1 Mambo ya Nyakati Mlango 21 1st Chronicles

1 Mambo ya Nyakati 21:1

Tena shetani akasimama juu ya Israeli, akamshawishi Daudi kuwahesabu Israeli.

1 Mambo ya Nyakati 21:2

Basi Daudi akamwambia Yoabu, na wakuu wa watu, Nendeni kawahesabu Israeli toka Beer-sheba mpaka Dani; mkanipashe habari, nipate kujua jumla yao.

1 Mambo ya Nyakati 21:3

Naye Yoabu akasema, Bwana na awaongeze watu wake mara mia hesabu yao ilivyo; lakini, bwana wangu mfalme, si wote watumishi wa bwana wangu? Mbona basi bwana wangu analitaka neno hili? Mbona awe sababu ya hatia kwa Israeli?

1 Mambo ya Nyakati 21:4

Lakini neno la mfalme likawa na nguvu juu ya Yoabu. Kwa hiyo Yoabu akaenda zake, akapita kati ya Israeli wote, akafika Yerusalemu.

1 Mambo ya Nyakati 21:5

Naye Yoabu akamtolea Daudi jumla ya hesabu ya watu. Na hao wote wa Israeli walikuwa watu elfu mara elfu, na mia elfu, wenye kufuta panga; na wa Yuda watu mia nne na sabini elfu, wenye kufuta panga.

1 Mambo ya Nyakati 21:6

Lakini Lawi na Benyamini hakuwahesabu miongoni mwao; kwa sababu neno la mfalme limemchukiza Yoabu.

1 Mambo ya Nyakati 21:7

Neno hilo likawa baya machoni pa Mungu; kwa hiyo akawapiga Israeli.

1 Mambo ya Nyakati 21:8

Naye Daudi akamwambia Mungu, Nimekosa sana, kwa kuwa nimelifanya jambo hili; lakini sasa uuondolee mbali, nakusihi, uovu wa mtumwa wako; kwani nimefanya upumbavu kabisa.

1 Mambo ya Nyakati 21:9

Naye Bwana akanena na Gadi, mwonaji wake Daudi, akisema,

1 Mambo ya Nyakati 21:10

Nenda ukanene na Daudi, ukisema, Bwana asema hivi, Nakuwekea mambo matatu; katika haya ujichagulie moja, nikutendee hilo.

1 Mambo ya Nyakati 21:11

Basi Gadi akamwendea Daudi, akamwambia, Bwana asema hivi, Kubali upendavyo;

1 Mambo ya Nyakati 21:12

miaka mitatu ya njaa; au miezi mitatu kuangamia mbele ya adui zako, ukipatwa na upanga wa watesi wako; au siku tatu upanga wa Bwana, yaani tauni katika nchi, na malaika wa Bwana akiharibu kati ya mipaka yote ya Israeli. Haya basi ufikiri ni jawabu gani nimrudishie yeye aliyenituma.

1 Mambo ya Nyakati 21:13

Naye Daudi akamwambia Gadi, Nimeingia katika mashaka sana; basi sasa na nianguke katika mkono wa Bwana; kwa kuwa rehema zake ni nyingi sana; wala nisianguke katika mkono wa wanadamu.

1 Mambo ya Nyakati 21:14

Basi Bwana akawaletea Israeli tauni; nao wakaanguka wa Israeli watu sabini elfu.

1 Mambo ya Nyakati 21:15

Naye Mungu akatuma malaika aende Yerusalemu ili auangamize; naye alipokuwa tayari kuangamiza, Bwana akatazama, akaghairi katika mabaya, akamwambia malaika aharibuye, Basi yatosha; sasa ulegeze mkono wako. Naye malaika wa Bwana akasimama karibu na kiwanja cha kupuria cha Arauna, Myebusi.

1 Mambo ya Nyakati 21:16

Daudi akainua macho yake, akamwona huyo malaika wa Bwana amesimama kati ya nchi na mbingu, naye alikuwa na upanga wazi mkononi, umenyoshwa juu ya Yerusakmu. Ndipo Daudi na wazee wakaanguka kifulifuli, nao wamevaa nguo za magunia.

1 Mambo ya Nyakati 21:17

Daudi akamwambia Mungu, Je! Si mimi niliyeamuru watu wahesabiwe? Naam, mimi ndimi niliyekosa, na kufanya yaliyo maovu sana; lakini kondoo hawa, wamefanya nini? Mkono wako, nakusihi, Ee Bwana, Mungu wangu, na uwe juu yangu, na juu ya nyumba ya babangu; wala si juu ya watu wako, hata wao wapigwe.

1 Mambo ya Nyakati 21:18

Ndipo huyo malaika wa Bwana akamwamuru Gadi kwamba amwambie Daudi, ya kuwa Daudi akwee, akamwinulie Bwana madhabahu katika kiwanja cha kupuria cha Arauna, Myebusi.

1 Mambo ya Nyakati 21:19

Basi Daudi akakwea sawasawa na neno la Gadi, alilolinena kwa jina la Bwana.

1 Mambo ya Nyakati 21:20

Arauna alipogeuka, na kumwona yule malaika, ndipo yeye na wanawe wanne waliokuwa pamoja naye wakajificha. Naye Arauna alikuwa akipura ngano.

1 Mambo ya Nyakati 21:21

Basi Daudi alipokuwa akimjia Arauna, Arauna akatazama, akamwona Daudi, akatoka katika kile kiwanja, akamsujudia Daudi kifulifuli hata nchi.

1 Mambo ya Nyakati 21:22

Ndipo Daudi akamwambia Arauna, Unipe mahali pa kiwanja hiki, ili kwamba nimjengee Bwana madhabahu hapa; kwa thamani yake kamili utanipa; ili kwamba tauni izuiliwe katika watu.

1 Mambo ya Nyakati 21:23

Arauna akamwambia Daudi, Ujitwalie, na bwana wangu mfalme na afanye yaliyo mema machoni pake; tazama, ng'ombe kwa sadaka za kuteketezwa, na vyombo vya kupuria kwa kuni, na ngano kwa sadaka ya unga, nazitoa; zote nazitoa.

1 Mambo ya Nyakati 21:24

Mfalme Daudi akamwambia Arauna, La, sivyo, lakini kweli nitazinunua kwa thamani yake kamili; kwani sitamtwalia Bwana kilicho chako, wala kutoa sadaka ya kuteketezwa isiyo na gharama.

1 Mambo ya Nyakati 21:25

Basi Daudi akampimia Arauna thamani ya mahali pale shekeli mia sita za dhahabu kwa uzani

1 Mambo ya Nyakati 21:26

Kisha Daudi akamjengea Bwana madhabahu huko, akatoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani, akamlingana Bwana; naye akamwitikia kutoka mbinguni kwa moto juu ya madhabahu hiyo ya sadaka ya kuteketezwa.

1 Mambo ya Nyakati 21:27

Bwana naye akamwamuru malaika; naye akaurudisha upanga wake alani mwake tena.

1 Mambo ya Nyakati 21:28

Wakati huo, Daudi alipoona ya kwamba Bwana amemwitikia katika kiwanja cha Arauna, Myebusi, ndipo hutoa dhabihu huko.

1 Mambo ya Nyakati 21:29

Kwa maana ile maskani ya Bwana, aliyoifanya Musa jangwani, na madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, vilikuwapo wakati huo mahali pa juu pa Gibeoni.

1 Mambo ya Nyakati 21:30

Wala Daudi hakuweza kwenda mbele yake ili kumwuliza Mungu; kwa sababu aliona hofu kwa ajili ya upanga wa yule malaika wa Bwana.