Hesabu Mlango 14 Numbers

Hesabu 14:1

Mkutano wote wakapaza sauti zao wakalia; watu wakatoka machozi usiku ule.

Hesabu 14:2

Kisha wana wa Israeli wote wakamnung'unikia Musa na Haruni; mkutano wote wakawaambia, Ingekuwa heri kama tungalikufa katika nchi ya Misri, au, ingekuwa heri kama tungalikufa katika jangwa hili.

Hesabu 14:3

Mbona Bwana anatuleta mpaka nchi hii ili tuanguke kwa upanga? Wake zetu na watoto wetu watakuwa mateka; je! Si afadhali turudi Misri?

Hesabu 14:4

Wakaambiana, Na tumweke mtu mmoja awe akida, tukarudi Misri.

Hesabu 14:5

Ndipo Musa na Haruni wakaanguka kifudifudi mbele ya mkutano wa kusanyiko la wana wa Israeli.

Hesabu 14:6

Na Yoshua mwana wa Nuni, na Kalebu mwana wa Yefune, waliokuwa miongoni mwao walioipeleleza nchi, wakararua nguo zao;

Hesabu 14:7

wakanena na mkutano wote wa wana wa Israeli wakasema, Nchi ile tuliyopita kati yake ili kuipeleleza, ni nchi njema mno ya ajabu.

Hesabu 14:8

Ikiwa Bwana anatufurahia, atatuingiza katika nchi hii atupe iwe yetu, nayo ni nchi yenye wingi wa maziwa na asali.

Hesabu 14:9

Lakini msimwasi Bwana, wala msiwaogope wale wenyeji wa nchi, maana wao ni chakula kwetu; uvuli uliokuwa juu yao umeondolewa, naye Bwana yu pamoja nasi; msiwaogope.

Hesabu 14:10

Lakini mkutano wote wakaamuru wapigwe kwa mawe. Ndipo utukufu wa Bwana ukaonekana katika hema ya kukutania, mbele ya wana wa Israeli wote.

Hesabu 14:11

Bwana akamwuliza Musa, Je! Watu hawa watanidharau hata lini? Wasiniamini hata lini? Nijapokuwa nimefanya ishara hizo zote kati yao.

Hesabu 14:12

Nitawapiga kwa tauni, na kuwaondolea urithi wao, nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, kisha yenye nguvu kuliko wao.

Hesabu 14:13

Basi Musa akamwambia Bwana, Ndipo Wamisri watasikia habari hiyo; kwa kuwa wewe uliwaleta watu hawa kwa uweza wako, kutoka kati yao;

Hesabu 14:14

kisha watawaambia wenyeji wa nchi hii; wamesikia wao ya kuwa wewe Bwana u kati ya watu hawa; maana, wewe Bwana waonekana uso kwa uso, na wingu lako lasimama juu yao, kisha wewe watangulia mbele yao, katika nguzo ya wingu mchana, na katika nguzo ya moto usiku.

Hesabu 14:15

Basi kama wewe ukiwaua watu hawa mfano wa mtu mmoja, ndipo mataifa yaliyosikia habari za sifa zako watakaponena na kusema,

Hesabu 14:16

Ni kwa sababu yeye Bwana hakuweza kuwaleta watu hao kuwatia katika nchi aliyowaapia, kwa ajili ya hayo amewaua nyikani.

Hesabu 14:17

Basi sasa nakusihi sana, uweza wa Bwana wangu na uwe mkuu, kama ulivyonena, uliposema,

Hesabu 14:18

Bwana ni mpole wa hasira, mwingi wa rehema, mwenye kusamehe uovu na makosa, naye hatamfanya mwenye hatia kuwa hana makosa kwa njia yo yote; mwenye kuwapatiliza wana kwa uovu wa baba zao, katika kizazi cha tatu na cha nne.

Hesabu 14:19

Nakusihi, usamehe uovu wa watu hawa, kama ukuu wa rehema yako ulivyo, kama ulivyowasamehe watu hawa, tangu huko Misri hata hivi sasa.

Hesabu 14:20

Bwana akasema, Mimi nimewasamehe kama neno lako lilivyokuwa;

Hesabu 14:21

lakini hakika yangu, kama niishivyo, tena kama dunia hii nzima itakavyojawa na utukufu wa Bwana;

Hesabu 14:22

kwa sababu watu hawa wote, ambao wameuona utukufu wangu na ishara zangu, nilizozitenda huko Misri, na huko jangwani, pamoja na haya wamenijaribu mara hizi kumi, wala hawakuisikiza sauti yangu;

Hesabu 14:23

hakika yangu hawataiona hiyo nchi niliyowaapia baba zao, wala katika hao wote walionidharau hapana atakayeiona;

Hesabu 14:24

lakini mtumishi wangu Kalebu, kwa kuwa alikuwa na roho nyingine ndani yake, naye ameniandama kwa moyo wote, nitamleta yeye mpaka nchi hiyo aliyoingia; na uzao wake wataimiliki.

Hesabu 14:25

Basi Mwamaleki na Mkanaani wakaa katika bonde; kesho geukeni, mkaende jangwani kwa njia iendayo Bahari ya Shamu.

Hesabu 14:26

Kisha Bwana akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia,

Hesabu 14:27

Je! Nichukuane na mkutano mwovu huu uninung'unikiao hata lini? Nimesikia manung'uniko ya wana wa Israeli, waninung'unikiayo.

Hesabu 14:28

Waambieni, Kama niishivyo, asema Bwana, hakika yangu kama ninyi mlivyonena masikioni mwangu, ndivyo nitakavyowafanyia ninyi;

Hesabu 14:29

mizoga yenu itaanguka katika jangwa hili, na wote waliohesabiwa miongoni mwenu, kama jumla ya hesabu yenu, tangu waliopata umri wa miaka ishirini na zaidi, hao walioninung'unikia,

Hesabu 14:30

hakika yangu hamtaingia ninyi katika nchi, ambayo niliinua mkono wangu ya kwamba nitawaketisha humo, isipokuwa Kalebu mwana wa Yefune, na Yoshua mwana wa Nuni.

Hesabu 14:31

Lakini Watoto wenu, ambao mlisema watakuwa mateka, ndio nitakaowaleta na kuwatia ndani, nao wataijua nchi ninyi mliyoikataa.

Hesabu 14:32

Lakini katika habari zenu, mizoga yenu itaanguka katika jangwa hili.

Hesabu 14:33

Kisha watoto wenu watakuwa wachungaji jangwani muda wa miaka arobaini nao watauchukua mzigo wa uasherati wenu, hata mizoga yenu itakapoangamia jangwani.

Hesabu 14:34

Kwa hesabu ya hizo siku mlizoipeleleza ile nchi, yaani, siku arobaini kila siku kuhesabiwa mwaka, mtayachukua maovu yenu, ndiyo miaka arobaini, nanyi mtakujua kufarikana kwangu.

Hesabu 14:35

Mimi Bwana nimekwisha nena, hakika yangu ndilo nitakaloutenda mkutano mwovu huu wote, waliokusanyika juu yangu; wataangamia katika nyika hii, nako ndiko Watakakokufa.

Hesabu 14:36

Kisha hao watu, ambao Musa aliwatuma waipeleleze nchi, waliorudi, na kufanya mkutano wote kumnung'unikia, kwa walivyoleta habari mbaya juu ya nchi,

Hesabu 14:37

watu hao walioileta habari mbaya ya nchi wakafa kwa tauni mbele ya Bwana.

Hesabu 14:38

Lakini Yoshua mwana wa Nuni, na Kalebu mwana wa Yefune, wakabaki hai miongoni mwa wale watu waliokwenda kuipeleleza nchi.

Hesabu 14:39

Kisha Musa akawaambia wana wa Israeli wote maneno haya, na hao watu wakaombolea sana.

Hesabu 14:40

Wakainuka na mapema asubuhi, wakakwea juu ya mlima hata kileleni, wakisema, Tazameni, sisi tupo hapa, nasi tutakwea kwenda mahali Bwana alipotuahidi; kwani tumefanya dhambi.

Hesabu 14:41

Musa akawaambia, Kwa nini ninyi sasa kuyahalifu maagizo ya Bwana? Maana halitafanikiwa jambo hilo.

Hesabu 14:42

Msikwee, kwa kuwa Bwana hamo kati yenu; msipigwe na kuangushwa mbele ya adui zenu.

Hesabu 14:43

Kwa kuwa Mwamaleki na Mkanaani wako mbele yenu, nanyi mtaanguka kwa upanga, kwa sababu mmerudi nyuma msimwandame Bwana, kwa hiyo Bwana hatakuwa pamoja nanyi.

Hesabu 14:44

Lakini walithubutu kukwea mlimani hata kileleni; ila sanduku la agano la Bwana halikutoka humo maragoni, wala Musa hakutoka.

Hesabu 14:45

Ndipo Mwamaleki, na Mkanaani waliokaa huko mlimani, wakatelemka, wakawapiga na kuwaangusha, hata kufikilia Horma.