1 Mambo ya Nyakati Mlango 10 1st Chronicles

1 Mambo ya Nyakati 10:1

Basi Wafilisti wakapigana juu ya Israeli; nao watu wa Israeli wakakimbia mbele ya Wafilisti, wakaanguka wameuawa katika mlima Gilboa.

1 Mambo ya Nyakati 10:2

Nao Wafilisti wakamfuatia sana Sauli na wanawe; Wafilisti wakawaua Yonathani, na Abinadabu, na Malkishua, wana wa Sauli.

1 Mambo ya Nyakati 10:3

Tena vita vilikuwa vikali sana juu ya Sauli, na wapiga upinde wakampata; hata akafadhaika sana kwa sababu ya wapiga upinde.

1 Mambo ya Nyakati 10:4

Ndipo Sauli akamwambia yule mchukua silaha zake, Futa upanga wako, unichome nao, wasije watu hawa wasiotahiriwa wakanisimanga. Lakini huyo mchukua silaha zake akakataa; kwa sababu aliogopa sana. Basi Sauli akautwaa upanga wake, akauangukia.

1 Mambo ya Nyakati 10:5

Na mchukua silaha zake alipoona ya kuwa Sauli amekufa, yeye naye akauangukia upanga wake, akafa.

1 Mambo ya Nyakati 10:6

Hivyo Sauli akafa, na wanawe watatu; na nyumba yake yote wakafa pamoja.

1 Mambo ya Nyakati 10:7

Kisha watu wote wa Israeli, waliokuwa huko bondeni, walipoona ya kuwa wamekimbia, na ya kuwa Sauli na wanawe wamekufa, wakaiacha miji yao, wakakimbia; nao Wafilisti wakaenda wakakaa humo.

1 Mambo ya Nyakati 10:8

Hata ikawa siku ya pili yake Wafilisti walipokwenda kuwateka nyara hao waliouawa, walimwona Sauli na wanawe wameanguka juu ya mlima Gilboa.

1 Mambo ya Nyakati 10:9

Wakamvua mavazi, wakamtwalia kichwa, na silaha zake, kisha wakapeleka wajumbe kwenda nchi ya Wafilisti pande zote, ili kutangaza habari kwa sanamu zao, na kwa watu.

1 Mambo ya Nyakati 10:10

Wakaziweka silaha zake nyumbani mwa miungu yao, wakakikaza kichwa chake nyumbani mwa Dagoni.

1 Mambo ya Nyakati 10:11

Na watu wote wa Yabesh-gileadi waliposikia hayo yote Wafilisti waliyomtenda Sauli,

1 Mambo ya Nyakati 10:12

wakainuka mashujaa wote, wakautwaa mwili wake Sauli, na miili ya wanawe, wakaileta Yabeshi, wakaizika mifupa yao chini ya mwaloni huko Yabeshi, nao wakafunga muda wa siku saba.

1 Mambo ya Nyakati 10:13

Basi Sauli alikufa kwa sababu ya kosa lake alilomkosa Bwana, kwa sababu ya neno la Bwana, asilolishika; na tena kwa kutaka shauri kwa mwenye pepo wa utambuzi, aulize kwake,

1 Mambo ya Nyakati 10:14

asiulize kwa Bwana; kwa hiyo akamwua, na ufalme akamgeuzia Daudi, mwana wa Yese.