Mithali Mlango 7 Proverbs

Mithali 7:1

Mwanangu, yashike maneno yangu, Na kuziweka amri zangu akiba kwako.

Mithali 7:2

Uzishike amri zangu ukaishi, Na sheria yangu kama mboni ya jicho lako.

Mithali 7:3

Zifunge katika vidole vyako; Ziandike juu ya kibao cha moyo wako.

Mithali 7:4

Mwambie hekima, Wewe ndiwe umbu langu; Mwite ufahamu jamaa yako mwanamke.

Mithali 7:5

Wapate kukulinda na malaya, Na mgeni akubembelezaye kwa maneno yake.

Mithali 7:6

Maana katika dirisha la nyumba yangu Nalichungulia katika shubaka yake;

Mithali 7:7

Nikaona katikati ya wajinga, Nikamtambua miongoni mwa vijana, Kijana mmoja asiyekuwa na akili,

Mithali 7:8

Akipita njiani karibu na pembe yake, Akiishika njia iendayo nyumbani kwake,

Mithali 7:9

Wakati wa magharibi, wakati wa jioni, Usiku wa manane, gizani.

Mithali 7:10

Na tazama, mwanamke akamkuta, Ana mavazi ya kikahaba, mwerevu wa moyo;

Mithali 7:11

Ana kelele, na ukaidi; Miguu yake haikai nyumbani mwake.

Mithali 7:12

Mara yu katika njia kuu, mara viwanjani, Naye huotea kwenye pembe za kila njia.

Mithali 7:13

Basi akamshika, akambusu, Akamwambia kwa uso usio na haya,

Mithali 7:14

Kwangu ziko sadaka za amani; Leo hivi nimeziondoa nadhiri zangu;

Mithali 7:15

Ndiyo maana nikatoka nikulaki, Nikutafute uso wako kwa bidii, nami nimekuona.

Mithali 7:16

Nimetandika kitanda changu, magodoro mazuri, Kwa matandiko ya Kimisri yenye mistari.

Mithali 7:17

Nimetia kitanda changu manukato, Manemane na udi na mdalasini.

Mithali 7:18

Haya, na tushibe upendo hata asubuhi, Tujifurahishe nafsi zetu kwa mahaba.

Mithali 7:19

Maana mume wangu hayumo nyumbani, Amekwenda safari ya mbali;

Mithali 7:20

Amechukua mfuko wa fedha mkononi; Atarudi wakati wa mwezi mpevu.

Mithali 7:21

Kwa maneno yake mengi na ulaini akamshawishi, Kwa ubembelezi wa midomo yake akamshinda.

Mithali 7:22

Huyo akafuatana naye mara hiyo, Kama vile ng'ombe aendavyo machinjoni; Au mpumbavu kuadhibiwa katika pingu;

Mithali 7:23

Hata mshale umchome maini; Kama ndege aendaye haraka mtegoni; Wala hajui ya kuwa ni hasara ya nafsi yake.

Mithali 7:24

Basi, wanangu, nisikilizeni sasa, Mkayaangalie maneno ya kinywa changu.

Mithali 7:25

Moyo wako usizielekee njia zake, Wala usipotee katika mapito yake.

Mithali 7:26

Maana amewaangusha wengi waliojeruhi, Naam, jumla ya waliouawa naye ni jeshi kubwa.

Mithali 7:27

Nyumba yake ni njia ya kwenda kuzimu, Hushuka mpaka vyumba vya mauti.