Mithali Mlango 3 Proverbs

Mithali 3:1

Mwanangu, usiisahau sheria yangu, Bali moyo wako uzishike amri zangu.

Mithali 3:2

Maana zitakuongezea wingi wa siku. Na miaka ya uzima, na amani.

Mithali 3:3

Rehema na kweli zisifarakane nawe; Zifunge shingoni mwako; Ziandike juu ya kibao cha moyo wako.

Mithali 3:4

Ndivyo utakavyopata kibali na akili nzuri, Mbele za Mungu na mbele ya mwanadamu.

Mithali 3:5

Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe;

Mithali 3:6

Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako.

Mithali 3:7

Usiwe mwenye hekima machoni pako; Mche Bwana, ukajiepushe na uovu.

Mithali 3:8

Itakuwa afya mwilini pako, Na mafuta mifupani mwako.

Mithali 3:9

Mheshimu Bwana kwa mali yako, Na kwa malimbuko ya mazao yako yote.

Mithali 3:10

Ndipo ghala zako zitakapojazwa kwa wingi, Na mashinikizo yako yatafurika divai mpya.

Mithali 3:11

Mwanangu, usidharau kuadhibiwa na Bwana, Wala usione ni taabu kurudiwa naye.

Mithali 3:12

Kwa kuwa Bwana ampendaye humrudi, Kama vile baba mwanawe ampendezaye.

Mithali 3:13

Heri mtu yule aonaye hekima, Na mtu yule apataye ufahamu.

Mithali 3:14

Maana biashara yake ni bora kuliko biashara ya fedha, Na faida yake ni nyingi kuliko dhahabu safi.

Mithali 3:15

Yeye ana thamani kuliko marijani, Wala vyote uvitamanivyo havilingani naye.

Mithali 3:16

Ana wingi wa siku katika mkono wake wa kuume, Utajiri na heshima katika mkono wake wa kushoto.

Mithali 3:17

Njia zake ni njia za kupendeza sana, Na mapito yake yote ni amani.

Mithali 3:18

Yeye ni mti wa uzima kwao wamshikao sana; Ana heri kila mtu ashikamanaye naye.

Mithali 3:19

Kwa hekima Bwana aliiweka misingi ya nchi; Kwa akili zake akazifanya mbingu imara;

Mithali 3:20

Kwa maarifa yake vilindi viligawanyika; Na mawingu yadondoza umande.

Mithali 3:21

Mwanangu, yasiondoke haya machoni pako, Shika hekima kamili na busara.

Mithali 3:22

Basi yatakuwa uzima kwa nafsi yako, Na neema shingoni mwako.

Mithali 3:23

Ndipo utakapokwenda katika njia yako salama, Wala mguu wako hautakwaa.

Mithali 3:24

Ulalapo hutaona hofu; Naam, utalala na usingizi wako utakuwa mtamu.

Mithali 3:25

Usiogope hofu ya ghafula, Wala uharibifu wa waovu utakapofika.

Mithali 3:26

Kwa kuwa Bwana atakuwa tumaini lako, Naye atakulinda mguu wako usinaswe.

Mithali 3:27

Usiwanyime watu mema yaliyo haki yao, Ikiwa katika uwezo wa mkono wako kuyatenda.

Mithali 3:28

Usimwambie jirani yako, Nenda, urudi halafu, na kesho nitakupa; Nawe unacho kitu kile karibu nawe.

Mithali 3:29

Usiwaze mabaya juu ya jirani yako, Ambaye anakaa karibu nawe na kujiona salama.

Mithali 3:30

Usishindane na mtu bila sababu, Ikiwa hakukudhuru kwa lo lote.

Mithali 3:31

Usimhusudu mtu mwenye jeuri, Wala usiichague mojawapo ya njia zake.

Mithali 3:32

Maana mtu mkaidi ni chukizo kwa Bwana, Bali siri yake ni pamoja na wanyofu.

Mithali 3:33

Laana ya Bwana i katika nyumba ya waovu, Bali huibariki maskani ya mwenye haki.

Mithali 3:34

Hakika yake huwadharau wenye dharau, Bali huwapa wanyenyekevu neema.

Mithali 3:35

Wenye hekima wataurithi utukufu, Bali kukuzwa kwa wapumbavu ni fedheha.