Mithali Mlango 15 Proverbs

Mithali 15:1

Jawabu la upole hugeuza hasira; Bali neno liumizalo huchochea ghadhabu.

Mithali 15:2

Ulimi wa mwenye hekima hutamka maarifa vizuri; Bali vinywa vya wapumbavu humwaga upumbavu.

Mithali 15:3

Macho ya Bwana yako kila mahali; Yakimchunguza mbaya na mwema.

Mithali 15:4

Ulimi safi ni mti wa uzima; Bali ukorofi wa ulimi huvunja moyo.

Mithali 15:5

Mpumbavu hudharau kurudiwa na babaye; Bali yeye aangaliaye maonyo hupata busara.

Mithali 15:6

Katika nyumba ya mwenye haki mna akiba nyingi; Bali mapato ya mtu mbaya huwa taabu tu.

Mithali 15:7

Midomo ya mwenye haki hueneza maarifa; Bali moyo wa mpumbavu haufanyi hivyo.

Mithali 15:8

Sadaka ya mtu mbaya ni chukizo kwa Bwana; Bali maombi ya mtu mnyofu ni furaha yake.

Mithali 15:9

Njia ya mtu mbaya ni chukizo kwa Bwana; Bali humpenda mtu afuatiaye wema.

Mithali 15:10

Adhabu kali ina yeye aiachaye njia; Naye achukiaye kukemewa atakufa.

Mithali 15:11

Kuzimu na Uharibifu vi wazi mbele za Bwana; Si zaidi basi, mioyo ya wanadamu?

Mithali 15:12

Mwenye mzaha hapendi kukaripiwa; Wala yeye hawaendei wenye hekima.

Mithali 15:13

Moyo wa furaha huchangamsha uso; Bali kwa huzuni ya moyo roho hupondeka.

Mithali 15:14

Moyo wa mwenye ufahamu hutafuta maarifa; Bali kinywa cha wapumbavu hula upumbavu.

Mithali 15:15

Siku zote za mtu ateswaye ni mbaya; Bali ukunjufu wa moyo ni karamu ya daima.

Mithali 15:16

Kuwa na mali chache pamoja na kumcha Bwana; Ni bora kuliko mali nyingi pamoja na taabu.

Mithali 15:17

Chakula cha mboga penye mapendano; Ni bora kuliko ng'ombe aliyenona pamoja na kuchukiana.

Mithali 15:18

Mtu wa hasira huchochea ugomvi; Bali asiye mwepesi wa hasira hutuliza mashindano.

Mithali 15:19

Njia ya mtu mvivu ni kama boma la miiba; Bali mapito yao wenye unyofu hufanyika njia kuu.

Mithali 15:20

Mwana mwenye hekima humfurahisha babaye; Bali mpumbavu humdharau mamaye.

Mithali 15:21

Upumbavu ni furaha kwake aliyepungukiwa na akili; Bali mwenye ufahamu huunyosha mwenendo wake.

Mithali 15:22

Pasipo mashauri makusudi hubatilika; Bali kwa wingi wa washauri huthibithika.

Mithali 15:23

Mtu hulifurahia jibu la kinywa chake; Na neno linenwalo wakati wa kufaa ni jema kama nini!

Mithali 15:24

Kwa mtu mwenye akili njia ya uhai huenda juu; Ili atoke katika kuzimu chini.

Mithali 15:25

Bwana ataing'oa nyumba ya mwenye kiburi; Bali atauthibitisha mpaka wa mjane.

Mithali 15:26

Mashauri mabaya ni chukizo kwa Bwana; Bali maneno yapendezayo ni safi.

Mithali 15:27

Atamaniye faida huifadhaisha nyumba yake mwenyewe; Bali achukiaye zawadi ataishi.

Mithali 15:28

Moyo wa mwenye haki hufikiri jinsi atakavyojibu; Bali kinywa cha wasio haki humwaga mabaya.

Mithali 15:29

Bwana yu mbali na wasio haki; Bali huisikia sala ya mwenye haki.

Mithali 15:30

Mng'ao wa macho huufurahisha moyo; Habari njema huinenepesha mifupa.

Mithali 15:31

Sikio lisikilizalo lawama yenye uhai Litakaa kati yao wenye hekima.

Mithali 15:32

Akataaye maonyo huidharau nafsi yake mwenyewe; Bali yeye asikilizaye lawama hujipatia ufahamu.

Mithali 15:33

Kumcha Bwana ni maonyo ya hekima; Na kabla ya heshima hutangulia unyenyekevu.