Mithali Mlango 13 Proverbs

Mithali 13:1

Mwana mwenye hekima husikiliza mausia ya babaye; Bali mwenye dharau hasikilizi maonyo.

Mithali 13:2

Mtu atakula mema kwa matunda ya kinywa chake; Bali nafsi ya mtu haini itakula jeuri.

Mithali 13:3

Yeye alindaye kinywa chake huilinda nafsi yake; Bali afunuaye midomo yake atapata uharibifu.

Mithali 13:4

Nafsi ya mtu mvivu hutamani asipate kitu; Bali nafsi ya mwenye bidii itanenepeshwa.

Mithali 13:5

Mwenye haki huchukia kusema uongo; Bali mtu mbaya huwa karaha, hupatwa na aibu.

Mithali 13:6

Haki humlinda yeye aliye mnyofu katika njia yake; Bali ubaya humwangusha mwenye dhambi.

Mithali 13:7

Kuna mtu mwenye kujitajirisha, lakini hana kitu; Kuna ajifanyaye kuwa maskini, lakini ana mali nyingi.

Mithali 13:8

Dia ya nafsi ya mtu ni utajiri wake; Bali mtu maskini hasikii ogofyo lo lote.

Mithali 13:9

Nuru ya mwenye haki yang'aa sana; Bali taa ya mtu mbaya itazimika.

Mithali 13:10

Kiburi huleta mashindano tu; Bali hekima hukaa nao wanaoshauriana.

Mithali 13:11

Mali iliyopatikana kwa haraka itapunguka; Bali yeye achumaye kidogo kidogo atazidishiwa.

Mithali 13:12

Kilichotarajiwa kikikawia kuja, moyo huugua. Bali haja ya mtu ikipatikana, ni mti wa uzima.

Mithali 13:13

Kila alidharauye neno hujiletea uharibifu; Bali yeye aiogopaye amri atapewa thawabu.

Mithali 13:14

Sheria ya mwenye akili ni chemchemi ya uzima, Ili kuepukana na tanzi za mauti.

Mithali 13:15

Ufahamu mwema huleta upendeleo; Bali njia ya haini huparuza.

Mithali 13:16

Kila aliye na busara hutenda kazi kwa maarifa; Bali mpumbavu hueneza upumbavu.

Mithali 13:17

Mjumbe mbaya huanguka maovuni; Bali mjumbe mwaminifu ni afya.

Mithali 13:18

Umaskini na fedheha zitampata yeye akataaye kurudiwa; Bali yeye aangaliaye maonyo ataheshimiwa.

Mithali 13:19

Haja iliyopatikana ni tamu nafsini mwa mtu; Bali kujitenga na maovu ni chukizo kwa wapumbavu.

Mithali 13:20

Enenda pamoja na wenye hekima, nawe utakuwa na hekima; Bali rafiki wa wapumbavu ataumia.

Mithali 13:21

Uovu huwaandamia wenye dhambi; Bali mwenye haki atalipwa mema.

Mithali 13:22

Mtu mwema huwaachia wana wa wanawe urithi; Na mali ya mkosaji huwa akiba kwa mwenye haki.

Mithali 13:23

Chakula kingi chapatikana kwa ukulima wa maskini; Bali viko viharibiwavyo kwa sababu ya dhuluma.

Mithali 13:24

Yeye asiyetumia fimbo yake humchukia mwanawe; Bali yeye ampendaye humrudi mapema.

Mithali 13:25

Mwenye haki hula akaishibisha nafsi yake; Bali tumbo la mtu mbaya litaona njaa.