Mithali Mlango 27 Proverbs

Mithali 27:1

Usijisifu kwa ajili ya kesho; Kwa maana hujui yatakayozaliwa na siku moja.

Mithali 27:2

Mwingine na akusifu wala si kinywa chako mwenyewe; Mtu mgeni wala si midomo yako wewe.

Mithali 27:3

Jiwe ni zito, na mchanga hulemea; Lakini ghadhabu ya mpumbavu ni nzito kuliko hivi vyote viwili.

Mithali 27:4

Ghadhabu ni kali, na hasira ni gharika; Lakini ni nani awezaye kusimama mbele ya wivu.

Mithali 27:5

Lawama ya wazi ni heri, Kuliko upendo uliositirika.

Mithali 27:6

Jeraha utiwazo na rafiki ni amini; Bali kubusu kwa adui ni kwingi sana.

Mithali 27:7

Nafsi iliyoshiba hukinai sega la asali; Bali nafsi yenye njaa huona kila kitu kichungu kuwa kitamu.

Mithali 27:8

Kama ndege aendaye huko na huko mbali na kitundu chake; Ndivyo alivyo mtu aendaye huko na huko mbali na mahali pake.

Mithali 27:9

Marhamu na manukato huufurahisha moyo; Kadhalika utamu wa rafiki ya mtu utokao katika kusudi la moyo wake.

Mithali 27:10

Usimwache rafiki yako mwenyewe, wala rafiki ya baba yako, Wala usiende nyumbani mwa ndugu yako siku ya msiba wako. Afadhali jirani aliye karibu kuliko ndugu aliye mbali.

Mithali 27:11

Mwanangu, uwe na hekima na kunifurahisha moyo wangu; Ili nipate kumjibu anilaumuye.

Mithali 27:12

Mwenye busara huyaona mabaya na kujificha; Bali wajinga huendelea mbele wakaumia.

Mithali 27:13

Twaa nguo yake amdhaminiye mgeni; Mtoza rehani aliye mdhamini wa malaya.

Mithali 27:14

Mtu ambarikiye mwenzake kwa sauti kuu asubuhi na mapema; Itahesabiwa kuwa ni laana kwake.

Mithali 27:15

Kutona-tona daima siku ya mvua nyingi, Na mwanamke mgomvi ni sawasawa;

Mithali 27:16

Atakaye kumzuia huyo huuzuia upepo; Na mkono wake wa kuume hukuta mafuta.

Mithali 27:17

Chuma hunoa chuma; Ndivyo mtu aunoavyo uso wa rafiki yake.

Mithali 27:18

Yeye autunzaye mtini atakula matunda yake; Naye amhudumiaye bwana wake ataheshimiwa.

Mithali 27:19

Kama uso ufananavyo na uso katika maji; Kadhalika moyo wa mtu na mwenzake.

Mithali 27:20

Kuzimu na Uharibifu havishibi; Wala macho ya wanadamu hayashibi.

Mithali 27:21

Kalibu ni kwa fedha, na tanuru kwa dhahabu; Na mtu hujaribiwa kwa sifa zake.

Mithali 27:22

Hata ukimtwanga mpumbavu kwa mchi kinuni pamoja na ngano; Upumbavu wake hautamtoka.

Mithali 27:23

Fanya bidii kuijua hali ya makundi yako; Na kuwaangalia sana ng'ombe zako.

Mithali 27:24

Kwa maana mali haziwi za milele; Na taji je! Yadumu tangu kizazi hata kizazi?

Mithali 27:25

Manyasi huchukuliwa, na majani mabichi huonekana, Na maboga ya milimani hukusanyika.

Mithali 27:26

Wana-kondoo hufaa kwa mavazi yako; Na mbuzi ni thamani ya shamba

Mithali 27:27

Tena yatakuwapo maziwa ya mbuzi, Ya kukutosha kwa chakula chako, Na chakula cha watu wa nyumbani mwako, Na posho la vijakazi vyako.