1 Mambo ya Nyakati Mlango 22 1st Chronicles

1 Mambo ya Nyakati 22:1

Ndipo Daudi akasema, Hii ndiyo nyumba ya Bwana Mungu, na hii ndiyo madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa kwa Israeli.

1 Mambo ya Nyakati 22:2

Basi Daudi akaamuru wakusanyike wageni waliokuwa katika nchi ya Israeli; akaweka waashi wachonge mawe ili kujenga nyumba ya Mungu.

1 Mambo ya Nyakati 22:3

Daudi akaweka akiba tele ya chuma kwa misumari ya tarabe za malango, na kwa mafungo; na ya shaba akiba tele isiyo na uzani;

1 Mambo ya Nyakati 22:4

na mierezi isiyo na idadi; kwa kuwa Wasidoni na watu wa Tiro wakamletea Daudi mierezi tele.

1 Mambo ya Nyakati 22:5

Daudi akasema, Sulemani mwanangu akali ni mchanga bado, na mwororo, nayo nyumba atakayojengewa Bwana haina budi kuwa nzuri mno, yenye sifa na yenye fahari katika nchi zote; kwa hiyo mimi nitaiwekea akiba. Basi Daudi akaweka akiba tele kabla hajafa.

1 Mambo ya Nyakati 22:6

Ndipo akamwita Sulemani mwanawe, akamwagiza amjengee Bwana, Mungu wa Israeli, nyumba.

1 Mambo ya Nyakati 22:7

Daudi akamwambia Sulemani mwanawe, Kwangu mimi nia yangu ilikuwa kujenga nyumba kwa ajili ya jina la Bwana, Mungu wangu.

1 Mambo ya Nyakati 22:8

Lakini neno la Bwana likanijia, kusema, Wewe umemwaga damu nyingi, na vita vikubwa umevifanya; wewe hutajenga nyumba kwa ajili ya jina langu, kwa sababu umemwaga damu nyingi juu ya nchi machoni pangu;

1 Mambo ya Nyakati 22:9

tazama, utazaliwa mwana, atakayekuwa mtu wa kustarehe; nami nitamstarehesha mbele ya adui zake pande zote; kwani jina lake litakuwa Sulemani, nami nitawapa Israeli amani na utulivu siku zake ;

1 Mambo ya Nyakati 22:10

huyo ndiye atakayejenga nyumba kwa ajili ya jina langu; naye atakuwa mwanangu, nami nitakuwa babaye; nami nitakifanya imara milele kiti cha ufalme wake juu ya Israeli.

1 Mambo ya Nyakati 22:11

Sasa mwanangu, Bwana na awe pamoja nawe; ukafanikiwe, na kuijenga nyumba ya Bwana, Mungu wako, kama alivyonena kwa habari zako.

1 Mambo ya Nyakati 22:12

Bwana na akupe busara na akili, akakuagizie juu ya Israeli; ili uishike torati ya Bwana, Mungu wako.

1 Mambo ya Nyakati 22:13

Ndipo utakapofanikiwa, ukiangalia kuzitenda amri, na hukumu, Bwana alizomwagizia Musa juu ya Israeli; uwe hodari, na wa moyo mkuu; usiogope wala usifadhaike.

1 Mambo ya Nyakati 22:14

Basi sasa, tazama, katika shida yangu, nimeiwekea akiba nyumba ya Bwana, talanta elfu mia za dhahabu, na talanta elfu elfu za fedha; na shaba na chuma isiyo na uzani; kwa vile zilivyo tele; miti tena na mawe nimeweka akiba, nawe utaweza kuongeza.

1 Mambo ya Nyakati 22:15

Tena kwako kuna mafundi wengi, wenye kuchonga na kufanyiza kazi ya mawe na miti, na kila aliye mstadi kwa kazi yo yote;

1 Mambo ya Nyakati 22:16

ya dhahabu, ya fedha, na ya shaba, na ya chuma, hapana hesabu; basi inuka ushike kazi, naye Bwana na awe pamoja nawe.

1 Mambo ya Nyakati 22:17

Tena Daudi akawaamuru wakuu wote wa Israeli, kwamba wamsaidie Sulemani mwanawe, akisema,

1 Mambo ya Nyakati 22:18

Je! Si Bwana, Mungu wenu, aliye pamoja nanyi? Na kuwastarehesha pande zote? Kwa kuwa wenyeji wa nchi amewatia mkononi mwangu; nayo nchi imetiishwa mbele za Bwana, na mbele ya watu wake.

1 Mambo ya Nyakati 22:19

Basi sasa jitieni moyo na nia kumtafuta Bwana, Mungu wenu; inukeni basi, mkamjengee Bwana Mungu mahali patakatifu, ili kulileta sanduku la agano la Bwana, na vyombo vitakatifu vya Mungu, ndani ya nyumba itakayojengwa kwa ajili ya jina la Bwana.