Hesabu Mlango 32 Numbers

Hesabu 32:1

Basi wana wa Reubeni, na hao wana wa Gadi, walikuwa na wanyama wa mifugo wengi sana; nao walipoona nchi ya Yazeri, na nchi ya Gileadi, ya kuwa mahali hapo palikuwa ni mahali pa kuwafaa wanyama;

Hesabu 32:2

hao wana wa Gadi, na wana wa Reubeni, wakamwendea Musa na Eleazari kuhani, na wakuu wa mkutano, wakanena nao, wakisema,

Hesabu 32:3

Atarothi, na Diboni, na Yazeri, na Nimra, na Heshboni, na Eleale, na Sebamu, na Nebo na Beoni,

Hesabu 32:4

nchi hiyo ambayo Bwana aliipiga mbele ya mkutano wa Israeli, ni nchi ifaayo kwa mfugo wa wanyama, nasi watumishi wako tuna wanyama.

Hesabu 32:5

Wakasema, Kama tumepata kibali mbele ya macho yako, sisi watumishi wako na tupewe nchi hii iwe milki yetu; usituvushe mto wa Yordani.

Hesabu 32:6

Musa akawaambia wana wa Gadi na wana wa Reubeni, Je! Ndugu zenu waende vitani nanyi mtaketi hapa?

Hesabu 32:7

Mbona mwawavunja mioyo yao wana wa Israeli, wasivuke na kuingia nchi hiyo ambayo Bwana amewapa?

Hesabu 32:8

Ndivyo walivyofanya baba zenu, hapo nilipowatuma kutoka Kadesh-barnea ili waende kuiangalia hiyo nchi.

Hesabu 32:9

Kwa kuwa walipokwea na kuingia bonde la Eshkoli, na kuiona nchi, wakawavunja mioyo wana wa Israeli, ili wasikwee kuingia nchi Bwana aliyowapa.

Hesabu 32:10

Na siku ile hasira za Bwana ziliwaka, naye akaapa, akisema,

Hesabu 32:11

Hakika yangu hapana mtu mmoja katika wale watu waliotoka Misri, tangu huyo aliyepata umri wa miaka ishirini, na zaidi, atakayeiona hiyo nchi niliyomwapia Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo; kwa sababu hawakuniandama kwa moyo wote;

Hesabu 32:12

ila Kalebu mwana wa Yefune, Mkenizi, na Yoshua mwana wa Nuni; kwa kuwa wao wamemwandama Bwana kwa moyo wote.

Hesabu 32:13

Na hasira za Bwana ziliwaka juu ya Israeli, naye akawatembeza huku na huku jangwani muda wa miaka arobaini, hata kizazi hicho kizima kilichokuwa kimefanya uovu machoni pa Bwana kikaisha angamia.

Hesabu 32:14

Na tazama, ninyi mmeinuka badala ya baba zenu, maongeo ya watu wenye dhambi, ili kuongeza tena hizo hasira kali za Bwana juu ya Israeli.

Hesabu 32:15

Kwa kuwa mkigeuka msimwandame, yeye atawaacha tena nyikani; nanyi mtawaangamiza watu hawa wote.

Hesabu 32:16

Basi wakamwendea karibu, na kusema, Sisi tutafanya mazizi hapa kwa ajili ya wanyama wetu wa mifugo, na kujenga miji kwa ajili ya watoto wetu;

Hesabu 32:17

lakini sisi wenyewe tutakuwa tayari na silaha zetu kutangulia mbele ya wana wa Israeli, hata tutakapowafikisha mahali pao; na watoto wetu watakaa katika hiyo miji yenye maboma, kwa sababu ya wenyeji wa nchi.

Hesabu 32:18

Sisi hatutarudia nyumba zetu, hata wana wa Israeli watakapokuwa wamekwisha kurithi kila mtu urithi wake.

Hesabu 32:19

Kwa kuwa sisi hatutarithi pamoja nao huko ng'ambo ya pili ya Yordani, huko mbele; kwa sababu urithi wetu umetuangukia upande huu wa Yordani kwa mashariki.

Hesabu 32:20

Basi Musa akawaambia, Kama mtafanya jambo hili; kama mtajivika silaha, ili kutangulia mbele ya Bwana mwende vitani,

Hesabu 32:21

tena kama kila mume wa kwenu mwenye kuchukua silaha atavuka Yordani mbele ya Bwana, hata atakapokuwa amekwisha watoa adui zake mbele yake,

Hesabu 32:22

na hiyo nchi kushindwa mbele za Bwana; ndipo baadaye mtarudi, nanyi mtakuwa hamna hatia mbele za Bwana, wala kwa Israeli; na nchi hii itakuwa milki yenu mbele za Bwana.

Hesabu 32:23

Lakini kama hamtaki kufanya neno hilo, ninyi mmefanya dhambi mbele za Bwana, nanyi jueni ya kwamba hiyo dhambi yenu itawapata hapana budi.

Hesabu 32:24

Basi, jengeni miji kwa ajili ya watoto wenu, na mazizi kwa ajili ya kondoo zenu; mkayafanye hayo mliotamka kwa vinywa vyenu.

Hesabu 32:25

Ndipo wana wa Gadi na wana wa Reubeni wakanena na Musa, na kumwambia, Sisi watumishi wako tutafanya kama wewe bwana wangu utuagizavyo.

Hesabu 32:26

Watoto wetu, na wake wetu, na kondoo zetu, na ng'ombe zetu wote, watakuwa hapo katika miji ya Gileadi;

Hesabu 32:27

lakini sisi watumishi wako tutavuka, kila mume aliyevaa silaha za vita, mbele za Bwana, tuende vitani, kama wewe bwana wangu usemavyo.

Hesabu 32:28

Basi Musa akamwagiza Eleazari kuhani, na Yoshua mwana wa Nuni, na wakuu wa nyumba za mababa za kabila za wana wa Israeli, katika habari za watu hao.

Hesabu 32:29

Musa akawaambia, Kwamba wana wa Gadi, na wana wa Reubeni, watavuka Yordani pamoja nanyi, kila mtu aliyevaa silaha kwa vita, mbele za Bwana, nayo nchi itashindwa mbele yenu; ndipo mtawapa nchi ya Gileadi kuwa milki yao;

Hesabu 32:30

lakini ikiwa hawataki kuvuka pamoja nanyi, hali wamevaa silaha zao, ndipo watakuwa na milki zao kati yenu katika nchi ya Kanaani.

Hesabu 32:31

Wana wa Gadi, na wana wa Reubeni, wakajibu na kusema, Kama Bwana alivyotuambia sisi watumishi wako, ndivyo tutakavyofanya.

Hesabu 32:32

Tutavuka, hali tumevaa silaha zetu, mbele za Bwana, kuingia nchi ya Kanaani, nayo milki ya urithi wetu itakuwa ng'ambo ya pili ya Yordani.

Hesabu 32:33

Basi Musa akawapa wao, maana, wana wa Gadi, na wana wa Reubeni, na hiyo nusu ya kabila ya Manase, mwana wa Yusufu, ufalme wa Sihoni mfalme wa Waamori, na ufalme wa Ogu mfalme wa Bashani, hiyo nchi, kama miji yao ilivyokuwa, pamoja na mipaka yake, maana, miji ya hiyo nchi iliyozunguka kotekote.

Hesabu 32:34

Kisha wana wa Gadi wakajenga Diboni, na Atarothi, na Aroeri;

Hesabu 32:35

na Atrothi-shofani, na Yazeri, na Yogbeha;

Hesabu 32:36

na, Beth-nimra, na Beth-harani; miji yenye maboma, na mazizi ya kondoo.

Hesabu 32:37

Na wana wa Reubeni wakajenga Heshboni, na Eleale, na Kiriathaimu;

Hesabu 32:38

na Nebo, na Baal-meoni, (majina yake yalikuwa yamegeuzwa) na Sibma; nao wakaiita miji waliyoijenga majina mengine.

Hesabu 32:39

Na wana wa Makiri mwana wa Manase wakaenda Gileadi, na kuitwaa, na kuwapokonya Waamori waliokuwamo humo.

Hesabu 32:40

Basi Musa akampa Makiri, mwana wa Manase, Gileadi, naye akakaa humo.

Hesabu 32:41

Kisha Yairi mwana wa Manase akaenda na kuvitwaa vijiji vya Gileadi. Akaviita jina lake Hawoth-yairi.

Hesabu 32:42

Kisha Noba akaenda na kutwaa Kenathi na vijiji vyake, na kuita jina lake Noba, kwa kuandama jina lake mwenyewe.