Hesabu Mlango 24 Numbers

Hesabu 24:1

Basi Balaamu alipoona ya kuwa ilimpendeza Bwana kuwabariki Israeli, hakwenda, kama hapo kwanza, ili kutafuta uchawi, bali alielekeza uso wake jangwani.

Hesabu 24:2

Balaamu akainua macho yake akawaona Israeli wamekaa kabila kabila; roho ya Mungu ikamjia.

Hesabu 24:3

Akatunga mithali yake, akasema, Balaamu mwana wa Beori asema, Yule mtu aliyefumbwa macho asema;

Hesabu 24:4

Asema, yeye asikiaye maneno ya Mungu, Yeye aonaye maono ya Mwenyezi, Akianguka kifudifudi, amefumbuliwa macho;

Hesabu 24:5

Mahema yako ni mazuri namna gani, Ee Yakobo, Maskani zako, Ee Israeli!

Hesabu 24:6

Mfano wa bonde zimetandwa, Mfano wa bustani kando ya mto, Mfano wa mishubiri aliyoipanda Bwana, Mfano wa mierezi kando ya maji.

Hesabu 24:7

Maji yatafurika katika ndoo zake, Na mbegu zake zitakuwa katika maji mengi. Na mfalme wake ataadhimishwa kuliko Agagi, Na ufalme wake utatukuzwa.

Hesabu 24:8

Mungu amemleta kutoka Misri, Ana nguvu mfano wa nguvu za nyati; Atawameza mataifa walio adui zake, Ataivunja mifupa yao vipande vipande. Atawachoma kwa mishale yake.

Hesabu 24:9

Aliinama, akalala mfano wa simba, Na kama simba mke; ni nani atakayemstusha? Na abarikiwe kila akubarikiye, Na alaaniwe kila akulaaniye.

Hesabu 24:10

Hasira ya Balaki ikawaka juu ya Balaamu akayapiga makofi; Balaki akamwambia Balaamu, Nalikuita ili unilaanie adui zangu, na tazama, umewabariki kabisa mara tatu hizi.

Hesabu 24:11

Basi sasa kimbilia mahali pako; naliazimu kukuheshimu sana; lakini, tazama, Bwana amekuzuilia heshima.

Hesabu 24:12

Balaamu akamwambia Balaki, Je! Sikuwaambia wajumbe wako ulionipelekea, nikisema,

Hesabu 24:13

Kama Balaki angenipa nyumba yake imejaa fedha na dhahabu, siwezi kupita mpaka wa neno la Bwana, kutenda neno jema, wala neno baya, kwa nia yangu mwenyewe; Bwana atakalolinena ndilo nitakalolinena mimi.

Hesabu 24:14

Basi sasa, tazama, ninakwenda kwa watu wangu; haya, nitakuarifu mambo ambayo watu hawa watakayowatenda watu wako siku za mwisho.

Hesabu 24:15

Akatunga mithali yake akasema, Balaamu mwana wa Beori asema, Yule mtu aliyefumbwa macho asema,

Hesabu 24:16

Asema, yeye asikiaye maneno ya Mungu, Na kuyajua maarifa yake Aliye Juu. Yeye aonaye maono ya Mwenyezi, Akianguka kifudifudi, amefumbuliwa macho,

Hesabu 24:17

Namwona, lakini si sasa; Namtazama, lakini si karibu; Nyota itatokea katika Yakobo Na fimbo ya enzi itainuka katika Israeli; Nayo itazipiga-piga pembe za Moabu, Na kuwavunja-vunja wana wote wa ghasia.

Hesabu 24:18

Na Edomu itakuwa milki Seiri pia itakuwa milki, waliokuwa adui zake; Israeli watakapotenda kwa ushujaa.

Hesabu 24:19

Mwenye kutawala atakuja toka Yakobo, Atawaangamiza watakaobaki mjini.

Hesabu 24:20

Kisha akamwangalia Amaleki, akatunga mithali yake, akasema, Amaleki alikuwa ni wa kwanza wa mataifa; Lakini mwisho wake atafikilia uharibifu.

Hesabu 24:21

Kisha akamwangalia Mkeni, akatunga mithali yake, akasema, Makao yako yana nguvu, Na kitundu chako kimewekwa katika jabali.

Hesabu 24:22

Pamoja na haya Wakeni wataangamizwa, Hata Ashuru atakapokuchukua mateka.

Hesabu 24:23

Akatunga mithali yake akasema, Ole wao! Ni nani atakayepona, Mungu atakapofanya haya?

Hesabu 24:24

Lakini merikebu zitakuja kutoka pwani kwa Kitimu, Nazo zitamtaabisha Ashuru, na Eberi zitamtaabisha, Yeye naye atafikilia uharibifu.

Hesabu 24:25

Basi Balaamu akainuka, akaondoka na kurudi mahali pake; Balaki naye akaenda zake.