Mithali Mlango 1 Proverbs

Mithali 1:1

Mithali za Sulemani, mwana wa Daudi, mfalme wa Israeli.

Mithali 1:2

Kujua hekima na adabu; kutambua maneno ya ufahamu;

Mithali 1:3

kufundishwa matendo ya busara, katika haki na hukumu na adili.

Mithali 1:4

Kuwapa wajinga werevu, na kijana maarifa na hadhari;

Mithali 1:5

mwenye hekima asikie na kuongezewa elimu, na mwenye ufahamu ayafikie mashauri yenye njia.

Mithali 1:6

Kufahamu mithali na kitendawili, na maneno ya wenye hekima na mafumbo yao.

Mithali 1:7

Kumcha Bwana ni chanzo cha maarifa, Bali wapumbavu hudharau hekima na adabu.

Mithali 1:8

Mwanangu, yasikilize mafundisho ya baba yako, Wala usiiache sheria ya mama yako,

Mithali 1:9

Kwa maana hayo yatakuwa kilemba cha neema kichwani pako, Na mikufu shingoni mwako.

Mithali 1:10

Mwanangu, wenye dhambi wakikushawishi, Wewe usikubali.

Mithali 1:11

Wakisema, Haya! Njoo pamoja nasi, Na tuvizie ili kumwaga damu; Tumwotee asiye na hatia, bila sababu;

Mithali 1:12

Tuwameze hai kama kuzimu, Na wazima, kama wao washukao shimoni.

Mithali 1:13

Tutapata mali yote ya thamani, Tutazijaza nyumba zetu mateka.

Mithali 1:14

Wewe utashirikiana nasi; Tutakuwa na vitu vyote shirika.

Mithali 1:15

Mwanangu, usiende njiani pamoja nao; Uzuie mguu wako usiende katika mapito yao.

Mithali 1:16

Maana miguu yao huenda mbio maovuni, Nao hufanya haraka ili kumwaga damu.

Mithali 1:17

Kwa kuwa mtego hutegwa bure, Mbele ya macho ya ndege ye yote.

Mithali 1:18

Na hao hujiotea damu yao wenyewe, Hujinyemelea nafsi zao wenyewe.

Mithali 1:19

Ndivyo zilivyo njia za kila mwenye tamaa ya mali; Huuondoa uhai wao walio nayo.

Mithali 1:20

Hekima hupaza sauti yake katika njia kuu, Hutoa sauti yake katika viwanja;

Mithali 1:21

Hulia penye mikutano mikubwa ya watu, Mahali pa kuyaingilia malango, Ndani ya mji hutamka maneno yake.

Mithali 1:22

Enyi wajinga, hata lini mtapenda ujinga? Na wenye dharau kupenda dharau yao, Na wapumbavu kuchukia maarifa?

Mithali 1:23

Geukeni kwa ajili ya maonyo yangu; Tazama, nitawamwagia roho yangu, Na kuwajulisheni maneno yangu.

Mithali 1:24

Kwa kuwa nimeita, nanyi mkakataa; Nimeunyosha mkono wangu, asiangalie mtu;

Mithali 1:25

Bali mmebatilisha shauri langu, Wala hamkutaka maonyo yangu;

Mithali 1:26

Mimi nami nitacheka siku ya msiba wenu, Nitadhihaki hofu yenu ifikapo;

Mithali 1:27

Hofu yenu ifikapo kama tufani, Na msiba wenu ufikapo kama kisulisuli, Dhiki na taabu zitakapowafikia.

Mithali 1:28

Ndipo watakaponiita, lakini sitaitika; Watanitafuta kwa bidii, wasinione.

Mithali 1:29

Kwa kuwa walichukia maarifa, Wala hawakuchagua kumcha Bwana.

Mithali 1:30

Hawakukubali mashauri yangu, Wakayadharau maonyo yangu yote.

Mithali 1:31

Kwa hiyo watakula matunda ya njia yao, Watashiba mashauri yao wenyewe.

Mithali 1:32

Maana kurudi nyuma kwao wajinga kutawaua, Na kufanikiwa kwao wapumbavu kutawaangamiza.

Mithali 1:33

Bali kila anisikilizaye atakaa salama, Naye atatulia bila kuogopa mabaya.