1 Mambo ya Nyakati Mlango 14 1st Chronicles

1 Mambo ya Nyakati 14:1

Naye Hiramu, mfalme wa Tiro, akatuma wajumbe kwa Daudi, akampelekea na mierezi, na waashi, na maseremala, ili wamjengee nyumba.

1 Mambo ya Nyakati 14:2

Daudi akajua ya kwamba Bwana amemweka imara ili amiliki juu ya Israeli, kwa kuwa milki yake imeinuka kwa ajili ya watu wake Israeli.

1 Mambo ya Nyakati 14:3

Tena Daudi akazidi kuoa wake huko Yerusalemu; akazidi Daudi kuzaa wana na binti.

1 Mambo ya Nyakati 14:4

Na haya ndiyo majina ya watoto aliozaliwa huko Yerusalemu; Shamua, na Shobabu, na Nathani, na Sulemani;

1 Mambo ya Nyakati 14:5

na Ibhari, na Elishua, na Elpeleti;

1 Mambo ya Nyakati 14:6

na Noga, na Nefegi, na Yafia;

1 Mambo ya Nyakati 14:7

na Elishama, na Eliada, na Elifeleti.

1 Mambo ya Nyakati 14:8

Na waliposikia hao Wafilisti ya kwamba Daudi ametiwa mafuta ili awe mfalme juu ya Israeli wote, Wafilisti wote wakapanda kumtafuta Daudi; naye Daudi akasikia, akatoka nje kupigana nao.

1 Mambo ya Nyakati 14:9

Basi hao Wafilisti walikuwa wamekuja na kuteka nyara katika bonde la Warefai.

1 Mambo ya Nyakati 14:10

Daudi akamwuliza Mungu, kusema, Je! Nipande juu ya Wafilisti! Utawatia mikononi mwangu? Naye Bwana akamwambia, Panda; kwa kuwa nitawatia mikononi mwako.

1 Mambo ya Nyakati 14:11

Basi wakapanda mpaka Baal-perasimu, Daudi naye akawapiga huko; Daudi akasema, Bwana amewafurikia adui zangu kwa mkono wangu, kama mafuriko ya maji. Basi wakapaita mahali pale jina lake Baal-perasimu.

1 Mambo ya Nyakati 14:12

Nao wakaiacha miungu yao huko; naye Daudi akaamuru, ikateketezwa kwa moto.

1 Mambo ya Nyakati 14:13

Lakini hao Wafilisti wakateka nyara tena mara ya pili bondeni.

1 Mambo ya Nyakati 14:14

Na Daudi akamwuliza Mungu tena; naye Mungu akamwambia, Hutapanda kuwafuata; uwageukie mbali, ukawajie huko kuielekea miforsadi.

1 Mambo ya Nyakati 14:15

Kisha itakuwa utakapoisikia sauti ya kwenda katika vilele vya miforsadi, ndipo utakapokwenda nje vitani; kwa maana ndipo Mungu ametoka mbele yako, awapige jeshi la Wafilisti.

1 Mambo ya Nyakati 14:16

Daudi akafanya kama vile Mungu alivyomwamuru; wakawapiga jeshi la Wafilisti toka Geba mpaka Gezeri.

1 Mambo ya Nyakati 14:17

Sifa za Daudi zikafika nchi zote; naye Bwana akawaletea mataifa yote hofu yake.