1 Mambo ya Nyakati Mlango 11 1st Chronicles

1 Mambo ya Nyakati 11:1

Ndipo Israeli wote wakamkusanyikia Daudi huko Hebroni, wakisema, Tazama, sisi tu mfupa wako na nyama yako.

1 Mambo ya Nyakati 11:2

Katika zamani za kale, hata hapo Sauli alipokuwa mfalme, wewe ndiwe uliyewatoa na kuwaingiza Israeli. Naye Bwana, Mungu wako, akakuambia, Ndiwe, utakayewalisha watu wangu Israeli, ndiwe utakayekuwa mkuu juu ya watu wangu Israeli.

1 Mambo ya Nyakati 11:3

Basi wazee wote wa Israeli wakamjia mfalme huko Hebroni; naye Daudi akafanya agano nao huko Hebroni mbele za Bwana; nao wakamtia Daudi mafuta, awe mfalme wa Israeli, sawasawa na neno la Bwana kwa mkono wa Samweli.

1 Mambo ya Nyakati 11:4

Kisha Daudi na Israeli wote wakaenda Yerusalemu, (ndio Yebusi;) nao Wayebusi, wenyeji wa nchi, walikuwamo.

1 Mambo ya Nyakati 11:5

Na hao wenyeji wa Yebusi wakamwambia Daudi, Hutaingia humu. Walakini Daudi akaitwaa ngome ya Sayuni; huu ndio mji wa Daudi.

1 Mambo ya Nyakati 11:6

Naye Daudi akasema, Mtu ye yote atakayekuwa wa kwanza wa kuwapiga Wayebusi, yeye atakuwa mkuu na jemadari. Naye wa kwanza aliyepanda ni Yoabu mwana wa Seruya, naye akawa mkuu.

1 Mambo ya Nyakati 11:7

Basi Daudi akakaa ngomeni; kwa hiyo huuita mji wa Daudi.

1 Mambo ya Nyakati 11:8

Akaujenga huo mji pande zote, toka Milo na kuuzunguka; naye Yoabu akautengeneza mji uliosalia.

1 Mambo ya Nyakati 11:9

Naye Daudi akaendelea, akazidi kuwa mkuu; kwa maana Bwana wa majeshi alikuwa pamoja naye.

1 Mambo ya Nyakati 11:10

Basi hawa ndio wakuu wa mashujaa aliokuwa nao Daudi, waliojitia nguvu pamoja naye katika ufalme wake, pamoja na Israeli wote, ili kumfanya awe mfalme, sawasawa na neno la Bwana alilonena juu ya Israeli.

1 Mambo ya Nyakati 11:11

Na hii ndiyo hesabu ya hao mashujaa aliokuwa nao Daudi; Yashobeamu, Mhakmoni, mkuu wa maakida; huyo aliuinua mkuki wake juu ya watu mia tatu, akawaua pamoja.

1 Mambo ya Nyakati 11:12

Na baada yake kulikuwa na Eleazari, mwana wa Dodai, Mwahohi, mmojawapo wa wale mashujaa watatu.

1 Mambo ya Nyakati 11:13

Huyo alikuwa pamoja na Daudi huko Pasdamimu; ndiko Wafilisti walikokusanyika vitani, palipokuwa na konde limejaa shayiri ;na hao watu wakakimbia mbele ya wafilisti.

1 Mambo ya Nyakati 11:14

Ndipo hao wakasimama katikati ya konde lile, wakalipigania, wakawaua Wafilisti; naye Bwana akafanya wokovu mkuu.

1 Mambo ya Nyakati 11:15

Tena, watatu miongoni mwa wale thelathini waliokuwa wakuu wakashuka mwambani, wakamwendea Daudi, hata pango la Adulamu; na jeshi la Wafilisti walikuwa wamefanya kambi bondeni mwa Warefai.

1 Mambo ya Nyakati 11:16

Na Daudi wakati ule alikuwako ngomeni, na walinzi wa Wafilisti wakati ule walikuwa huko Bethlehemu.

1 Mambo ya Nyakati 11:17

Naye Daudi akatamani, akasema, Laiti mtu angeninywesha maji ya kisima cha Bethlehemu, kilicho karibu na lango!

1 Mambo ya Nyakati 11:18

Basi hao watatu wakapenya jeshi la Wafilisti, wakateka maji kutoka kile kisima cha Bethlehemu, kilicho karibu na lango, wakayachukua, wakamletea Daudi; walakini Daudi hakukubali kuyanywa, akayamimina mbele za Bwana;

1 Mambo ya Nyakati 11:19

akasema, Mungu wangu apishe mbali, nisifanye hivi; je! Ninywe damu ya watu hao waliohatirisha nafsi zao? Maana kwa hatari ya nafsi zao wameyaleta. Kwa hiyo hakukubali kuyanywa. Hayo ndiyo waliyoyafanya wale mashujaa watatu.

1 Mambo ya Nyakati 11:20

Tena Abishai, nduguye Yoabu, alikuwa mkuu wa wale watatu; kwa kuwa aliuinua mkuki wake juu ya watu mia tatu, akawaua; akawa na jina kati ya wale watatu.

1 Mambo ya Nyakati 11:21

Katika wale watatu yeye alikuwa mwenye heshima kuliko hao wawili, akawa akida wao; ila hakudiriki kuwamo katika wale watatu.

1 Mambo ya Nyakati 11:22

Tena, Benaya, mwana wa Yehoyada, mtu hodari, wa Kabseeli, aliyekuwa amefanya mambo makuu, ndiye aliyewaua simba wakali wawili wa Moabu; pia akashuka ,akamwua simba katikati ya shimo wakati wa theruji.

1 Mambo ya Nyakati 11:23

Huyo akamwua Mmisri, mtu mrefu sana, aliyekuwa wa dhiraa tano urefu wake; na yule Mmisri alikuwa na mkuki kama mti wa mfumaji mkononi; lakini yeye akamshukia na gongo, akamnyakulia Mmisri mkuki mkononi, akamwua kwa mkuki wake mwenyewe.

1 Mambo ya Nyakati 11:24

Mambo hayo ndiyo aliyoyafanya Benaya, mwana wa Yehoyada, akawa na jina kati ya wale mashujaa watatu.

1 Mambo ya Nyakati 11:25

Tazama, alikuwa mwenye heshima kuliko wale thelathini, ila hakudiriki kuwamo katika wale watatu; naye Daudi akamweka juu ya walinzi wake.

1 Mambo ya Nyakati 11:26

Tena hawa ndio mashujaa wa majeshi ya askari; Asaheli nduguye Yoabu, Elhanani mwana wa Dodo wa Bethlehemu;

1 Mambo ya Nyakati 11:27

Shama Mharodi, Helesi Mpeloni;

1 Mambo ya Nyakati 11:28

Ira mwana wa Ikeshi Mtekoi, Abiezeri Mwanathothi;

1 Mambo ya Nyakati 11:29

Sibekai Mhushathi, Salmoni Mwahohi;

1 Mambo ya Nyakati 11:30

Maharai Mnetofathi, Heledi mwana wa Baana Mnetofathi;

1 Mambo ya Nyakati 11:31

Itai mwana wa Ribai wa Gibea wa wana wa Benyamini, Benaya Mpirathoni;

1 Mambo ya Nyakati 11:32

Hurai wa vijito vya Gaashi, Abieli Mwaibathi;

1 Mambo ya Nyakati 11:33

Azmawethi Mbaharumi, Eliaba Mshaalboni;

1 Mambo ya Nyakati 11:34

wana wa Yasheni Mgiloni, Yonathani mwana wa Shama Mharari;

1 Mambo ya Nyakati 11:35

Ahiamu mwana wa Sharari Mharari, Elifeleti mwana wa Ahasbai; Heferi

1 Mambo ya Nyakati 11:36

Mmaakathi, Ahia Mpeloni;

1 Mambo ya Nyakati 11:37

Hezro Mkarmeli, Paarai mwana wa Ezbai Mwarki;

1 Mambo ya Nyakati 11:38

Yoeli nduguye Nathani, Mibhari mwana wa Hagri;

1 Mambo ya Nyakati 11:39

Seleki Mwamoni, Naharai Mbeorothi, mchukua silaha wa Yoabu, mwana wa Seruya;

1 Mambo ya Nyakati 11:40

Ira Mwithri, Garebu Mwithri;

1 Mambo ya Nyakati 11:41

Uria Mhiti, Zabadi mwana wa Alai;

1 Mambo ya Nyakati 11:42

Adina mwana wa Shiza Mreubeni, mkuu wa Wareubeni, na thelathini pamoja naye;

1 Mambo ya Nyakati 11:43

Hanani mwana wa Maaka, na Yoshafati Mmithni;

1 Mambo ya Nyakati 11:44

Uzia Mwashterathi, Shama na Yeieli wana wa Hothamu Mwaroeri;

1 Mambo ya Nyakati 11:45

Yediaeli mwana wa Shimri, na Yoha nduguye, Muzi;

1 Mambo ya Nyakati 11:46

Elieli Mmahawi, na Yeribai, na Yoshavia, wana wa Elnaamu, na Ithma Mmoabi;

1 Mambo ya Nyakati 11:47

Elieli, na Obedi, na Yaasieli Mmesobai.