

Ili matumaini yako uyaweke kwa Bwana, leo nimekujulisha wewe haya, naam, wewe.

Mithali 22:20

Je! Sikukuandikia mambo makuu juu ya mashauri na juu ya maarifa;

Mithali 22:21

ili kukujulisha hakika ya maneno ya kweli, uwarudishie wakutumao maneno ya kweli?

Mithali 22:22

Usimnyang'anye maskini, kwa kuwa ni maskini; Wala usimdhulumu mtu mnyonge langoni;

Mithali 22:23

Kwa sababu Bwana atawatetea; Naye atawateka uhai wao waliowateka.

Mithali 22:24

Usifanye urafiki na mtu mwenye hasira nyingi; Wala usiende na mtu wa ghadhabu nyingi;

Mithali 22:25

Usije ukajifunza njia zake; Na kujipatia nafsi yako mtego.

Mithali 22:26

Usiwe mmoja wao wawekao rehani; Au walio wadhamini kwa deni za watu;

Mithali 22:27

Kama huna kitu cha kulipa; Kwani ukaondolee kitanda chako chini yako?

Mithali 22:28

Usiiondoe alama ya mpaka wa zamani, Uliowekwa na baba zako.

Mithali 22:29

Je! Wamwona mtu mwenye bidii katika kazi zake? Huyo atasimama mbele ya wafalme; Hatasimama mbele ya watu wasio na cheo.