1 Mambo ya Nyakati Mlango 12 1st Chronicles

1 Mambo ya Nyakati 12:1

Basi hawa ndio wale waliomjia Daudi huko Siklagi, alipokuwa akijificha kwa ajili ya Sauli, mwana wa Kishi; nao walikuwamo miongoni mwa wale mashujaa, waliomsaidia vitani.

1 Mambo ya Nyakati 12:2

Walikuwa wenye kupinda upinde, nao walikuwa hodari wa kutumia mkono wa kuume na wa kushoto, kwa kutupa mawe ya teo, na kwa kupiga mishale ya upinde; walikuwa wa nduguze Sauli, wa Benyamini.

1 Mambo ya Nyakati 12:3

Mkubwa wao alikuwa Ahiezeri, kisha Yoashi, wana wa Shemaa Mgibeathi; na Yezieli, na Peleti, wana wa Azmawethi; na Beraka, na Yehu Mwanathothi;

1 Mambo ya Nyakati 12:4

na Ishmaya Mgibeoni, shujaa wa wale thelathini, naye alikuwa juu ya wale thelathini; na Yeremia, na Yahazieli, na Yohana, na Yozabadi Mgederathi;

1 Mambo ya Nyakati 12:5

Eluzai, na Yerimothi, na Bealia, na Shemaria, na Shefatia Mharufi;

1 Mambo ya Nyakati 12:6

Elkana, na Ishia, na Azaleli, na Yoezeri, na Yashobeamu, Wakora;

1 Mambo ya Nyakati 12:7

na Yoela, na Zebadia, wana wa Yerohamu, wa Gedori.

1 Mambo ya Nyakati 12:8

Na wa Wagadi wakajitenga kumfuata Daudi ngomeni huko nyikani, waume mashujaa, watu waliozoea vita, walioweza kutumia ngao na mkuki; ambao nyuso zao zilikuwa kama nyuso za simba, nao walikuwa wepesi kama kulungu juu ya milima;

1 Mambo ya Nyakati 12:9

Ezeri mkubwa wao, Obadia wa pili, Eliabu wa tatu;

1 Mambo ya Nyakati 12:10

Mishmana wa nne, Yeremia wa tano;

1 Mambo ya Nyakati 12:11

Atai wa sita, Elieli wa saba;

1 Mambo ya Nyakati 12:12

Yohana wa nane, Elzabadi wa kenda;

1 Mambo ya Nyakati 12:13

Yeremia wa kumi, Makbanai wa kumi na moja.

1 Mambo ya Nyakati 12:14

Hao wa wana wa Gadi walikuwa maakida wa jeshi, yeye aliyekuwa mdogo amelingana na mia, na yeye aliyekuwa mkuu, na elfu.

1 Mambo ya Nyakati 12:15

Hao ndio wale waliovuka Yordani katika mwezi wa kwanza, ulipofurika kingo zake zote; nao wakawakimbiza wote wa bondeni kuelekea mashariki na magharibi pia.

1 Mambo ya Nyakati 12:16

Tena wakafika ngomeni kwa Daudi baadhi ya wana wa Benyamini na Yuda.

1 Mambo ya Nyakati 12:17

Naye Daudi akatoka ili kuwalaki, akajibu, akawaambia, Kama mmenijia kwa amani ili kunisaidia, basi moyo wangu utaambatana nanyi; lakini kama mmekuja ili kunisaliti kwa adui zangu, kwa kuwa hamna udhalimu mikononi mwangu, Mungu wa baba zetu na alitazame neno hili, na kulikemea.

1 Mambo ya Nyakati 12:18

Ndipo roho ikamjilia Abishai, mkuu wa wale thelathini, naye akasema, Sisi tu watu wako, Ee Daudi; Na wa upande wako, Ee mwana wa Yese; Amani, naam, amani iwe kwako, Na amani iwe kwao wakusaidiao; Maana akusaidiye ndiye Mungu wako. Ndipo Daudi akawakaribisha, akawaweka wawe maakida wa kile kikosi.

1 Mambo ya Nyakati 12:19

Wa Manase pia wengine walimwangukia Daudi, alipokwenda pamoja na Wafilisti juu ya Sauli vitani, lakini hawakuwasaidia; kwani wale mabwana wa Wafilisti wakafanya shauri, wakamfukuza, wakisema, kwa hatari ya vichwa vyetu atamwangukia bwana wake Sauli.

1 Mambo ya Nyakati 12:20

Naye alipokuwa akienda Siklagi, wakamwangukia hawa wa Manase, Adna, na Yozabadi, na Yediaeli, na Mikaeli, na Yozabadi, na Elihu, na Silethai, maakida wa maelfu waliokuwa wa Manase.

1 Mambo ya Nyakati 12:21

Wakamsaidia Daudi juu ya kile kikosi kilichomshambulia; kwani walikuwa waume mashujaa wote, nao wakawa maakida jeshini.

1 Mambo ya Nyakati 12:22

Maana siku kwa siku humjia Daudi watu wa kumsaidia, hata wakapata kuwa jeshi kubwa, kama jeshi la Mungu.

1 Mambo ya Nyakati 12:23

Na hizi ni hesabu za vichwa vya watu wenye silaha za vita, waliokuja Hebroni kwa Daudi, ili kumgeuzia ufalme wa Sauli, sawasawa na neno la Bwana.

1 Mambo ya Nyakati 12:24

Wana wa Yuda, waliochukua ngao na mkuki, walikuwa elfu sita na mia nane, wenye silaha za vita.

1 Mambo ya Nyakati 12:25

Wa wana wa Simeoni, waume mashujaa wa vita, elfu saba na mia moja.

1 Mambo ya Nyakati 12:26

Wa wana wa Lawi, elfu nne na mia sita.

1 Mambo ya Nyakati 12:27

Na Yehoyada alikuwa kichwa cha mbari ya Haruni, na pamoja naye walikuwa elfu tatu na mia saba;

1 Mambo ya Nyakati 12:28

tena Sadoki, kijana shujaa, na wa nyumba ya babaye, maakida ishirini na wawili.

1 Mambo ya Nyakati 12:29

Na wa wana wa Benyamini nduguze Sauli, elfu tatu; kwani hata sasa walio wengi wao walikuwa wameuhifadhi uaminifu wao kwa nyumba ya Sauli.

1 Mambo ya Nyakati 12:30

Na wa wana wa Efraimu, ishirini elfu na mia nane, waume mashujaa, watu wenye sifa katika mbari za baba zao.

1 Mambo ya Nyakati 12:31

Na wa nusu kabila ya Manase, kumi na nane elfu, waliotajwa majina yao, ili waje kumtawaza Daudi awe mfalme.

1 Mambo ya Nyakati 12:32

Na wa wana wa Isakari, watu wenye akili za kujua nyakati, kuyajua yawapasayo Israeli wayatende; vichwa vyao walikuwa watu mia mbili na ndugu zao wote walikuwa chini ya amri yao.

1 Mambo ya Nyakati 12:33

Wa Zabuloni, watu wawezao kwenda pamoja na jeshi, hodari wa kupanga vita, wenye zana za vita za kila namna, hamsini elfu; askari wastadi wasiokuwa wenye moyo wa kusita-sita.

1 Mambo ya Nyakati 12:34

Na wa Naftali, maakida elfu, na pamoja nao watu wenye ngao na mkuki thelathini na saba elfu.

1 Mambo ya Nyakati 12:35

Na wa Wadani, watu hodari wa kupanga vita, ishirini na nane elfu na mia sita.

1 Mambo ya Nyakati 12:36

Na wa Asheri, watu wawezao kwenda pamoja na jeshi, hodari wa kupanga vita, arobaini elfu.

1 Mambo ya Nyakati 12:37

Tena, ng'ambo ya pili ya Yordani, wa Wareubeni, na wa Wagadi, na wa nusu kabila ya Manase, wenye zana za vita za kupigania za kila namna, mia na ishirini elfu.

1 Mambo ya Nyakati 12:38

Hao wote, watu wa vita, askari wastadi, wakaja Hebroni wenye moyo mkamilifu, ili kumtawaza Daudi awe mfalme juu ya Israeli wote; tena wote waliosalia wa Israeli nao walikuwa na moyo mmoja kwamba wamtawaze Daudi.

1 Mambo ya Nyakati 12:39

Nao walikuwako huko pamoja na Daudi siku tatu, wakila na kunywa; kwani ndugu zao walikuwa wamewaandalia tayari.

1 Mambo ya Nyakati 12:40

Zaidi ya hayo, wale waliokuwa karibu nao, hata mpaka kwa Isakari, na Zabuloni, na Naftali, wakaleta chakula juu ya punda, na ngamia, na nyumbu, na ng'ombe, vyakula vya unga, mikate ya tini, na vichala vya zabibu kavu, na divai, na mafuta, na ng'ombe, na kondoo tele; kwa kuwa kulikuwa na furaha katika Israeli.