1 Mambo ya Nyakati Mlango 19 1st Chronicles

1 Mambo ya Nyakati 19:1

Ikawa baada ya hayo, Nahashi, mfalme wa wana wa Amoni, akafa, akamiliki mwanawe mahali pake.

1 Mambo ya Nyakati 19:2

Naye Daudi akasema, Nitamtendea wema Hanuni, mwana wa Nahashi, kwa kuwa babaye alinitendea mimi wema. Basi Daudi akapeleka wajumbe ili kumtuliza kwa habari za babaye. Wakaja watumishi wa Daudi katika nchi ya wana wa Amoni kwa Hanuni, ili wamtulize.

1 Mambo ya Nyakati 19:3

Lakini wakuu wa wana wa Amoni wakamwambia Hanuni, Je! Waona Daudi amheshimu babayo kwa kukupelekea wafariji? Je! Hawakukujia watumishi wake ili kuiangalia nchi, na kuiangamiza, na kuipeleleza?

1 Mambo ya Nyakati 19:4

Basi Hanuni akawatwaa watumishi wa Daudi, akawanyoa, akawakatia nguo zao katikati, hata matakoni, akawatoa waende zao.

1 Mambo ya Nyakati 19:5

Wakaenda watu wakamwambia Daudi jinsi walivyotendewa wale watu. Naye akatuma watu kuwalaki; kwa sababu watu hao walikuwa wametahayarika sana. Mfalme akasema, Ngojeni Yeriko, hata mtakapoota ndevu zenu, ndipo mrudi.

1 Mambo ya Nyakati 19:6

Na wana wa Amoni walipoona ya kuwa wamekuwa machukizo kwa Daudi, Hanuni na wana wa Amoni wakapeleka talanta elfu za fedha ili kujiajiria magari na wapanda farasi kutoka Mesopotamia, na kutoka Atam-maaka, na kutoka Soba.

1 Mambo ya Nyakati 19:7

Basi wakajiajiria magari thelathini na mbili elfu, na mfalme wa Maaka na watu wake; nao walikuja wakatua mbele ya Medeba. Na wana wa Amoni wakakusanyika kutoka miji yao, wakaja vitani.

1 Mambo ya Nyakati 19:8

Basi Daudi aliposikia habari akamtuma Yoabu, na jeshi lote la mashujaa.

1 Mambo ya Nyakati 19:9

Wakatoka wana wa Amoni, wakapanga vita langoni pa mji; na hao wafalme waliokuja walikuwa peke yao uwandani.

1 Mambo ya Nyakati 19:10

Basi Yoabu alipoona ya kwamba uso wa vita umekuwa juu yake mbele na nyuma, akachagua baadhi ya wateule wote wa Israeli, akawapanga juu ya Washami.

1 Mambo ya Nyakati 19:11

Na hao watu waliosalia akawatia mikononi mwa Abishai, nduguye, nao wakajipanga juu ya wana wa Amoni.

1 Mambo ya Nyakati 19:12

Akasema, Wakiwa Washami ni hodari mno kwangu, ndipo wewe utanisaidia; lakini wana wa Amoni wakiwa ni hodari mno kwako, ndipo mimi nitakusaidia wewe.

1 Mambo ya Nyakati 19:13

Uwe hodari, tukajitie moyo mkuu kwa ajili ya watu wetu, na kwa ajili ya miji ya Mungu wetu; naye Bwana afanye yaliyo mema machoni pake.

1 Mambo ya Nyakati 19:14

Basi Yoabu, na watu waliokuwa pamoja naye, wakakaribia kupigana na Washami; nao wakakimbia mbele yake.

1 Mambo ya Nyakati 19:15

Na wana wa Amoni walipoona ya kwamba Washami wamekimbia, wakakimbia nao mbele ya Abishai, nduguye, wakaingia mjini. Ndipo Yoabu akaja Yerusalemu.

1 Mambo ya Nyakati 19:16

Na Washami walipojiona kuwa wameshindwa mbele ya Israeli, wakapeleka wajumbe, wakawavuta Washami walioko ng'ambo ya Mto, na Shobaki, jemadari wa jeshi la Hadadezeri, akawaongoza.

1 Mambo ya Nyakati 19:17

Alipoambiwa Daudi; akakusanya Israeli wote, akavuka Yordani, akawajia, akapanga vita juu yao. Basi Daudi alipopanga vita juu ya Washami, wakapigana naye.

1 Mambo ya Nyakati 19:18

Washami wakakimbia mbele ya Israeli; naye Daudi akawaua katika Washami watu wa magari saba elfu, na askari waendao kwa miguu arobaini elfu, akamwua na Shobaki, jemadari wa jeshi.

1 Mambo ya Nyakati 19:19

Na watumwa wa Hadadezeri walipojiona kuwa wameshindwa mbele ya Israeli, walifanya amani na Daudi, wakamtumikia; wala Washami hawakukubali kuwasaidia wana wa Amoni tena.